Marekani na Korea Kusini zaanza mazoezi ya kijeshi
Wanajeshi wa Marekani na Korea Kusini wameanza mazoezi
ya kijeshi ya kila mwaka, baada ya marais wa Marekani na Korea Kaskazini
kujibizana maneno ya kuashiria vita na majaribio mawili ya makombora ya
Korea Kaskazini.
Mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi ya kila mwaka yajulikanayo kama
'Ulchi Freedom Guardian' ambayo kwa kiasi kikubwa yanaendeshwa kwa
kompyuta kwa teknolojia ya kidijitali na kufanyika kila majira ya joto,
yamepokewa kwa hasira na upande wa Korea Kaskazini, ambayo inayatazama
kama mazoezi ya kujitayarisha kwa uvamizi.
Akizungumza na Baraza
lake la mawaziri, Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in, amesema leo kwamba
ushirikiano wa kijeshi kati ya Korea Kusini na Marekani haukusudii
kuongeza mvutano kwenye rasi ya Korea, na ameionya Korea Kaskazini dhidi
ya kulitumia zoezi hilo la kijeshi kama sababu ya kufanya vitendo vya
uchochezi.
"Korea Kaskazini inapaswa kufahamu kwamba kutokana na
uchokozi wake wa mara kwa mara, zoezi la pamoja kati ya Korea Kusini na
Marekani litaendelea. Natumai kuwa maafisa wa serikali zetu pamoja na
wanajeshi wapo tayari kujibu uchokozi wowote ule utakaotokana na zoezi
la mara hii, na nawataka watu wetu kuwa na mshikamano zaidi kuliko
wakati mwengine wowote," amesema Rais, Moon Jae-in, wa Korea Kusini.
Post a Comment