Dkt Mohamed Shein amesema serikali yake haitishiki na tishio la kukatiwa umeme
\
Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesema serikali yake haitishiki na tishio la kukatiwa umeme na iko tayari kutumia vibatari na deni linalodaiwa sio la leo wala jana.
Matamshi yake yanajiri siku moja tu baada ya shirika la umeme nchini Tanzania Tanesco kutoa ilani ya siku 14 kwa wadeni wake kwamba litawakatia moto.
Hatua hiyo ya Tanesco inajiri baada ya rais Magufuli kuiagiza Tanesco kuwakatia umeme wadeni wake wote kikiwemo kisiwa cha Zanzibar.
Makamu wa rais wa kwanza nchini Tanzania Dkt. Shein ametoa msimamo huo katika mkutano wake na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Zanzibar mara aliporejea kutoka Indonesia.
Ziara hiyo ya Indonesia ilikuwa ya kuhudhuria mkutano wa nchi zilizopakana na bahari ya hindi ambapo alimwakilisha Rais John Magufuli.
Amesema deni linalodaiwa serikali italipa na yeye kama rais hana taarifa yoyote ya Zanzibar kukatiwa umeme ingawa hatarajii kitendo hicho kufanyika.
Dkt. Shein ameelezea mkutano huo na makubaliano yaliyofikiwa ambapo amesema utaleta tija na faida kubwa kwa Wazanzibari na Watanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi ikiwemo utalii, uvuvi, ulinzi ,vita dhidi ya uharamia na uchumi wa bahari.
Dkt. Shein ambaye aliongoza ujumbe wa mawaziri katika mkutano ambao ulikuwa wa kutimiza miaka 20 ya jumuiya ulihudhuriwa na marais wa nchi hizo za bahari ya hindi huku mkutano ujao unatarajiwa kufanyika Afrika Kusini.
Post a Comment