Header Ads

Sheria ya dawa za kulevya kung’ata zaidi

         Sheria ya dawa za kulevya kung’ata zaidi



SERIKALI imefanya marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini kwa kuwabana zaidi wafanyabiashara na watumiaji wa dawa hizo pamoja na kuwapa nguvu maofi sa wa mamlaka ya kuzuia na kupambana na dawa hizo ambapo sasa watatumia silaha kupambana na wanaouza dawa hizo.
Kibano hicho kimewekwa kwenye marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2017 yaliyowasilishwa na kupitishwa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama.

Kibano kwa wafanyabiashara wa dawa hizo ni pamoja na kuwekwa katazo na mtu atakayebainika kuwezesha au kusababisha mtu kuwekwa rehani ili kufanikisha biashara ya dawa za kulevya atakabiliwa na adhabu ya kifungo cha maisha.
Pia sheria hiyo sasa imeongeza makosa yatakayokosa dhamana kuwa ni kumiliki mitambo ya kutegeneza dawa za kulevya, kufadhili biashara ya dawa za kulevya na kuwaingiza watoto kwenye biashara na matumizi ya dawa hizo.
“Msingi wa hili ni kudhibiti ongezeko la wafanyabiashara wakubwa kupunguza viwango vya utunzaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini, mfano kokeni na heroini na kutohofia kuendelea kufanya biashara ya bangi na mirungi kwa sababu uwezekano wa kupata dhamana ni mkubwa kutokana na viwango vya uzito uliopo kwenye sheria kwa sasa ni vikubwa ambavyo ndivyo vigezo vya utoaji dhamana,” alisema.
Wafanyabiashara hao wanabanwa kwenye mali zao ambapo sasa badala ya mali za mtuhumiwa kutaifishwa za miaka mitano nyuma, zitataifishwa za miaka 10 nyuma tangu tarehe ya kushtakiwa.
Jenista alisema sasa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Dawa za Kulevya amepewa uwezo wa kushikilia akaunti za benki za watuhumiwa wa dawa hizo kwa muda ili kurahisisha, kuimarisha na kuboresha taratibu za uchunguzi na kuweka uhakika wa fedha haramu kutotoroshwa kwa urahisi au uchunguzi kutoharibiwa.
Alisema serikali itakuwa na mamlaka ya kutaifisha mali zilizo nje ya nchi za mtu aliyetiwa hatiani chini ya sheria hii ya kupambana na dawa za kulevya, kwa mujibu wa taratibu za kimataifa kati ya serikali ya Tanzania na nchi husika.
Marekebisho hayo pia yamewezesha uchukuaji wa maelezo ya watuhumiwa au mashahidi kwa njia za kisasa kama vile rekoda, video na vifaa vya dijitali. Jenista alisema Mahakama za chini zinapewa mamlaka ya kushughulikia makosa ya usafirishaji wa kiasi kidogo cha dawa za kulevya na kemikali bashirifu na hivyo kupunguza msongamano wa kesi Mahakama Kuu.
Kwa sasa mashauri yote ya dawa hizo zenye uzito unaozidi gramu mbili kwa kokeni na heroini, gramu 50 kwa bangi na kilo mbili kwa mirungi hupelekwa Mahakama Kuu.
Waziri huyo alisema sheria hiyo sasa inawapa nguvu maofisa wa mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya kumiliki na kutumia silaha inapobidi na kufafanua “wafanyabiashara kutokana na nguvu ya pesa wanamiliki silaha na kujiwekea kinga ya kiulinzi wakati wote hivyo kufanya mazingira ya kiutendaji ya mamlaka kuwa hatarishi wakati wa ukamataji.”
Kwa upande wa watumiaji wa dawa hizo, faini imetoka Sh milioni 20 au kifungo kisichopungua miaka 20 au vyote kwa pamoja na kuwa faini isiyopungua Sh milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka 30 au vyote kwa pamoja.
Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, Mwenyekiti wake Dk Jasmine Tiisekwa alisema wakati wa kutunga kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo, serikali ione umuhimu wa kuongeza pombe aina ya viroba na dawa nyingine za binadamu ambazo zinaweza kutumiwa kama dawa za kulevya ili ziwe sehemu ya orodha ya dawa za kulevya ili kudhibiti mbinu mpya za kuzalisha dawa hizo nchini.
Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Masoud Abdallah Salim alisema upinzani unapingana na ofisa wa mamlaka ya kudhibiti dawa za kulevya kuruhusiwa kutumia silaha kwani hawana mafunzo ya kipolisi na wanaweza kutumia silaha vibaya.

No comments