Marekani imechukua
hatua isiyo ya kawaida na kuwaita Maseneta wote kwa kikao cha kupashwa
habari kuhusu Korea Kaskazini katika ikulu ya White House.
Washington
imeendelea kueleza wasiwasi wake kuhusu mpango wa Korea Kaskazini
kuendelea kufanya majaribio ya makombora na silaha za nyuklia, na
vitisho vyake kwa majirani zake na Marekani.
Kikao hicho, ambacho
kitashirikisha maseneta 100 pamoja na waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani
Rex Tillerson na Waziri wa Ulinzi James Mattis kitafanyika Jumatano.
China, mshirika mkuu wa Korea Kaskazini, imehimiza pande zote kuwa na uvumilivu.
Rais wa China Xi Jinping alitoa wito huo alipozungumza kwa simu na Rais Donald Trump Jumapili.
Bw
Xi alihimiza pande zote mbili "kuvumiliana na kujiepusha na vitendo
ambavyo vinaweza vikaongeza wasiwasi zaidi", kwa mujibu wa wizara ya
mambo ya nje ya China.
Kwa upande wake, bw Trump amesema Korea
Kaskazini inahatarisha uthabiti katika rasi ya Korea kwa kuendelea na
msimamo wake mkali.
Maafisa wa Ikulu ya White House mara kwa mara
huwapasha habari wabunge kuhusu masuala ya usalama, lakini ni nadra sana
kwa bunge lote la Seneti kwenda White House.
Pamoja na Bw
Tillerson na Jenerali Mattis, kutakuwepo pia na Mkuu wa Taifa wa Ujasusi
Dan Coats na Jenerali Joseph Dunford, Mwenyekiti wa Jopo la Wakuu wa
Majeshi ya Marekani.
Msemaji wa ikulu ya White House Sean Spicer
alipoulizwa maswali kuhusu kikao hicho aliwaomba wanahabari waelekeze
maswali yao kwa kiongozi wa wengi katika bunge la Seneti, Mitch
McConnell.
Wasaidizi wakuu wa Rais Trump ambao walihojiwa na
Reuters, walisema Bunge la Wawakilishi pia linataka kuandaliwe kikao
sawa na hicho cha maseneta kuhusu Korea kaskazini.
Washington imesema kundi la meli za kivita, likiongozwa na meli
kubwa yenye uwezo wa kubeba ndege USS Carl Vinson, linatarajiwa kufika
rasi ya Korea siku chache zijazo.
Hii ni licha yakuwepo na habari za utata kuhusu zilikokuwa zinaelekea meli hizo awali.
Meli
hizo za kivita vilikuwa zimedaiwa kuwa njiani kuelekea rasi ya Korea
zikitokea Australia lakini baadaye zikaelekea hadi mlango wa kuingia
Bahari ya Hindi.
Lakini sasa maafisa wa jeshi la wanamaji la Marekani wamethibitisha kwamba meli hizo zinaelekea rasi ya Korea.
Bw
Trump pia ameambia mabalozi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
kwenye mkutano White House kwamba Umoja wa Mataifa ni sharti uiwekee
Korea Kaskazini vikwazo vipya.
Gazeti la chama tawala cha Workers' Party Rodong Sinmun alieleza meli hiyo kuwa "mnayama".
Korea
Kaskazini imeahidi kuendelea na majaribio yake ya makombora licha ya
onyo la Bw Trump na wataalamu wanasema kwamba taifa hilo linajiandaa
kufanya jaribio jingine la silaha ya nyuklia.
Washington ina
wasiwasi kwamba Pyongyang inaweza kupata uwezo wa kuweka bomu la nyuklia
kwenye kombora linaloweza kuifikia Marekani.
China inahofia
uwezekano wa kuzuka kwa vita kamili rasi ya Korea, ambavyo vinaweza
kusababisha kusambaratika kwa utawala wa Kim Jong-un.
China ina
wasiwasi kwamba tukio kama hilo linaweza kupelekea wakimbizi wengi
kukimbilia usalama China. Aidha, uwepo wa Wamarekani Korea Kaskazini
utaifanya Marekani kuwa na udhibiti wa eneo linalopakana na China.
Post a Comment