Merkel, Macron waazimia kuimarisha ushirikiano
Ziara ya Rais Emmanuel Macron mjini Berlin jana jioni ilikuwa ya
kwanza kwake kama rais wa Ufaransa nje ya nchi, baada ya
kukabidhiwa
rasmi madaraka juzi Jumapili. Alilakiwa na umati wa watu waliokusanyika
karibu na ofisi ya Kansela Angela Merkel,
baadhi wakipeperusha bendera
ya Umoja wa Ulaya. Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari,
Merkel na Macron waliojawa na tabasamu, walisisitiza umuhimu wa
ushirikiano wa nchi zao kwa manufaa ya Ulaya nzima. Kansela Merkel
alisema anaunga mkono Ufaransa yenye nguvu.
''Kila mmoja wetu
anasimamia maslahi ya nchi yake, lakini, kijadi maslahi ya Ujerumani
yamefungamana na maslahi ya Ufaransa'', alisema Bi Merkel, na kuongeza
kuwa. Ujerumani inaweza kufanikiwa tu, ikiwa mambo yanakwenda vizuri
Ulaya, na mambo yatakwenda vizuri Ulaya, ikiwa kuna Ufaransa yenye
nguvu.
Msukumo mpya kwa Ulaya
Aidha,
Kansela Merkel alieleza kuwa yeye na mgeni wake wamekubaliana juu ya
mipango kadhaa ya kuupa msukumo mpya uhusiano kati ya Ufaransa na
Ujerumani, ukiwemo wa mikutano ya mawaziri mwezi Julai baada ya Ufaransa
kukamilisha uchaguzi wa bunge.
Viongozi hao wawili hali
kadhalika walizungumzia utayarifu wao wa kukubali mabadiliko katika
muundo wa Umoja wa Ulaya, kwa madhumuni ya kuufanya umoja huo kuwa wenye
ufanisi zaidi. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema yeye hataogopa
kuyaleta mezani masuala ambayo siku za nyuma yalikuwa yakinyamaziwa.
Alisema,
''Aghalabu, suala la mabadiliko katika mkataba wa Ulaya limekuwa mwiko
nchini Ufaransa. Kwangu haitakuwa hivyo. Matarajio yangu ni kwamba
mwelekeo wa pamoja wa Ulaya uwe wa kurejesha ufanisi katika kanda
inayotumia sarafu ya yuro, na katika Umoja wa Ulaya. Na ikiwa mchakato
huo utahitaji mabadiliko ya kitaasisi, sisi tuko tayari''.
Hofu kuhusu sera ya deni la pamoja
Rais
Emmanuel Macron pia alitumia mkutano wa jana kutuliza hofu za wanasiasa
wa nchini Ujerumani, kuhusu pendekezo lake la awali la kuwepo bajeti ya
pamoja kwa nchi 19 zinazotumia sarafu ya yuro, kwa madhumuni ya
kushughulikia vyema zaidi mzozo wa kifedha. Baadhi ya wanasiasa wa
Ujerumani walilichukulia pendekezo hilo kama njia ya kuwatwisha mzigo
zaidi walipa kodi wa Ujerumani, mnamo wakati uchaguzi muhimu ukikaribia.
Macron
alifafanua kuwa pendekezo lake hilo halilengi kuugawa mzigo wa madeni
ya siku za nyuma miongoni mwa wanachama wa kanda ya sarafu ya yuro,
akisema badala yake anataka mpango wa pamoja wa siku za usoni katika
masuala ya uwekezaji.
Mkutano kati ya viongozi hao wa nchi mbili
ambazo zinachukuliwa kama mihimili ya Umoja wa Ulaya, umefanyika wakati
umoja huo ukikabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwemo kujiondoa kwa
Uingereza katika mchakato ambao unajulikana kama Brexit, na kukua kwa
hisia za kuutilia mashaka umoja huo miongoni mwa raia wa nchi
zinazouunda.
Post a Comment