Papa Francis aanza ziara nchini Misri
Kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis
ameanza ziara nchini Misri, katika juhudi za kuhimiza maelewano kati ya
Wakristu na Waislamu na kuepusha ghasia zinazofanywa kwa kutumia jina la
Mungu.
Mara tu baada ya kuwasili mjini Cairo mchana wa leo, Papa Francis
amepokelewa na Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi kwa heshima za
kijeshi, huku makasisi wakijipanga mstari kumsalimia. Baadaye
ametembelea chuo kikuu maarufu cha Kiislamu cha Al-Azhar, ambako
amefanya mazungumzo na Mufti Mkuu Ahmed al-Tayeb, yaliyoelezewa kama
yenye kukamilisha mchakato wa kuboresha mahusiano kati ya Wakatoliki na
Waislamu wa madhehebu ya Sunni. Akizungumza na waandishi wa habari ndani
ya ndege kabla ya kutua mjini Cairo, Papa Francis amesema ziara yake ya
masaa 27 itakuwa ya kusajiisha umoja na udugu. Ujumbe huo pia ndio
alioutoa kwa watu wa Misri, kabla ya kufunga safari kuizuru nchi yao.
''Kwa
moyo wenye furaha na shukrani nitaitembelea nchi yenu, ambayo ni kitovu
cha ustaarabu na zawadi wa Mto Nile, nchi ya jua na ukaribu, ambako
maaskofu na manabii waliishi, na ambako Mungu mwenye rehema na uwezo,
aliitoa sauti yake'', alisema Papa Francis na kuongeza, ''Ninayo furaha
ya kweli kuja kama rafiki, na kama mjumbe wa amani katika nchi ambayo
miaka 2000 iliyopita, iliipa hifadhi familia takatifu iliyokuwa
ikikimbia kitisho cha mfalme Herod.''
Mjadala kati ya waislamu na wakristo
Katika
ziara yake hiyo fupi, Papa Francis atakutana kwa pamoja na viongozi wa
Kiislamu na wa Kikristu, kabla ya kulitembelea kanisa lililoshambuliwa
kwa mabomu mwezi Desemba mwaka jana. Watu 29 walipoteza maisha katika
shambulio hilo. Shambulio jingine kwenye kanisa la Koptiki mwezi huu wa
Aprili liliuwa waumini 45.
Makanisa yote nchini Misri yamewekewa
ulinzi wa ziada, kwa hofu kuwa mashambulizi mengine yanaweza kufanywa
wakati huu wa ziara ya Papa Francis. Licha ya wasiwasi kuhusu usalama
lakini, Papa Francis anatarajiwa kutumia gari la kawaida tu katika
shughuli zake.
Wakati ya ziara yake hii nchini Misri, Papa
Francis atahutubia mkutano wa kimataifa kuhusu amani ambao umeandaliwa
na chuo cha al-Azhar, ambacho ni kituo cha maarufu cha elimu kwa zaidi
ya miaka 1000, chenye msikiti wenye historia ya fahari kubwa.
Kukosoa makosa ya Papa Benedikt wa XVI
Francis
ni Papa wa kwanza kuitembelea Misri tangu ziara nyingine ya kihistoria
iliyofanywa nchini humo na Papa John Paul wa II mwaka 2000. Uhusiano
kati ya Misri na makao makuu ya Kanisa Katoliki uliingia doa enzi za
Papa Benedikt wa 16, ambaye kufuatia shambulizi jingine kwenye kanisa la
Koptik mwaka 2006 alitoa kauli iliyochukuliwa kama yenye kuunganishi
dini ya Islamu na ghasia, kauli iliyokosolewa na chuo cha Al-Azhar kama
uingiliaji wa mambo ya ndani ya Misri.
Wakristu wa madhehebu ya
Koptik ni asilimia kumi ya wakazi wote milioni 92 wa Misri, na wamekuwa
wakilengwa na mashambulizi ya mara kwa mara. Rais wa sasa wa Misri, japo
anachukuliwa kama mtu anayetawala kwa mkono wa chuma amekuwa rafiki wa
wakristu walio wachache nchini humo, na mwaka 2015 alikuwa rais wa
kwanza wa Misri kushiriki katika ibada ya Krismasi.
Post a Comment