Monaco ina kibarua kigumu dhidi ya Juve
Ni timu
zipi zitaelekea Cardiff kwa fainali ya Champions League barani Ulaya,
swali hilo linaanza kupatiwa jibu leo wakati
mkondo wa pili wa mchezo wa nusu fainali kati ya Juventus, na AS Monaco
utakapofanyika.
Monaco pamoja na Atletico Madrid zinakabiliwa na majukumu
ambayo yanaonekana kuwa karibu ya kutowezekana katikati ya wiki
hii katika michezo ya mkondo wa pili wa nusu fainali ya kombe
la ligi ya mabingwa , Champions League barani Ulaya, ambapo
wapinzani wao Juventus na Real Madrid wapo katika ukingo wa
kukutana mjini Cardiff katika fainali ya mwaka huu 2017.
Hata
kocha wa Monaco Leonardo Jardim anaukadiria mchezo huo kwa
kiwango cha nafasi moja tu katika 20 zilizopo. Na wengi
wangesema kwamba huo ni msimamo wa matumaini kwa nafasi ilizonazo
kikosi chache chenye wachezaji wachanga kuweza kubadilisha
matokeo ya awali ya mabao 2-0 dhidi ya Juventus Turin.
Mabingwa
hao watarajiwa wa ligi ya Ufaransa ambao hupachika mabao bila
shida katika ligi ya nyumbani , wamepachika mabao 3 mara 27
msimu huu. Lakini hakuna timu iliyokwisha fanya hivyo dhidi ya
ngome ya Juventus ambayo imeruhusu mabo mawili , mara tano tu
katika michezo 51 katika kampeni ya mwaka huu, haijashindwa
nyumbani katika muda wa miezi 20 na ngome yake imevujisha mabao
mawili tu katika michezo 11 ya Champions League.
Takwimu
hizi zinatoa nguvu zaidi kwa Bibi Kizee, wakati timu hiyo ikiwa
na uwezo wake wote wa wachezaji, kama ilivyokuwa wakati
walipofanikiwa kutuliza mzuka wa washambuliaji hatari wa Monaco
katika mji wa kitalii wa Monaco wiki iliyopita, ama wakati Leo
Messi na wenzake wa Barcelona walipopigwa sindano ya ganzi na
kuendeshwa mchakamchaka mjini Turin.
Kutokana na hilo,
kocha wa Monaco Jardim alisema jukumu lake la kwanza lilikuwa
kuingiza imani katika kikosi chake kwamba hawapambani na dude
lililokufa.
"ni wajibu wetu kufanya kitu tofauti. Iwapo
unashindwa nyumbani kwa mabao 2-0 ni wazi kwamba unapaswa kuja
na kitu cha ziada," Jardim alisema katika mkesha wa kuamkia
mchezo huo.
"Mjini Monaco tulipata kipigo kutokana na
uzoefu: mikwaju yetu kuelekea golini ilikuwa sawa na Juventus.
Tofauti ilikuwa kiwango cha mafanikio yao kilikuwa asilimia 100,
kwa upande wetu ilikuwa ziro." Ameongeza Jardim.
Kocha wa Juve Massimiliano Allegri
Kocha
wa Juve Massimiliano Allegri alicheka baada ya kuambiwa kwamba
matokeo yamekamilika na timu yake tayari ni mshindi. "Huwezi
kujua kile kitakachotokea katika mchezo. Monaco huenda wakaingia
katika mchezo huo katika mtindo tofauti kabisa na kufanya hali
kuwa ngumu na wana wachezaji wenye uwezo mkubwa, vipaji vya juu
kabisa," amesema.
"Tunapaswa kuanza mwanzo kabisa ,
tuhakikishe tunacheza kwa nguvu katika mchezo huo na matumaini
ni kwamba tutakuwa bora kiufundi kuliko tulivyokuwa kule Monaco,
ambako tulipata fursa nyingi na kutengeneza mazingira yaliyoleta
hatari na mara nyingi tulifanya makosa.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / dpae
Post a Comment