Header Ads

Kamusi mpya ya Kiswahili sasa mtandaoni


Meneja wa Kampuni ya Uchapishaji ya Oxford University Press Tanzania, Fatma Shangazi (kushoto) akionesha Kamusi ya Kiswahili Sanifu ambayo itapatikana mtandaoni bila malipo wakati wa uzinduzi uliofanyika Dar es Salaam. Kulia ni Ofisa Utawala wa Oxford, Betty Paul. (Picha na Rahel Pallangyo).


KATIKA kutambua umuhimu wa wazungumza Kiswahili kutumia lugha hiyo kwa ufasaha duniani kote, kampuni ya uchapishaji ya Oxford University Press (Tanzania), imezindua Kamusi ya Kiswahili Sanifu ambayo itapatikana mtandaoni bila malipo.
Kwa mujibu wa Meneja wa Oxford Tanzania, Fatma Shangazi, uzinduzi wa kamusi hiyo ya tatu ya Kiswahili ni sehemu ya kuadhimisha miaka 50 tangu kuanza kazi zake za uchapishaji nchini.
“Uzinduzi wa kamusi kwa njia ya mtandao unaenda sanjari na maadhimisho ya miaka 50 ya kampuni ya Oxford nchini ambayo ilianza kazi zake kwa mara ya kwanza mwaka 1967 jijini Dar es Salaam,” anasema Fatma.
Anasema kitengo cha Kamusi cha Oxford kimezindua kamusi hiyo ili kutoa fursa kwa watumiaji wa Kiswahili kote duniani kupata kwa urahisi maneno ya Kiswahili yaliyofanyiwa utafiti mpana na kutolewa maelezo ya kina.
“Tunaona fahari kubwa kuwapa mamilioni ya watumiaji wa Kiswahili fursa ya kufikia yaliyomo kwenye kamusi yetu pamoja na kuwa wataweza kuchangia katika maendeleo ya Kiswahili,” anasema Fatma.
Anasema hatua hiyo inaleta mapinduzi kwa mamilioni ya watu duniani kwa kuwarahisishia upatikanaji wa lugha yao katika mfumo wa dijiti hivyo wanaweza kupata huduma hiyo hata kwenye simu zao za mkononi. Meneja huyo anasema tunaishi katika wakati muhimu kutokana na mtandao wa intaneti na athari zake katika upanuzi wa lugha na uwezo wake wa ufanisi.
Anafafanua kwamba Kiswahili ni lugha ya nne kati ya lugha za Kiafrika zilizowekwa kwenye mpango huu, baada ya isiZulu, Northern Sotho, na Setswana. Maneno katika mtandao huo yametoka katika kamusi maarufu “Kamusi ya Kiswahili Sanifu, ambayo imeandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kamusi hiyo ya Kiswahili inapatikana kupitia https:// sw.oxforddictionaries.com. Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ernesta Mosha, anasema kwa kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia na kwa kuzingatia kwamba lugha ya Kiswahili inakua kwa kasi, matumizi ya Kamusi za Kiswahili kwa njia ya mtandao hayaepukiki.
Anasema uingizaji wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu mtandaoni ni mwendelezo wa juhudi zilizokwishaanzishwa na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili kupitia kamusi zake za Kiswahili–Kiingereza na Kiingereza –Kiswahili.
Mradi wa Oxford Global Languages (OGL) Mradi wa Oxford Global Languages (OGL), ulizinduliwa Septemba 2015 kama hatua mpya kutoka katika kitengo cha Kamusi Oxford kuandaa kamusi na nyenzo za kileksikografia kwa takribani lugha 100 na kuziweka mtandaoni ili ziwafikie watumiaji wengi kwa muda mfupi.
Kwa mara ya kwanza, maneno mengi ya kileksikografia na yenye ubora wa kipekee yatatungwa, yatakusanywa na kuwekwa wazi, katika mtandao mmoja, kwa watafiti, wanafunzi na watumiaji wengine.
