Jeshi la Ujerumani kufanyiwa mageuzi baada ya kashfa-Waziri
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen
amesema ataanzisha mageuzi katika jeshi la nchi hiyo, kufuatia ugunduzi
wa mienendo ya kushabikia unazi miongoni mwa wanajeshi.
Waziri Ursula von der Leyen ameitangaza azma hiyo mjini Berlin,
wakati uchunguzi ukiwa tayari unaendelea kuhusu visa vya wanajeshi wa
Ujerumani kubainika na mienendo inayoashiria misimamo mikali ya
kizalendo, ambayo imezusha masuali kuhusu uwezo wa uongozi kwa upande wa
Bi von der Leyen. Akizungumza asubuhi leo mbele ya kamati ya bunge
inayohusika na masuala ya ulinzi, waziri huyo amesema mchakato wa
mageuzi utakuwa mpana, na utawagusa wanajeshi wengi, kuanzia ngazi ya
chini hadi ya juu kabisa.
''Nimewasilisha hatua tofauti ambazo
tutazichukua kuanzia kanuni za kinidhamu jeshini hadi mpango mpya wa
uongozi wa ndani katika jeshi'' amesema von der Leyen na kuongeza kuwa
hayo yatajumuisha kwa aina ya pekee kutazama upya maagizo yaliyokuwepo,
na pia kutathmini upya elimu ya siasa katika jeshi letu.
Sura
ya Jeshi la Ujerumani (Bundeswehr) imetiwa doa na mienendo ya siasa
kali za mrengo wa kulia miongoni mwa baadhi ya wanajeshi.
Juhudi
hizi zinakuja siku moja baada ya kukamatwa kwa mwanajeshi
aliyetambulishwa kama Maximilian T, kama mshukiwa katika njama ya
kufanya mashambulizi yenye kushawishiwa na mtizamo mkali wa kizalendo,
kuwalenga maafisa wa ngazi ya juu nchini Ujerumani, mashambulizi ambayo
wakimbizi wangesingiziwa kuyafanya.
Maximilian T. anahusishwa na
mshukiwa mwingine anayejulikana na Franco A., afisa mwingine wa jeshi la
Ujerumani ambaye alitaka kujifanya mkimbizi kutoka Syria, ili lawama
dhidi ya mashambulizi aliyopanga kuyafanya ziwaendee wakimbizi.
Waziri
Ursula von der Leyen ambaye anatoka katika chama cha Christian
Democratic Union CDU cha Kansela Angela Merkel, amekuwa akishambuliwa
kutoka kila upande wa kisiasa, kwa kushindwa kung'amua mapema mfumo wa
siasa kali za kizalendo miongoni mwa wanajeshi.
Jeshi la
Ujerumani, Bundeswehr kwa wakati huu linaendesha msako katika kambi zote
za jeshi kutafuta vitu vya ukumbusho wa enzi za utawala wa wanazi,
katika mchakato mzima wa kuwatambua wanajeshi wenye misimamo mikali ya
mrengo wa kulia. Vitu vya aina hiyo viligunduliwa katika kambi mbili,
moja wapo ikiwa Illkirch alikokuwa akiishi mshukiwa Franco A.
Msako wa washukiwa wa ugaidi
Wakati
mageuzi hayo yakipendekezwa jeshini, ofisi ya Mwendeshamashtaka wa
Shirikisho la Ujerumani Frauke Koehler amesema polisi wamefanya upekuzi
kwenye nyumba za watu katika majimbo manne, kuhusiana na watu watatu
wanaoshukiwa kuwa na mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu,
IS. Majimbo yaliyohusika katika upekuzi huo ni Berlin, Bavaria, Saxon na
Saxony-Anhalt.
Washukiwa wawili kuhusiana na msako huo
wanatuhumiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi, huku wa tatu akishukiwa
kuunga mkono kundi hilo.
Waendeshamashitaka wamesema washukiwa
hao wana uhusiano na raia wa Syria aliyekamatwa mwaka 2016, akituhumiwa
kutaka kufanya shambulio la bomu, na pia msyria mwingine aliyekamatwa
wiki iliyopita mjini Leipzig, ambaye pia anakabiliwa na mashitaka ya
kuwa mwanachama wa kundi la IS.
Post a Comment