Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga 'ameapishwa kuwa rais wa wananchi wa kenya
Kiapo hicho alilishwa na mbunge wa Ruaraka TJ Kajwang.
Hatahivyo wakuu wa chama hicho akiwemo Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula hawakuwepo wakati wa kiapo hicho kilichochukuliwa katika Bustani ya eneo la Uhuru Park alipoapishiwa.
Akiwa amevalia nguo nyeupe na kofia nyeusi, Raila aliapa kwa kutumia kitabu cha biblia na baadaye kutia saini nakala zilizotumiwa kula kiapo.
''Mimi Raila Odinga naapa kwamba nitalinda taifa kama rais wa wananchi, kwamba nitakuwa mwaminifu. Mungu nisaidie'', alisema katika uwanja wa uhuru Park uliopo katikati ya mji wa Nairobi.
Mashabiki wake waliofika katika uwanja huo mapema alfajiri waliimba na kucheza densi huku wakipiga firimbi.
Raila Odinga aliapishwa na mbunge wa Ruraka TJ Kajwang na aliyekuwa mgombea wa kiti cha Ugavana jijini Nairobi Miguna Miguna.
Hatahivyo haijulikani ni nini atakachofanya kiongozi huyo huyo baada ya kula kiapo kwa kuwa Kenya ina rais Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto.
Alitarajiwa kuapishwa pamoja na naibu wake Kalonzo Musyoka, lakini kiongozi huyo wa chama cha Wiper hakuonekana katika bustani ya Uhuru Park.
Hatahivyo Raila amesema kuwa Kalonzo atakula kiapo baadaye.
"Kalonzo hayuko kwa sababu ya maneno ambayo yalifanyika mtajua baadaye ataapishwa baadaye'', alisema Raila.
Viongozi wengine wawili wa NASA, akiwemo mwenyekiti wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetangula hawakuwepo katika sherehe.
Raila aliwashukuru raia wa Kenya kwa kuuonyesha ulimwengu kwamba umoja wa wananchi hauwezi kusambaratishwa.
''Mamia ya maelfu ya raia wa Kenya wamehudhuria sherehe hii ili kusema kwamba wamechoshwa na wizi wa kura'', alisema.
''Hii ni hatua ya kwanza katika kukabiliana na wizi wa kura .Nawashukuru raia wa Kenya kwa subra na ujasiri wao''
Kiongozi huyo wa chama cha ODM amesema kuwa hatambui kiapo cha urais alichokula rais uhiuru Kenyatta.
Mapema baadhi ya vituo vya redio na televisheni vya Royal Media Services (RMS), vikiwemo runinga ya Citizen TV, vimefungiwa matangazo pamoja na kituo cha televisheni cha NTV kinachomilikiwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG) katika baadhi ya maeneo.
Vituo hivyo vimekuwa vikipeperusha matangazo kuhusu sherehe iliyopangiwa kufanyika leo ya kuapishwa kwa kiongozi wa upinzani Kenya Raila Odinga.
Serikali ilikuwa imetahadharisha vituo vya habari Kenya dhidi ya kupeperusha moja kwa moja hafla hiyo.
Mmoja wa wahariri wakuu wa Citizen Peter Opondo ameambia BBC kwamba maafisa wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) kwamba polisi wakiandamana na polisi walivamia vituo vya kupeperushia matangazo na kuzima matangazo.
Citizen TV ndicho kituo cha runinga kinachoongoza Kenya. Matangazo ya kituo cha NTV yanapatikana pekee kupitia ving'amuzi vya kulipia.
Kituo kingine kikubwa KTN bado kinarusha matangazo
Wakati huohuo hali ilikuwa kama kawaida katika ngome za chama tawala cha cha Jubilee huku raia wengi waliohojiwa katika maeneo ya kati ya Kenya kama vile nyeri wakipinga mpango huo wa kuapishwa kwa Raila wakidai kuwa huenda ukazua fujo.
Vilevile waangalizi wanasema kuwa kuapishwa kwa Raila huenda kukaligawanya taifa hilo zaidi na kuongezea kuwa kufungiwa kwa vyombo vya habari kutaleta wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya demokrasia nchini.
chanzo bbc
Post a Comment