Muuaji wa tembo atiwa mbaroni
POLISI mkoani Kigoma inamshikilia Maneno Tanu (26) kwa tuhuma za mauaji ya tembo na kuhusika kwenye shughuli za ujangili.
Meneja wa Kanda wa Pori la Akiba la Muyowosi Kigosi, Aloyce Mganga alisema kuwa mtuhumiwa alikamatwa majira ya saa 11 alfajiri jana katika kijiji cha Kagera Nkanda Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Mganga alisema kuwa awali mtuhumiwa alikamatwa katika msako ulioendeshwa kwa pamoja na polisi na shirika linalojihusisha na kampeni ya kuzuia ujangili la Friedkin Anti Poaching na kufanikiwa kumkatamata mtuhumiwa akiwa na bunduki moja aina ya SMG yenye risasi 98, magazini moja na mtambo wa kutengeneza gobore.
Alisema kuwa kwa wiki mbili walikuwa kwenye msako wa kumtafuta mtu huyo na baada ya kupata fununu yupo kijiji cha Kagera Nkanda walitengeneza mtego kwa kushirikiana na polisi na kufanikiwa kumkamata.
Aidha Meneja huyo alisema kuwa wakati anakamatwa mtuhumiwa hakuwa na nyara yeyote ya serikali lakini baada ya mahojiano alikiri kuhusika na mauaji ya tembo wawili katika pori hilo karibu wiki tatu zilizopita lakini pia alikiri kuwinda wanyama na kuuza nyama bila kuwa na vibali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martini Otieno hakutaka kukiri wala kukanusha habari hiyo badala yake alisema kuwa yuko kwenye ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Yussuf Masauni na kwamba atatoa taarifa baada ya kumaliza shughuli za ziara hiyo.
Post a Comment