Nani alihusika katika shambulio la kirusi cha mtandaoni
Nani alihusika katika shambulio la
kirusi cha mtandaoni ambacho kiliathiri kompyuta katika zaidi ya mataifa
150 duniani, zikiwemo Kenya na Tanzania? Kumeibuka madai kwamba huenda
wadukuzi walitoka Korea Kaskazini.
Lakini kufikia sasa, hakuna ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha hilo.
Huenda
hujawahi kusikia kuhusu kundi linaloitwa Lazarus Group, lakini pengine
unafahamu baadhi ya matokeo ya shughuli zake. Kundi hili lilihusika
katika kudukua mfumo wa kompyuta wa Sony Pictures mwaka 2014 na tena
wakadukua benki moja ya Bangladesh mwaka 2016.
Inasadikika kwamba wadukuzi hao wa Lazarus Group walifanyia kazi yao China lakini kwa niaba ya Korea Kaskazini.
Wataalamu
wa usalama mtandaoni sasa wanahusisha shambulio la kirusi cha WannaCry
na kundi hilo baada ya ugunduzi uliofanywa na mtaalamu wa usalama wa
kompyuta wa Google Neel Mehta.
Mehta aligundua kwamba maelezo ya
kutunga programu ya kompyuta ya kirusi cha WannaCry yanafanana na
maelezo ya programu zilizowahi kutumiwa na Lazarus Group awali.
Huenda ikawa labda ni sadfa tu, lakini kuna viashiria vingine.
Kutofautisha maelezo ya kompyuta
Prof
Alan Woodward, mtaalamu wa usalama wa mifumo ya kompyuta, anasema
ujumbe wa kuitisha kikombozi unatumia lugha inayoonekana kana kwamba
aliyetafsiri alitumia kompyuta kuufanya kuwa wa Kiingereza, na ujumbe
ulioandikwa kwa Kichina unaonekana kuandikwa na Mchina asilia.
"Mnavyoona uhusiano ni mdogo sana na labda ni sadfa tu," Prof Woodward anasema.
"Hata hivyo, uchunguzi zaidi unahitajika.
"Ugunduzi
wa Neel Mehta ndio kiashiria muhimu zaidi kufikia sasa kuhusu chanzo
cha WannaCry," kampuni ya usalama wa kompyuta ya Urusi, Kaspersky,
inasema.
Hata hivyo, maafisa hao wanasema habari zaidi zinahitajika kuhusu aina za awali za WannCry kabla ya uamuzi kamili kufanywa.
"Tunaamini kwamba ni muhimu watafiti wengine maeneo
mengine ya dunia wachunguze kuhusu kufanana huku na wajaribu kuchimba
zaidi kupata maelezo zaidi kuhusu asili ya WannaCry," kampuni hiyo
ilisema.
"Ukiangalia shambulio la udukuzi la benki hiyo ya
Bangladesh, siku za mwanzo, hakukuwa na maelezo mengi ya kulihusisha na
kundi la Lazarus Group.
"Baadaye, ushahidi zaidi ulitokea na
kutuwezesha, pamoja na wengine, kuhusisha kundi hilo na shambulio hilo
kwa imani zaidi. Utafiti zaidi unaweza kuwa muhimu sana katika
kubainisha ukweli."
Huwa vigumu sana kubaini nani amehusika katika shambulio la mtandao - na mara nyingi hutegemea maafikiano badala ya uthibitisho.
Kwa
mfano, Korea kaskazini haijawahi kukiri kuhusika katika udukuzi wa Sony
Pictures - na ingawa watafiti, na serikali ya Marekani, wanaamini
kwamba ni Korea Kaskazini iliyohusika, hakuna anayeweza kupuuzilia mbali
uwezekano kwamba madai hayo si ya kweli.
Wadukuzi walio na
utaalamu wa juu wanaweza kuifanya ionekane kwamba shambulio hilo
lilitoka Korea Kaskazini kwa kutumia mbinu mbalimbali.
'Ushahidi hauwezi kujisimamia'
Kuhusu WannaCry, kuna uwezekano kwamba wadukuzi walinakili tu maelezo ya kompyuta yaliyotumiwa awali na Lazarus Group.
Lakini
Kaspersky wanasema dalili za kupotosha katika maelezo ya WannaCry
zinaweza kuwepo lakini ni vigumu kiasi, kwani katika toleo la baadaye la
kirusi hicho, maelezo yaliyokuwa yanafanana nay a Lazarus Group
yaliondolewa.
Post a Comment