TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, mwishoni mwa wiki iliyopita ilicheza na Benin katika mchezo wa kimataifa wa kirafi ki uliopo katika kalenda ya Fifa, Shirikisho la Kimataifa la Soka.
Mechi hizo zilizomo katika kalenda ya Fifa ni muhimu sana, kwani zinasaidia kujua timu ya taifa husika iko katika nafasi gani katika viwango vya ubora vya shirikisho hilo, ambavyo hutolewa kila mwezi.
Tanzania, yaani Taifa Stars ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Benin ugenini na sare hiyo inaweza kuipandisha kidogo Taifa Stars, ambayo iko katika nafasi ya 136 katika viwango vya mwezi uliopita, ambavyo vilitolewa Oktoba 16.
Katika viwango hivyo vya Oktoba, wenzetu Benin wenyewe wako katika nafasi ya 79 na inaonekana kuwa waliipata nafasi hiyo baada ya kupanda kwa nafasi tisa. Tanzania yenyewe ilipata nafasi hiyo ya 136 baada ya kuporoma kwa nafasi 19.
Hongera Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kujitahidi kuipatia Taifa Stars mechi za kimataifa za kirafi ki na hii itasaidia siyo tu kujua nafasi yetu katika viwango vya Fifa, ila pia itawawezesha wachezaji wetu kupata uzoefu wa mechi za kimataifa.
Nchi yetu ina vipaji vingi katika michezo mbalimbali na hasa soka, lakini kinachokosekana ni kutoibuliwa au kuendelezwa tofauti na wenzetu wanavyofanya. Mechi hizo za kimataifa za mara kwa mara zitawasaidia sana wachezaji wetu kutokuwa wageni na vitu au wachezaji mbalimbali wakubwa watakapokuwa wakishiriki mashindano fulani makubwa Afrika na dunia kwa ujumla.
Huko nyuma tuliona wachezaji wetu baadhi yao walikuwa wakishangaa hata viwanja vya wenzetu jinsi vilivyo vikubwa na vizuri, lakini kwa sasa hilo halipo tena, kwani hata sisi tuna uwanja unaofanana na vile vya Ulaya kwa ubora wa sehemu ya kuchezea na mahali pa kukaa watazamaji.
Hivyo kwa upande wa kuipatia Taifa Stars mechi za kimataifa za kirafi ki, TFF wanastahili pongezi kubwa kwa kuipatia Taifa Stars mechi hizo karibu kila mwezi. Hata hivyo, sasa wakati umefi ka kwa TFF kuhakikisha kila tunapocheza na timu, basi iwe iko juu yetu katika kiwango cha kimataifa ili tuweze kujifunza kitu kutoka kwa wenzetu hata kama tutafungwa.
Muhimu ni kuiandaa vizuri timu yetu kwa ajili ya kucheza na timu zenye uwezo zaidi yetu ili tuweze kuambulia kitu fulani na siyo kucheza na timu zilizopo chini yetu. Mchezo dhidi ya Benin angalau tulicheza na wenzetu waliopo juu yetu, hivyo hapo tunaweza kupanda kidogo licha ya kutoka sare.
Inajulikana kuwa wakati fulani ni ngumu kucheza na timu zenye viwango vya juu kwani nazo zimekuwa zikilinga kucheza na timu ndogo na kutaka kucheza na wakubwa wenzao ili wafaidike na mechi hizo kwa kupata ushindani na kujifunza kitu kutoka kwa wapinzani wao hao.
Hata hivyo, hilo lisiwakatishe tamaa TFF mnachotakiwa kufanya ni bora mkaingia gharama kwa kuzigharamia timu hizo kubwa mradi zikubali kucheza nazo ili timu yetu ifaidike na kitu fulani.
Taifa Stars iandaliwe vizuri kwa ajili ya mashindano yajayo ya kimataifa ili siku moja Tanzania iweze kushiriki fainali za Kombe la Dunia na lile la Mataifa ya Afrika (Afcon). Kwa mara ya mwisho Tanzania ilishiriki mashindano ya Afcon mwaka 1980 nchini Nigeria na tangu wakati huo tumekuwa tukiishia katika hatua ya kufuzu tu na kushindwa kucheza mashindano hayo au fainali za Kombe la Dunia. TFF jitahidini na msichoke kuiandaa timu hiyo pamoja na zingine za taifa ili Tanzania iweze kurejea katika mashindano ya kimataifa.
Post a Comment