Mwendo kasi unavyopukutisha maisha
WAKATI tumevuka Chalinze, basi nililopanda kwenda Mbeya lilianza kwenda mwendo kasi uliopitiliza. Niliogopa maana ni siku chache tu kulikuwa kumetokea ajali za mabasi ya City Boys huko Manyoni, nilimfuata dereva kumwomba apunguze mwendo.
“Nilishangaa abiria wenzangu walinipinga na kunizomea, wakasema kama ninaogopa nishuke. Wakachangishana pesa ili wanipe kama nauli nipande basi jingine, niligoma lakini wakaendelea kunikejeli, kuona hivyo nikaamua kutoa taarifa kwa polisi Morogoro,” anasema Kaifa Malusu.
Malusu alipanda moja ya basi linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Tunduma (jina tunalo). Kwa maelezo yake basi hilo lilibeba abiria wengi ambao ni wafanyabiashara waliokuwa wanaenda Tunduma. Anasema kitendo cha yeye kumwomba dereva asiende mwendo kasi kiliwakera abiria hao ambao walidai wana haraka na wanahitaji kufika mapema.
“Mimi baada ya kuona abiria wananikejeli na dereva akawa hanisikii, nilipiga picha mwendo wa lile gari na kugundua lilikuwa linaenda kilometa 120. Nilitoa taarifa sehemu mbili kwa RTO Morogoro na kwa mmoja wa viongozi wa Chama cha Kutetea Haki za Abiria,” anasema Malusu.
Malusu anasema basi hilo lilipofika Morogoro lilisimamishwa na askari wa usalama barabarani ambaye alianza kutoa elimu kwa abiria kuhusu umuhimu wa gari kutembea mwendo wa kilometa 80 kwa sasa na umuhimu wa abiria kushirikiana ili kumzuia dereva asiende mwendo kasi.
Tabia ya dereva wa gari hili alilopanda Malusu kupenda kuendesha mwendo kasi uliopitiliza na kushabikiwa na abiria, ndio hali halisi ya usafiri wa mabasi mengi hapa nchini. Ni tabia hii ya ovyo ambayo imechangia maisha ya watu wengi kupotea kwa ajali za barabarani.
Inapotokea ajali, abiria wakiwemo hawa wanaowashangilia basi liende mwendo kasi, dereva mwenyewe kwa pamoja na waenda kwa miguu ni makundi ya watu ambao wanapoteza maisha kwa wingi kutokana na ajali za barabarani.
Mwendo kasi unasababisha mabasi ya abiria kupinduka, kugongana na kuua watu wengi wakati waenda kwa miguu nao wamejikuta wanapoteza maisha kwa kugongwa na magari hayo yanayoendeshwa kwa kasi.
Ripoti ya Shirika la Afya duniani (WHO) ya mwaka 2015 inasema kuwa asilimia 31 ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani ni waenda kwa miguu wakati asilimia 31 ya vifo hivyo ni madereva na abiria wa mabasi na asilimia 7 ya vifo ni madereva wa magari madogo.
Issa Kipula, katibu wa chama cha madereva (UWAMATA) anasema chanzo cha ajali za mabasi ni Sumatra. Anasema ratiba iliyowekwa na Sumatra inayoonesha muda ambao magari yanatakiwa kufika mkoa yanakoenda haiendani na mwendo ulioainishwa kwenye sheria ya usalama barabarani.
Anatoa mfano kwamba ratiba ya Sumatra inataka basi linaloondoka saa 12 stendi ya Ubungo lifike Mwanza saa 5:30 usiku jambo ambalo anasema kwamba kwa mwendo wa kilometa 30, 50 na 80 kwa saa ambao unawekwa na sheria ya usalama barabarani haumwezeshi dereva kufika Mwanza wakati huo.
“Ili dereva afike Mwanza muda huo ni lazima aendeshe gari kati ya spidi ya kilometa 100 hadi 120 kwa saa ndipo ataweza kufika muda huo,” anasema Kipula. Kipula anasema kwa mwendo wa kilometa 80 kwa saa dereva hawezi kufika Mwanza badala yake atalazimika kulala Igunga mkoani Tabora au Misigiri mkoani Singida.
“Kwa hali hii tunalazimika kwenda mwendo kasi ili kuwahi muda uliowekwa na Sumatra.” Anasema kutokana na ratiba hiyo ya Sumatra, mmiliki wa gari anataka gari lake lifike Mwanza au Kahama muda huo na dereva anayekiuka ratiba hiyo ni lazima afukuzwe kazi.
“Ukisema utembee mwendo wa kilometa 80 kwa saa lazima ulale njiani, na ukifanya hiyo lazima tajiri atakufukuza kazi.” Anasema UWAMATA imewahi kuiomba Sumatra ibadilishe ratiba hiyo ili magari yawe yanalala njiani, lakini kilichofuata hapo ni yeye kutishiwa maisha na baadhi ya wamiliki wa magari.
