Ujerumani, Poland na England zajiimarisha
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Löw
alikamilisha kazi yake baada ya mabingwa hao wa dunia kupata ushindi wa
tano kwenye mechi tano katika Kundi lao la kufuzu Kombe la Dunia.
Ushindi wao wa 4-1 dhidi ya Azerbaijan mjini Baku ulikuwa suala
rahisi tu kwa Wajerumani ambao walifungwa bao lao la kwanza kabisa
katika Kundi C. Ujerumani wanaongoza kileleni na pengo la pointi tano
dhidi ya Ireland ya Kaskazini ambayo iliizaba Norway 2-0. Nayo Jamhuri
ya Czech iliizaba San Marino 6-0. Kocha Löw alielezea kuridhika kwake na
matokeo hayo
Kundi F
Uwanjani
Wembley, England ilipambana na kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya
Lithuania. Ni mechi ambayo mshambuliaji Jermain Defoe mwenye umri wa
miaka 34 alirejeshwa kikosini na akafunga bao lake la 20 la kimataifa.
England sasa imejiimarisha kileleni mwa Kundi F. Vijana hao wa kocha
Garry Southgate sasa ndio timu pekee ya Ulaya ambayo haijafungwa bao
hata moja kufikia sasa. England wana pointi 13, nne mbele ya Slovakia
ambao walisonga katika nafasi ya pili ya kundi hilo kwa kupata ushindi
wa 3-1 dhidi ya Malta. Scotland wako nyuma na pengo la pointi sita baada
ya kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya Slovenia.
Katika Kundi E,
nahodha wa Poland Robert Lewandowski alifunga bao katika mechi ya kumi
mfululizo na kuiweka kileleni timu yake kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya
Montenegro. Montenegro sasa iko na pointi saba sawa na Denmark baada ya
Wadenmark kutoka sare tasa na Romania, ambayo ina pointi sawa na
Armenia. Armenia iliifunga Kazakhstan 2-0 na kuyaweka hai matumaini ya
kucheza mechi za mchujo.
Kocha wa uholanzi atimuliwa
Wakati
huo huo, Kocha wa Uholanzi Danny Blind ameüigwa kalamu, ikiwa ni chini
ya saa 24 tu baada ya kichapo cha 2-0 dhidi ya Bulgaria kuiacha timu
yake katika nafasi ya nne ya Kundi A la kufuzu katika dimba la Kombe la
Dunia. Shirikisho la kandanda la Uholanzi lilitangaza uamuzi huo kupitia
taarifa baada ya Blind, kuitwa kwa ajili ya mazungumzo ya dharura.
Kocha
huyo mwenye umri wa miaka 55 amelalamikia uamuzi huo akisema kuwa timu
yake ilikuwa kwenye mkondo sahihi na kichapo cha Bulgaria kilikuwa ni
pigo. Timu ya taifa ya Uholanzi imekuwa ikiyumba tangu ilipokosa
kushiriki dimba la Ubingwa wa Ulaya 2016 hasa ikizingatiwa kuwa miaka
miwili kabla, ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye dimba la Kombe la
Dunia 2014 nchini Brazil. Jean Paul Decossau ni mkurugenzi wa shirikisho
la soka la Uholanzi na hapa anaelezea kilichojiri
Kichapo hicho
kimeiacha Uholanzi ikikabiliwa na mtihani mkubwa wa kumaliza katika
mojawapo ya nafasi mbili za kwanza za kufuzu katika Kundi A. Ina pointi
saba baada ya kucheza mechi tano na wako nyuma ya vinara Ufaransa ambao
wana pointi 13, Sweden ina 10 na Bulgaria ina 9. Kocha msaidizi Fred
Grim atachukua usukani katika mchuano wa kirafiki kesho dhidi ya Italia
mjini Amsterdam wakati kocha mpya akitafutwa.
Post a Comment