Duterte aahidi polisi waliomuua kijana wa miaka 17 watakwenda jela
Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte, jana ameuhakikishia umma wake
kwamba maafisa wa polisi waliohusika na kifo cha kijana wa kiume
aliyekuwa na umri wa miaka 17 wakati wa operesheni ya kupambana na
madawa ya kulevya watatumikia kifungo jela,
wakikutikana na hatia.
Duterte ameongeza kwamba Idara ya Sheria tayari imeshaiamuru Ofisi ya
Taifa ya Uchunguzi kubaini iwapo maafisa wa polisi walihusika katika
kifo cha, Kian Loyd Delos Santos, kilichotokea wiki iliyopita. Masaa
machache kabla ya hapo,
mamia ya watu waliandamana katika mji mkuu wa
Manila, kupinga kifo cha Delos Santos, ambaye familia yake na marafiki
wamekana kwamba alikuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya. Kampeni ya
kupambana na madawa ya kulevya ya Rais Duterte, ambayo imesababisha vifo
vya maelfu ya watu ndani ya mwaka mmoja, imekuwa ikishutumiwa sana na
makundi ya kutetea haki za binaadamu pamoja na serikali za kigeni.
Post a Comment