Anasema alienda kutoa ripoti polisi Magomeni lakini hakuna hatua iliyochukuliwa. Kipula anasema kwamba mmiliki wa gari yuko tayari atozwe faini hata mara sita kwa siku, lakini gari lake lifike linakoenda kwa wakati. Anasema faini zote wanazotozwa madereva kwa kuendesha mwendo kasi zinatolewa na wamiliki wa mabasi.
“Gari anakabidhiwa kondakta. Dereva yeye ni kibarua tu, hivyo dereva unaambiwa hakikisha gari inafika Mwanza muda huu, endesha unavyoweza, kama kuna tochi tajiri atalipa,” anasema dereva huyo ambaye ana miaka 15 kwenye tasnia hiyo.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani, Mohammed Mpinga wakati anazungumza na gazeti hili hivi karibuni alisema: “Ni kweli, kuna askari wetu ambao wanashirikiana na madereva kuhujumu mpango wa tochi ambao tumeuweka, mabasi bado yanaenda mwendo kasi na hilo binafsi nina ushahidi nao.”
Mpinga anasema hivi karibuni aliweka askari ambaye alivalia kiraia kwenye moja ya mabasi yanayoenda Mwanza. Anasema katika mtego ule kwa kuwa walikuwa wameweka kamera yenye GPS kila spidi ya gari hilo ilikuwa inatumwa moja kwake.
“Lile gari lili-overspeed (kwenda kiwango kisichokubalika) mara 20 wakati linaenda Mwanza na wakati linarudi Dar es Salaam lili-over speed mara 18, Hii inathibitisha madai kwamba kuna askari ambao wanakiuka maadili ya utumishi wao na hao tutashughulika nao kwa karibu zaidi,” anasema kamanda Mpinga.
Kamanda huyo anasema moja ya njia watakazotumia kuwabana trafiki hao ambao wanashirikiana na madereva na baadhi ya wamiliki wa magari kuihujumu tochi ni kuwa na baadhi ya abiria kwenye mabasi ambao watakuwa wanatoa taarifa za mwendo wa gari husika.
Anasema wamejipanga kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma ili abiria wasiwe wanawashangilia madereva wanaoenda kwa mwendo kasi na akatoa mfano kuwa baadhi ya abiria wamewasaidia hivi karibuni askari watatu wa usalama barabarani waliobainika kushirikiana na madereva kuhujumu tochi na wamechukuliwa hatua za kinidhamu.
Hata hivyo, anasema pamoja na mikakati yote, suala la usalama barabara litaheshimiwa na madereva iwapo sheria ya sasa itabadilishwa kwa kile anachodai kuwa madereva wameizoea na hawaigopi kwa kuwa haina makali. Sheria hiyo inaeleza kuwa dereva anayeendesha mwendo kasi kupita kilometa 80 kwa saa ambao umewekwa kwa madereva wa mabasi ya abiria akikamatwa na polisi faina anayotozwa na polisi ni Sh 30,000.
Kanuni za Sheria hiyo ya usalama barabara inatambua mwendo unaotakiwa kuendesha kwa magari yanayofanya safari zake mijini ambayo ni kilometa 50 kwa saa. Mwendo huo pia ndio unaotumika kwenye maeneo ya makazi ya watu.
Kwa mwendo wa kilometa 80 kwa saa ni mwendo unaoruhusiwa kwa magari makubwa ya mizigo yenye uzito halisi wa gari wa kg 3500 na magari ya huduma za umma kama mabasi, mabasi ya safari ndefu, lakini sio teksi nje ya maeneo ya makazi. Mwendo wa kilometa 100 kwa sasa umeruhusiwa kwa magari madogo na magari mengine ya wastani katika eneo la makazi.
Maeneo ambako hakuna maeneo ya makazi magari hayo madogo hayajawekewa ukomo wa mwendo kasi. Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Tike Mwambipile anasema mwendo kasi umeendelea kuwa sababu kubwa ya ajali zinazogharimu uhai wa watu wengi.
Anasema pia kuwa sheria ya sasa inayo mapungufu kadhaa pamoja na juhudi nyingi zinazofanywa na polisi na wadau wengine kutika kudhibiti jambo hilo limeendelea kuwa tatizo. Tike anasema adhabu zisizokidhi wala kuleta hofu kwa madereva wasiotaka kutii zimeendelea kufifisha juhudi za kudhibiti tatizo hili.
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) Johansen Kahatano, akizungumzia adhabu zinazotolewa na Polisi kwa madereva wanaovunja sheria za usalama barabarani, anasema adhabu hizo ziko chini na haziwaogopeshi madereva na wamiliki wa mabasi.
Anatoa mfano wa dereva kutozwa Sh 30,000 kwa kosa lolote la barabarani ni kulea makosa yaendelee kufanyika. Anapendekeza sheria ya usalama barabarani irekebishwe kwani yeye angependa kuona kila mtu anaadhibiwa kulingana na kosa lake. “Faini kidogo inawafanya watu wawe sugu na waizoee, adhabu haistashili kuzoewa inatakiwa watu waogope.”
Post a Comment