Grace Mugabe kurejea Zimbabwe
Grace Mugabe kurejea Zimbabwe
Baada ya kupewa kinga ya kidiplomasia na serikali ya
Afrika Kusini, mke wa rais wa Zimbabwe Grace Mugabe alirejea nyumbani
siku ya Jumapili, licha ya miito kwamba ashitakiwe kwa madai ya
kumshabulia mwanamitindo Jo'berg.
Shirika la utangazaji la Zimbabwe ZBC lilimuonyesha Grace Mugabe
akisalimiana na maafisa wa serikali na jeshi katika uwanja wa ndege wa
Harare baada ya kushuka kwenye ndege ya shirika la ndege la Zimbabwe
pamoja na mume wake, ambaye alihudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa
kanda ya kusini mwa Afrika mjini Pretoria. Mugabe na mke wake
hawakuhudhuria mazishi ya kitaifa ya afisa mwandamizi wa chama tawala
katika mji mkuu wa Zimbabwe; kawaida rais anakuwa mgeni rasmi katika
matukio kama hayo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Afrika Kusini,
Maite Nkoana-Mashabane, ilimpa kinga ya kidiplomasia Grace Mugabe
kupitia taarifa iliyochapishwa katika gazeti la serikali lililochapishwa
siku ya Jumapili. Taarifa hiyo iliyosainiwa siku ya Jumamosi, inatambua
"kinga na fursa za mke wa rais wa Zimbabwe, Dk. Grace Mugabe."
Awali
polisi ya Afrika Kusini ilitoa tahadhari ya kiusalama kwenye maeneo ya
mipakani kuhakikisha haondoki bila kutambuliwa, na walisema walikuwa
wanasubiri uamuzi wa serikali kuhusu maombi ya kinga.
Mwanamitindo Gabriella Engels akionyesha jeraha alilolipata baada ya kupigwa kwa waya na mke wa rais wa Zimbabwe, Grace Mugabe.
Chama
kikuu cha upinzani nchini humo, cha Democratic Alliance kimetaka
ufanyike uchunguzi wa bunge kuhusu uamuzi wa serikali kumuachia mke wa
rais wa Zimbabwe kuondoka na kilisema kupitia ukurasa wake wa twitter,
kwamba serikali haikuwa tena na uhalali katika nyanja ya diplomasia ya
kimataifa na inaonyesha kupuuza kabisaa utawala wa sheria.
Kisa chalinganishwa na kuachiwa Hassan al-Bashir 2015
John
Steenhuisen, afisa mwandamizi wa upinzani, alilinganisha namna serikali
ya Afrika Kusini ilivyoshughulikia kesi ya Mugabe na uamuzi wa serikali
kumruhusu Rais wa Sudan Omar al-Bashir kuondoka nchini humo mwaka 2015,
hata wakati alipotakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa madai
ya uhalifu wa kivita, liliripoti shirika la Afrika.
Gabriella
Engels, mwanamitindo mwenye umri wa miaka 20, alisema Grace Mugabe
alimshambulia Agosti 13, kwa kumchapa na waya wa umeme uliomkata kwenye
paji la uso. Likizungumzia habari za kurejea kwa Mugabe nchini Zimbabwe,
kundi linalomwakilisha Engels lilisema Jumapili kwamba litakwenda
mahakamani kuipinga serikali ya Afrika Kusini kuhusu suala la kinga.
"Tutatumia
mkakati wa muda mrefu kuhusu suala hili," alisema Willie Spies,
mwakilishi wa kisheria kutoka kampuni ya AfriForum, ambalo ni shirika
linalowawakilisha Waafrika Kusini weupe wa jamii ya wachache ya
Afrikaner.
"Anaweza kuwa amerudi Zimbabwe, lakini hiyo inaweza
kumaanisha kwamba itakuwa vigumu kwake kuja tena Afrika Kusini huko
mbeleni," Spies alisema. Vyombo vya habari vya serikali ya Zimbabwe
vimekuwa kimya kwa kiasi kikubwa kuhusu kadhia hiyo ya mke wa rais wa
Zimbabwe.
Mke huyo wa rais wa Zimbabwe amekosolewa kwa kuwa na
hasira za haraka na safari za manunuzi makubwa, lakini nyota yake ya
kisiasa inayozidi kupanda imewafanya baadhi wajiulize iwapo anafanya
mikakati ya kumrithi mume wake.
Hivi
karibuni alisema chama tawala cha Zimbabwe kinapaswa kurejesha kipengee
kwenye katiba, kinachosema kwamba mmoja wa makamu wa rais anapaswa kuwa
mwanamke, alimpa changamoto waziwazi mume wake mwenye umri wa miaka 93
atangaze mrithi.
Pia siku ya Jumapili, mmoja wa makamu wawili wa
rais wa Zimbabwe, Phelekezela Mphoko, aliongoza mazishi ya Shuvai Ben
Mahofa, mwanachama mwandamizi wa chama tawala cha Zanu-PF aliefariki
wiki moja iliyopita.
Kuzuwiliana safari za ndege za mashirika ya serikali
Shirika
la ndege la Afrika Kusini wakati huo lilisema Jumapili - saa chache
baada ya Mugabe kurejea mjini Harare - kwamba lilikuwa linarejesha
safari zake kati ya Afrika Kusini na Zimbabwe, baada ya safari hizo
kuzuwiwa na maafisa wa Zimbabwe.
Hatua ya Zimbabwe iliochukuliwa
Jumamosi, ilifuatia kuzuwiwa kwa ndege ya shirika la Zimbabwe katika
uwanja mkuu wa Johannesburg Ijumaa jioni. Ndege hiyo iliruhusiwa kuruka
Jumamosi usiku, walisema maafisa wa usafiri wa anga. HAikuwa bayana
iwapo Mugabe alitumia ndege hiyo hiyo kurejea nchini Zimbabwe.
Mataifa
yote mawili yalisema yameweka vikwazo kwa sababu ndege zilizoathiriwa
hazikuwa na vibali vya operesheni za nje." Willie Spies, wakili
anaemwakilisha mwanamitindo aliesema ameshambuliwa, alisema huenda
mgogoro huo wa safari za ndege ulikuwa njama iliyosanifiwa kuondoa
nadhari kutoka kwenye matatizo ya mke wa rais.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape
Mhariri: Lilian Motono.
Post a Comment