Mashabiki wa Croatia walisherehekea usiku kucha baada ya taifa lao kuwaondoa England kutoka kwa michuano ya Kombe la Dunia Urusi na kufuzu kwa fainali kwa mara yao ya kwanza kabisa, England waliomboleza.
Croatia walipata ushindi wa 2-1 baada ya mechi kumalizika sare ya 1-1 muda wa ziada.
Mashabiki walijaza uwanja ulio katikati mwa mji mkuu wa Croatia wa Zagreb wakiimba na kupeperusha bendera za taifa hilo. Baadhi walijitumbukiza hadi kwenye chemchemi za maji zinazopamba uwanja huo.
Mabao yalivyofungwa
Kieran Trippier dakika ya 5 Croatia 0-1 England
Ivan Perisic dakika ya 68 Croatia 1-1 England
Mario Mandzukic dakika ya 109 Croatia 2-1 England
Croatia ni taifa la watu milioni nne hivi na ni moja ya mataifa yenye idadi ndogo sana ya watu kuwahi kufika fainali Kombe la Dunia
Watakutana na Ufaransa katika uwanja wa Luzhniki mjini Moscow Jumapili kwa fainali saa tatu usiku saa za Afrika Mashariki.
England watakutana na Ubelgiji mechi ya kuamua atakayemaliza nafasi ya tatu, mechi ambayo itachezewa mjini St Petersburg.
Kwa Croatia kukiwa kicheko na shangwe, kwa raia wa England kulienda masikitiko, huzuni na majonzi.
Hali ilivyokuwa kwa England:
Walianza kwa matumaini baada ya bao kufungwa dakika za kwanza lakini baadaye wakavunjwa moyo.
Katika bustani ya Hyde Park, London, takriban mashabiki 30,000 walifika kutazama England wakicheza nusufainali, mkusanyiko mkubwa wa watu London kutazama mchezo wa kandanda tangu Euro 96.
Post a Comment