March 31, 2018

Viongozi wa kisiasa wasipojijengea utamaduni wa kuvumiliana Tanzania itakuwa nchi ya ovyo kabisa kuishi...Nape Moses

SYLA TV YOUTBE
Image result for Nape Moses Nnauye

Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Moses Nnauye(CCM) amesema kuwa viongozi wa kisiasa wasipojijengea utamaduni wa kuvumiliana Tanzania itakuwa nchi ya ovyo kabisa kuishi.
Nape amesema hayo kwenye mtandao wa kijamii huku akitoa salamu za pole kufuatia cha Mzee Victor Kimesera huku akieleza kuwa kwa mzee huyo wanajifunza siasa za kuvumiliana.
Pumzika Mzee Kimesera, kwako tunajifunza siasa za kuvumiliana! Viongozi wa kisiasa tusipojenga Utamaduni wa Kuvumiliana Tanzania itakuwa nchi ya hovyo kabisa kuishi!,“ ameandika Nape katika ukurasa wake wa Twitter.
Victor Kimesera alikuwa ni mmoja wa waasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Waandamanaji saba wa Kipalestina wameuwawa kwa kupigwa risasi na askari wa Israel

Image result for Waandamanaji saba wa Kipalestina

Waandamanaji saba wa Kipalestina wameuwawa kwa kupigwa risasi na askari wa Israel na wengine zaidi ya 450 wamejeruhiwa wakati wa maandamano yaliyofanyika karibu na mpaka kati ya Gaza na Israel, kulingana na msemaji wa Wizara ya Afya ya Gaza, Ashraf al-Qedra.

 Mpalestina mmoja aliuwawa baada ya kupigwa risasi ya tumbo huko mashariki mwa Jabalia katika eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, na vijana wengine wawili waliuwawa baada ya kupigwa risasi kichwani huko mashariki mwa mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.

 Msemaji huyo wa wizara ya afya amesema machafuko yalianza leo asubuhi wakati askari wa Israel waliokuwepo kwenye mpaka kufyatua gesi ya machozi ili kuwatawanya mamia ya Wapalestina waliokuwa wanaelekea kwenye uzio wa mpaka. Kulingana na mashahidi,

 waandamanaji hao waliwarushia askari mawe. Chama cha Hamas kinacho tawala kwenye Ukanda wa Gaza kimeandaa maandamano hayo ili kusisitiza haki ya wakimbizi wa Kipalestina na vizazi vyao ya kurejea Palestina.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kuwepo uchunguzi


 Gaza | Marsch der Rückkehr (Reuters/I. Abu Mustafa)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kuwepo uchunguzi huru na wenye uwazi kuhusu mauaji ya waandamanaji 16 wa Kipalestina, waliouawa na wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza Ijumaa, 30.03.2018.

Usiku wa Ijumaa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao cha dharura mjini New York, kufuatia ombi la Kuwait, lakini hakuna tangazo la pamoja lililoafikiwa kuhusu ghasia zilizojitokeza Ukanda wa Gaza. Makabiliano haya kati ya jeshi la Israel na Wapalestina ndio mabaya zaidi kutokea tangu vita vya mwaka 2014.
''Kuna wasiwasi kwamba hali hii inaweza kuzorota zaidi mnamo siku chache zijazo'', amesema Taye-Brook Zerihoun, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na kuongeza kuwa umoja huo unataka pande husika zijizuie. Msemaji huyo vile vile amesema Umoja wa Mataifa uko tayari  kuzipa msukumo mpya juhudi za mazungumzo kati ya Israel na Wapalestina.
Ufaransa pia imeonya kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa mzozo mpya katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kimabavu na Israel.
Mamia wajeruhiwa
Wizara ya afya katika Ukanda wa Gaza imesema kwamba pamoja na watu 16 waliouawa, wengine 1,400 walikuwa wamejeruhiwa, wakiwemo 750 wenye majeraha ya risasi za moto. Waliosaria walijeruhiwa kwa risasi za mpira.
Ni kwa sababu hiyo kwamba mabalozi wa nchi muhimu katika Baraza la Umoja wa Mataifa waliwakilishwa na wasaidizi wao, na hakuna tangazo lililoafikiwa katika kikao hicho.Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Israel pamoja na Uingereza, zimesema zimesikitika kwamba kikao hicho kimefanyika wakati mbaya, sambamba na siku kuu muhimu ya dini ya Kiyahudi, hali iliyoufanya ujumbe wa Israel katika Umoja wa Mataifa usihudhurie kikao hicho.
Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour amesema amesikitishwa kwamba hakuna tangazo lililotolewa kulaani kile alichokiita, ''mauaji yenye chuki dhidi ya waandamanaji wa amani'', wala wito wowote wa kuwalinda raia wa Kipalestina.
Israel yasema Wapalestina wanaeneza uongo


