SUMAYE : WALIOFIKIRI SITAENDA IKULU HAWANIJUI VIZURI
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amesema watu waliodhani kwamba angeshindwa kuitikia wito wa Rais John Magufuli kwenda Ikulu wakati viongozi wakuu wastaafu wote walipoalikwa watakuwa hawamjui kwani kwenda kwake ilikuwa nafasi muhimu ya kuzungumza na kiongozi huyo kuhusu masuala ya kitaifa.
Sumaye amebainisha hayo wakati akizungumza kwenye kipindi cha Weekend BreakFast kinachorushwa siku ya Jumamosi na East Africa Radio na kusema alifurahi kupata mualiko huo kwani aliona ni fursa muhimu ya yeye kuweza kupata nafasi ya kutoa ushauri wake.
"Nilifurahi sana kupata mualiko wa Ikulu, nilijua nitaweza kupata nafasi ya kusema, niliitumia nafasi ile vizuri sana kumwambia Rais yale ninayoyafikiria wala siyo kumueleza ya kwangu binafsi bali yale ya taifa kwa ujumla. Hivyo waliofikiri tofauti kwamba sitakwenda basi hao ni watu ambao hawanijui vizuri", amesema Sumaye.
Mbali na hayo, Waziri Mkuu huyo Mstaafu amebainisha kwamba sababu kuu iliyomfanya yeye na baadhi ya viongozi wenzake kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) mnamo mwaka 2015 ilikuwa ni kwenda kuongeza nguvu katika chama cha upinzani.
"Tulitoka CCM kuja CHADEMA ili kuongeza nguvu huku ili mabadiliko yatakapotokea yasitokee upande huu mwingine ukiwa na hasira. Vipo vitu vingi ambavyo tumepandisha sana upinzani mpaka sasa", amesisitiza Sumaye.
Julai 03, 2018 Rais Magufuli aliwaalika viongozi wakuu wastaafu wote na kufanya nao mazungumzo Ikulu Jijini Dar es salaam ambapo waalikwa walikuwa ni Rais wastaafu wa awamu zilizopita, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu, Maspika na Majaji Wakuu.
Sumaye alikuwa Waziri Mkuu wa awamu ya tatu katika serikali iliyokuwa ikiiongozwa na Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa na alihama CCM mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu kwa madai ya kwamba anaunga mkono mabadiliko yaliyokuwa yakinadiwa na upinzani.
Post a Comment