Korea kaskazini yaendelea na ukaidi yafyatua kombora jingine
Korea kaskazini yaendelea na ukaidi yafyatua kombora jingine
Korea kaskazini imefanya jaribio la kombora leo
Jumamosi(29.04.2017)Korea ya
kusini na jeshi la Marekani zimesema,ikikaidi onyo la
Marekani na,China, zilizojaribu kwa miaka kadhaa kudhibiti
mpango wa silaha wa nchi hiyo.
Jaribio hilo lililofanywa katika eneo kaskazini mwa mji mkuu
wa Korea kaskazini , Pyongyang, linaonekana kuwa limeshindwa,
maafisa wa Marekani na Korea kusini wamesema, katika kile ambacho
ni jaribio la nne mfululizo la Korea kaskazini kushindwa tangu
mwezi Machi.
Jaribio hilo linakuja wakati waziri wa mambo
ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson amelionya baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa kwamba kushindwa kuudhibiti mpango wa
kinyuklia na makombora wa Korea kaskazini kunaweza kusababisha
"matokeo mabaya".
Maafisa
wa Marekani , wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina,
wamesema kombora hilo huenda ni la masafa ya kati linalofahamika
kama KN-17 na linaonekana kuwa liliripuka na kuvunjika katika
muda wa dakika chache tangu pale lilipofyatuliwa.
Korea
kusini imesema nchi hiyo ya kaskazini inacheza na moto na
kuionya kwamba itakabiliwa na vikwazo vikali zaidi ya Umoja wa
Mataifa.
Ukiukaji wa maazimio ya Umoja wa Mataifa
Jeshi
la Korea kusini limesema kwamba kombora hilo , lililofyatuliwa
kutoka katika jimbo la Pukchang katika mwelekeo wa kaskazini
mashariki, lilifikia umbali hewani wa kilometa 71 kabla ya
kuvunjika vunjika dakika chache wakati likiruka. Limesema kurushwa
kwa kombora hilo ni ukiukaji wa wazi wa maazimio ya Umoja wa
Mataifa na kuionya Korea kaskazini kutochukua hatua bila
kufikiria.
Utawala
wa rais wa Marekani Donald Trump unaweza kuchukua hatua dhidi
ya jaribio hilo la kombora la Korea kaskazini kwa kuharakisha
mipango yake kwa ajili ya vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya
Pyongyang, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa hatua dhidi ya maeneo
mahususi ya Korea kaskazini na China, afisa wa Marekani
ameliambia shirika la habari la Reuters jana.
Wakati Korea
kaskazini inachukua hatua kwa kukaidi mbinyo kutoka Marekani na
mshirika wake mkubwa China, Marekani inaweza kufanya luteka mpya
ya jeshi la majini na kuweka meli zaidi za kijeshi na ndege
katika eneo hilo kwa nia ya kuonesha uwezo wa nguvu zake ,
afisa huyo amesema , kwa masharti ya kutotajwa jina.
Vikwazo vipya
Afisa
huyo amesema vikwazo vyovyote vipya vinaweza kuwekwa katika
siku chache zijazo na vinaweza kulenga idadi kadhaa ya maeneo
ambayo tayari yametathminiwa na serikali ya Marekani kwa ajili
ya hatua kama hizo, wakati utawala huo wa Marekani unaendelea
kutayarisha mpango mkubwa zaidi wa vikwazo.
Maeneo lengwa
ya vikwazo hivyo , afisa huyo amesema , yanaweza kuwa taasisi za
kifedha na makampuni muhimu ya Korea kaskazini pamoja na China,
hatua ambayo huenda ikaikasirisha China.
Wakati
rais Trump amemsifu rais wa China Xi Jinping kwa kuashiria
ongezeko la ushirikiano kuhusiana na suala la Korea kaskazini ,
afisa huyo amesema Beijing bado "inahitajika kuchora aina fulani
ya msitari mchangani" na Pyongyang kuhusiana na mpango wake wa
kinyuklia.
Post a Comment