Israel, kupitia ujumbe wa maandishi uliotumwa na ubalozi wake katika Umoja wa Mataifa, imewashutumu wapalestina kutumia muda ambapo Wayahudi kote duniani wanasherehekea siku muhimu ya Pasaka, ''kueneza uongo dhidi ya Israel''.
Wanajeshi wa Israel wamewafyatulia risasi waandamanaji wa kipalestina waliosogelea mpaka wake ambao umejengewa ukuta imara, na kwa kutumia vifaru walivishambulia vituo vitatu vya chama cha Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Wapalestina wameishutumu Israel kutumia nguvu za ziada katika kuyakandamiza maandamano. Kwa upande wake Israel imeyataja maandamano hayo kama njama ya chama cha Hamas kutaka kufanya mashambulizi ndani ya Israel.

March 30, 2018

Mbaroni kwa kumchinja mkewe


Image result for Mbaroni


POLISI mkoani Katavi inamshikilia mwanamume mwenye umri wa miaka 45, akituhumiwa kumuua mkewe kwa kumchinja kisha kuchimba shimo na kufukia mwili. 
Inadaiwa kuwa mwanamume huyo, mkazi wa Kijiji cha Songambele Kata ya Simbwesa mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Tanganyika Mkoa wa Katavi, alitenda unyama huo miezi mitatu iliyopita huku mwanawe mdogo wa miaka mitano akishuhudia.
Inadaiwa alifanya hivyo, akimtuhumu mkewe mwenye umri wa miaka 31 kuwa ni malaya aliyekubuhu. Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Damas Nyanda hakuwa tayari kutaja majina ya mtuhumiwa huyo, akidai ni kwa sababu za upelelezi wa kipolisi.
Akisimulia mkasa huo, Kamanda Nyanda alisema mwili wa marehemu huyo, uligundulika saa sita mchana juzi katika Kijiji cha Songambele ukiwa umefukiwa shimoni, baada ya kufukiwa miezi mitatu iliyopita.
"Upelelezi wa awali wa kipolisi umebaini kuwa marehemu huyo aliuawa na kufukiwa shimoni humo Januari 15, mwaka huu, baada ya kushambuliwa na mumewe kwa kupigwa na mpini wa jembe na kucharazwa viboko kisha akamnyonga.
“Mume alikuwa akimtuhumu mkewe huyo kuwa ni malaya aliyekubuhu na wakati akimfanyia ukatili huo mkewe, mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka mitano alikuwa katika eneo hilo la tukio akishuhudia kila kitu kilichofanyika,” amesema Kamanda Nyanda.
Inadaiwa kuwa baada ya kufanya mauaji hayo, mwanamume huyo alirejea nyumbani na kuendelea na maisha yake kama kawaida, huku akimtishia mara kwa mara mtoto wake kuwa akivujisha siri hiyo, atakiona cha mtema kuni. Pia alimuelekeza kuwa akiulizwa, aseme kuwa mama yake amesafiri.
Amesema jeshi la polisi lilimtia nguvuni mwanamume huyo juzi na baada ya mahojiano alikiri kufanya mauaji hayo na alikuwa tayari kwenda kuwaonesha polisi alipomfukia mkewe.
Aliwaongoza polisi katika eneo la tukio ambapo alifukua udongo na mwili wa mkewe ulikutwa ukiwa umeshaharibika, na kwa sasa umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, mjini Mpanda.