Ujerumani huenda ikaondoa wanajeshi wake
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema Ujerumani inaweza kuondoa wanajeshi wake waliopo Uturuki iwapo Uturuki itaendelea kusisitiza kuwanyima ruhusa wabunge wa Ujerumani kuwatembelea wanajeshi hao.
Takriban wanajeshi 250 wa Kijerumani wapo katika kambi ya jeshi la
anga ya Incirlik nchini Uturuki, ukiwa ni mchango wa Ujerumani katika
ujumbe wa kijeshi unaoongozwa na Marekani unaopambana na kundi
linalojiita Dola la Kiislamu IS katika nchi jirani ya Syria.
Duru
za wizara ya mambo ya nje ya Uturuki zimeliambia shirika la habari la
Reuters, kwamba ziara ya wabunge wa Kijerumani katika kambi hiyo
haitakuwa hatua sahihi kwa sasa bila ya kutoa maelezo zaidi.
"Hii
ni bahati mbaya sana, na tumelisema hilo kwa njia tofauti. Tutaendelea
na mazungumzo na Uturuki lakini wakati huo huo tutalazimika kutafuta
njia nyingine za kutimiza lengo letu kwa sababu tumeshawahi kuwa na
tatizo hili la kuzuiwa ziara, kabla. Na hilo linamaanisha kutafuta njia
mbadala kwa kambi hii ya Incirlik na suluhu moja miongoni mwa nyingine
ni Jordan," amesema Kansela Angela Merkel, akiwa katika mkutano na
waandishi habari hapo jana, alipoulizwa juu ya uamuzi wa serikali ya
Uturuki wa kuwazuia wabunge wa Ujerumani kuwatembelea wanajeshi wao
katika kambi hiyo ya jeshi la anga ya Incirlik.
Timu
ya utafiti wa kijeshi ya Ujerumani itaizuru Jordan katika siku za
karibuni kuangalia uwezekano wa kupata kambi ya kijeshi nchini humo.
Hayo ni kulingana na duru za serikali ya Ujerumani.
Kutokana na
sababu za kihistoria na kama njia ya kuzuia matumizi mabaya ya madaraka,
jeshi la Ujerumani Bundeswehr linadhibitiwa na bunge la Ujerumani, na
sio serikali, hili linamaanisha kwamba wabunge wana haki ya kukagua
shughuli za jeshi la Ujerumani, ikiwa ni pamoja na vikosi vya kijeshi
vilivyotumwa nje ya nchi.
Uhusiano kati ya Uturuki na Ujerumani
uliporomoka kwa kasi kubwa kuelekea uchaguzi wa kura ya maoni wa Aprili
16 wa nchini Uturuki wa kupanua madaraka ya Rais wa nchi hiyo Tayyip
Erdogan.
Ujerumani na washirika wengine wa nchi za Magharini
wameonesha wasi wasi kuhusu kile wanachokitaja kuwa ni kuelekea utawala
wa kimabavu nchini Uturuki.
Mwaka jana Uturuki iliwaekea marufuku wabunge wa Ujerumani kutembelea kambi hiyo kwa miezi kadhaa ikiwa kama jawabu la azimio la bunge la Ujerumani la kutangaza mauaji ya Waarmenia yaliyofanywa na vikosi vya utawala wa Ottoman mwaka 1915 kuwa ni ya kimbari, matamshi yaliyokataliwa na Uturuki
Mwaka jana Uturuki iliwaekea marufuku wabunge wa Ujerumani kutembelea kambi hiyo kwa miezi kadhaa ikiwa kama jawabu la azimio la bunge la Ujerumani la kutangaza mauaji ya Waarmenia yaliyofanywa na vikosi vya utawala wa Ottoman mwaka 1915 kuwa ni ya kimbari, matamshi yaliyokataliwa na Uturuki
Msemaji wa
wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani amaesema Waziri wa Mambo ya Nje wa
Ujerumani Sigmar Gabriel atalizungumzia suala hilo la kambi ya Incirlik
na wenzake ambao pia ni wanachama wa NATO mjini Washington Marekani leo
hii.
Post a Comment