“Uzinduzi wa OGL Kiswahili unatoa fursa ya pekee kwa watumiaji wa Kiswahili kote duniani kupata, kwa urahisi, maneno ya Kiswahili yaliyofanyiwa utafiti mpana na kutolewa maelezo ya kina,” anasema Fatma. Lengo kuu la mradi wa OGL anasema ni kuleta mapinduzi kwa mamilioni ya watu duniani kwa kurahisisha upatikanaji wa lugha zao katika mfumo wa dijitali, tovuti, programu za simu na vifaa mbalimbali.
Mkurugenzi wa Kamusi za Oxford, Judy Pearsall, anasema OGL ni hatua madhubuti iliyochukuliwa na Oxford University Press kutokana na changamoto za kisasa na fursa kubwa iliyopo kutokana na mtandao wa intaneti na athari zake katika upanuzi wa lugha na uwezo wake wa ufanisi.
“Kote duniani, mawasiliano kwa njia ya dijiti yanaendelezwa hasa kwa Kiingereza na lugha nyingine zinazozungumzwa kote duniani kama vile Kichina, Kifaransa na Kihispania hivyo Kiswahili kitakuwa katika mfumo mpya ambao utawezesha kukua zaidi kama lugha zingine.
Kitengo cha Kamusi za Oxford kimebuni mfumo uitwao Lexical Engine and Platform (LEAP) ambapo data zitajumuishwa, zitasanifiwa, kisha kuenezwa ili kusaidia lugha kuhifadhiwa na kuhakikiwa katika mfumo mmoja. Oxford University Press ni nini? Kampuni ya Uchapishaji ya Oxford University Press (OUP) ni idara katika Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza.
Inaendeleza lengo la chuo la ubora katika utafiti, ufadhili wa masomo na elimu kupitia vitabu inavyochapisha kote ulimwenguni. OUP ndiyo kampuni kubwa zaidi duniani na inafika sehemu nyingi zaidi duniani kwani inachapisha maelfu ya vitabu vipya kila mwaka katika ofisi zake zilizopo katika takribani nchi hamsini na imeajiri watu wapatao 7,000 duniani kote.
Kama wachapishaji wa kamusi maarufu ya Kiingereza duniani ya Oxford English Dictionary, Oxford inaongoza duniani katika usambazaji wa vitabu vya Kiingereza mbali na kuwa inachapisha vitabu katika lugha zaidi ya 40.
Kwa ushirikiano na wataalamu wa teknolojia ya lugha, wana leksikografia wa Oxford na watafiti wa lugha ni kielelezo katika kuunda matini ya lugha iliyo mwafaka kwa mfumo wa dijiti, pamoja na kuwa wanatoa matini ya lugha iliyo mahususi kwa kampuni kubwa za teknolojia duniani.
Kwa sasa, kuna jopo jipya Oxford ambalo linaangazia lugha za dunia na zile za jamii-lugha ambazo hazina nyenzo za kutosha, haziwezi kufikia kwa urahisi vyombo vya kidijiti na zipo katika hatari ya kuachwa nyuma katika mfumo wa dijiti.
Programu hii mpya ya Oxford imeundwa ili kuwasaidia mamilioni ya watu kote duniani kutunga, kudumisha na kutumia nyenzo za lugha ambazo watahitaji na wakati huo huo wakiunda mfumo wa matini ya kidijiti ambao utazinduliwa ili kutosheleza utashi wa lugha kutoka kwa kampuni za kiteknolojia duniani.
Majaribio ya kuibuka na hali itakayomnufaisha kila mmoja yalihusisha jamii kuchangia matini. Wenye kupewa leseni watachukua matini hayo pamoja na mfumo mpya wa kidijiti watakaouhitaji na Oxford itagharimia uchapishaji na kudumisha huduma hii kwa watu wote bila malipo.
Ili kuunga mkono mradi huu muhimu, wataalamu wa teknolojia wanabuni mfumo ambao utaoanisha na kuleta pamoja matini ya lugha.

No comments