Bundesliga yarejea kwa kishindo
Msimu mpya wa Bundesliga ulianza rasmi kwa kishindo.
Borussia Moenchengladbach ilijigamba kwa kushinda mchuano wa watani wa
jimbo la Rhine, baada ya kuifunga FC Cologne bao moja kwa bila.
Bao lao lilipatikana mapema katika kipindi cha pili wakati Nico
Elvedi alifunga bao safi baada ya kupokea krosi kutoka kwa Ibrahima
Traore. Matthias Ginter ni beki wa Gladbach "michuano ya dabi huwa
maalum kwa mashabiki na wale wote wanaohusika na klabu. Kuna tofauti.
Iwe ni mtu kuja ofisini kesho na kuweka bendera ya Cologne au Gladbach.
Hii kawaida huwa michezo maalum na mazingira mazuri na ndio maana tuna
furaha kubwa kuwa tumeshinda.
Katika mechi nyingine ya jana,
Freiburg na Eintracht Frankfurt zilianza msimu kwa kutoka sare ya bila
kufungana. Freiburg ilifunga bao katika kipindi cha kwanza, lakini mfumo
wa kutumia video ulifuta bao la Tim Kleindienst baada ya kugundua kuwa
mchezaji mwenzake alikuwa ameotea wakati bao hilo lilifungwa.
Mfumo
huo wa VAR unafanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza katika ligi ya
Ujerumani msimu huu. Ulianza kutumika Ijumaa na Bayern walinufaika kwa
kupewa penalti ambayo Robert Lewandowski alifunga na kuwapa mabingwa hao
watetezi ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Bayer Leverkusen katika mechi ya
ufunguzi.
Kevin-Prince Boateng arejea Bundesliga
Kiungo wa Ghana Kevin-Prince Boateng alicheza mechi yake ya kwanza na Eintracht Frankfurt baada ya kuwa nje ya Bundesliga
kwa miaka miwili alipotupwa nje ya kikosi cha Schalke. Na hapa
anauzungumzia mchuano wa jana. "Nadhani tulionyesha mchezo mzuri.
Tulikuwa imara kabisa katika ulinzi na ni bao pekee lililokosekana.
Tulikuwa na nafasi mbili nzuri ambazo bahati mbaya hatukuzitumia vyema
na hivyo hatujaweza kuchukua pointi tatu leo. Lakini nnaridhishwa na
mchezo wa timu. Hatujaweza kuacha chochote nyuma.
Boateng mwenye
umri wa miaka 30 alikamilisha uhamisho wa haraka haraka kwa kusaini
mkataba wa miaka mitatu na Frankfurt baada ya kuihama klabu ya Las
Palmas ya Uhispania akitaja sababu za kibibafsi.
Katika mechi za
Jumamosi, Borussia Dortmund iliizidi nguvu VfL Wolfsburg kwa kuilaza
tatu bila. Kocha mpya Peter Bosz aliahidi kandanda la kuvutia, la
kushambulia na timu yake, ambayo ilimaliza katika nafasi ya tatu msimu
uliopita iliidhihirisha hilo. Mabao ya BVB yalifungwa na Christian
Pulisic, Marc Bartra na Pierre-Emerick Aubameyang. Msikilize kocha Bosz
"unapaswa kuridhika wakati umeshinda mabao matatu kwa sifuri dhidi ya
Wolfsburg na umekuwa na mchezo mzuri. Sehemu kubwa ya mchezo ilikuwa
nzuri sana, hatukufungwa bao, lazima uridhike.
Ousmane Dembele anaondoka au anabaki?
Na
wakati BVB walishinda bila ya nyota wao Ousmane Dembele, suali ni kuwa
je, anaondoka au atabaki? Afisa mkuu mtendaji wa Dortmund Hans-Joachim
Watzke anasema klabu hiyo haina nia ya kulegeza msimamo wake kuhusiana
na Dembele anayesakwa na Barcelona. Hiyo ina maana kuwa hatua ya
kumwondoa Dembele kwenye shughuli za kikosi cha kwanza baada ya kukosa
kufika mazoezini itaendelea kutekelezwa. Na Dortmund haitapunguza kiasi
cha fedha wanachotaka kupewa kwa ajili ya kumuuza nyota huyo mwenye umri
wa miaka 20.
Kwingineko, Schalke ilianza msimu kwa ushindi wa
mabao mawili kwa bila dhidi ya RB Leipzig ambao walimaliza wa pili msimu
uliopita. Na kwa matokeo hayo, inaonekana kuwa kocha wao chipukizi
Domenico Tedesco amejiandaa kuirejesha klabu hiyo katika kiwango cha
juu. Katika matokeo mengine, Hoffenheim walipata ushindi wa moja bila
dhidi ya Werder Bremen, Hertha Berlin ikaifunga Stuttgart mbili sifuri.
Vladimir Darida ni kiungo wa HSC "nadhani ilikuwa muhimu sana kwetu
kujiamini baada ya kupata pointi tatu katika mechi ya kwanza ya msimu.
Ni mwanzo mzuri, lakini msimu bado ni mrefu na lazima tuweze kucheza
katika kila mtangane kama tilivyocheza leo".
Hanover iliishinda
Mainz moja bila wakati Hamburg ambayo ilinusurika kushushwa daraja msimu
uliopita, iliifunga Ausburg moja bila, huyu hapa kiungo wa Hamburg,
Aaron Hunt. "Unaweza kufikiria nini kingetokea hapa tena kama
hatungekuwa tumeshinda. ndio maana timu imekuwa bora zaidi kwa sababu
inacheza kwa pamoja tena. Lazima niisifie timu. Imejaribu kucheza vizuri
kabisa kwa kujituma. Tumepambana kwelikweli leo na nadhani mwishowe
tulistahili kupata ushindi.
Lakini ushindi huo ulikuwa na gharama
yake baada ya mfungaji wa bao hilo Nicolai Mueller kuumia wakati
akishangilia goli lake na sasa atakuwa mkekani kwa karibu miezi saba
Post a Comment