Bayern yapaa juu, Leipzig yayumba
Tunaanza na Bundesliga ambapo Bayern Munich waliupanua
uongozi wao kileleni mwa ligi kuu hadi pointi tatu baada ya Thomas
Muller kufunga goli pekee katika ushindi wao wa 1-0 dhidi ya wenyeji
Borussia Moenchengladbach
Ni ushindi wa sita mfululizo kwa Bayern katika mashindano yote ambapo
walionekana kuutawala mchezo kwa asilimia 70. Lilikuwa bao la pili la
Muller msimu huu na lake la kwanza tangu desemba mwaka jana lakini
amegeuka kuwa mtoa pasi 11 zilizopelekea kufungwa mabao. Huyu hapa
Mueller "Inafuahisha sana kwamba tumeshinda. Pia nimeweza kufunga bao,
hiyo bila shaka inafurahisha. Tumeburudika. Ulikuwa mchuano mkali. Kwa
hivyo leo jumapili jioni ntakuwa hoi. Watu wengine watakuwa katika hali
ya kutulia. Bila shaka lazima tukutane".
Wenyeji Gladbach,
wameteremka hadi nafasi ya 10 baada ya kichapo hicho. Mapema jana,
Schalke 04 ilipanda nafasi mbili juu hadi ya tisa baada ya kupata
ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Mainz. Sead Kolasinac alipachika
wavuni bao hilo la ushindi. "Tulijitahidi sana kusogea nafasi za Europa
League na kushinda mechi ya Bundesliga kabla ya kujiunga na timu ya
taifa. Sasa tunaweza kujiunga na timu ya taifa kwa mechi za kimataifa
bila shinikizo kabla ya kuendelea katika wiki mbili zijazo".
Nambari
mbili kwenye ligi RB Leipzig waliendelea kusambaratika baada ya
kufungwa 3-0 na Werder Bremen siku ya Jumamosi. Kocha Ralph Hassenhtul
amesema ni vyema kukitumia kipindi kinachoanza wiki hii cha michezo ya
kimataifa kujinoa makali kabla ya kuanza kupambana katika mkondo wa
mwisho wa ligi. Kichapo hicho kimewaacha katika nafasi ya pili na pointi
49, ikiwa na tofauti ya pointi tatu mbele ya Dortmund
Wakati huo
huo Cologne waliimarisha nafasi zao za kucheza kandanda la Ulaya msimu
ujao baada ya kuwamiminia mabao manne kwa mawili Hertha Berlin
wanaoshikilia nafasi ya pili. Peter Stöger ni kocha wa Köln "Nna furaha
kubwa sana kwamba tumecheza vizuri sana dhidi ya mpinzani mkali kabisa
ambaye kila mara alikuwa hatari sana. Tulikuwa na nafasi ambazo
tungeweza kufunga mabao zaid. Tumeona tulichotaka, kuwa wajasiri na
matumaini ndani yetu na kushiriki kikamilifu katika mchezo huo na
kujaribu kujikinga. Tulitekeleza vyema kile tulichozungumza".
Mambo hayawaendei vyema vijana wa Leipzig
Ni mechi iliyokuwa muhimu sana kwa mshambuliaji Anthony Modeste aliyetikisa nyavu mara tatu.
Modeste
sasa ana mabao 22 nyuma ya Mshambuliaji wa Borussia Dortmund
Pierre-Emerick Aubameyang ambaye alifunga bao lake la 23 katika ushindi
wao wa Ijumaa usiku wa 1-0 dhidi ya Ingolstadt. Robert Lewandowski ni wa
tatu akiwa na mabao 21.
Wolfsburg waliwafunga washika mkia
Darmstadt 1-0 wakati nambari nne Hoffenheim walipata ushindi wa 1-0 na
sasa wako nyuma ya nambari tatu Borussia Dortmund na tofauti ya pointi
moja pekee. Julian Nagelsmann ni kocha wa Hoffenheim "Leverkusen ina
timu nziri sana, yenye wachezaji wa bei ghali na hivyo bado hawajatimiza
matarajio yao. Lakini bado ni timu kubwa katika Bundesliga. Na hilo pia
nimewaambia wachezaji wangu na mtu anaweza kuona. Katika kipindi cha
kwanza tulikuwa ovyo na mchezo wetu haukuwa sawa. Katika kipindi cha
pili, tulijipanga vyema na tukapata bao safi"
Vita vya juu ya
eneo la kushushwa ngazi vimepamba moto ambapo timu nne zina pointi 29.
Timu hizi ni Mainz, Werder, Augsburg na Wolfsburg. Hamburg ni ya tatu
kutoka nafasi ya mkia. Ingosltadt na Darmstadt sasa zinakodolea macho
shoka la kushushwa ngazi huku zikiwa zimesalia mechi 9 msimu kukamilika.
Post a Comment