Mshukiwa mkuu wa shambulizi la Barcelona atambuliwa
Mshukiwa mkuu wa shambulizi la Barcelona atambuliwa
Polisi nchini Uhispania imemtambua mshukiwa mkuu wa
shambulio la Barcelona. Hayo yanajiri huku msako dhidi ya mshukiwa huyo
anayeaminiwa kuwa raia wa Morocco ukitanuliwa barani Ulaya kwa jumla.
Polisi nchini Uhispania imethibitisha kuwa imemtambua mshukiwa mkuu
wa shambulio la Barcelona lililofanywa mwishoni mwa wiki iliyopita. Hayo
yanajiri huku msako dhidi ya mshukiwa huyo anayeaminiwa kuwa ni raia wa
Morocco ukitanuliwa barani Ulaya kwa jumla. Wakati huohuo idadi ya watu
waliouawa kufuatia shambulizi hilo imefikia 15. Hii ni baada ya polisi
kuupata mwili wa mtu aliyedungwa kisu ndani ya gari linaloaminika
kutumiwa na mshukiwa kutoroka.
Waziri wa jimbo la Catalonia
anayeshughulikia mambo ya ndani Joaquim Fornalisema katika mahojiano
na redio ya jimbo hilo kuwa dalili zote zinaashiria kuwa mshukiwa ni
Younes Abouyaaqoub, aliye na umri wa miaka 22, raia wa Morocco. Aidha
polisi imetoa tahadhari na kusema huenda Abouyaaqoub amejihami na hivyo
ni mtu hatari.
Uchunguzi watanuliwa Ulaya
Maafisa
nchini Uhispania, leo wameiarifu polisi ya Ulaya kuhusu utambulisho wa
mshukiwa huyo, ili kuwezesha uchunguzi na msako dhidi yake barani Ulaya
kwa jumla.
Akizungumza na wanahabari ambapo pia alionesha picha
ya mshukiwa huyo mkuu, afisa mkuu wa polisi wa Catalonia Juan Ignacio
Zoido alisema: "Hadi sasa juhudi za polisi zimelenga kumkamata mtu huyu,
Younes Abouyaaqoub ambaye ametambuliwa kuwa dereva wa lori lilotumiwa
katika shambulizi la Barcelona, na ambaye anasakwa na vyombo vya usalama
vya taifa pamoja na polisi, na ninafikiri ndiyo itakuwa shughuli kuu
katika siku zijazo hadi tumpate."
Inaaminika kuwa Abouyaaqoub
ndiye mshukiwa pekee ambaye hajakamatwa miongoni mwa wengine 12 ambao ni
wa kundi la kigaidi, na huenda yupo Uhispania au ametorokea nchi
nyingine.
Misako Ripoll
Forn
ameongeza kuwa wachunguzi wanaolenga kundi la kigaidi, wamepiga kambi
katika mji wa Ripoll, ambapo misako kadhaa imefanywa katika makaazi ya
watuhumiwa, ikiwemo nyumba ya imamu mmoja kutoka Morocco Abdelbaki Es
Satty ambaye anasemekana aliwapandikiza itikadi kali vijana wa Ripoll .
Imamu
huyo anayeamiwa aliuwawa katika mripuko uliotokea Alcanar siku ya
Jumatano wiki iliyopita, aliwahi kufungwa jela kando na kuwa wakati
mmoja alikuwa pamoja na mshukiwa mkuu anayesakwa sasa kwa tuhuma za
ugaidi. Polisi walipata mitungi 120 ya gesi na vifaa vya kutendeneza
milipuko ndani ya nyumba yake.
Maafisa wa polisi wametangaza pia
kuwa wameupata mwili wa mtu aliyedungwa kisu ndani ya gari linaloaminika
kuwa lilitumiwa na mshukiwa alipokuwa akitoroka kutoka eneo la
shambulizi.
Shambulio la Barcelona lilifuatiwa na jingine kama
hilo eneo la Cambrils saa kadhaa baadaye ambapo polisi waliwaua
washukiwa watano. Hadi sasa Jumla ya watu 15 wameuwawa na 130 kujeruhiwa
katika mashambulio hayo ya Barcelona.
Post a Comment