Header Ads

WATU watatu wamekufa wilayani Kalambo mkoani Rukwa kwa kupigwa na radi


 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, George Kyando


WATU watatu wamekufa wilayani Kalambo mkoani Rukwa wakiwemo wawili wa familia moja kwa kupigwa na radi, huku mtoto mwenye umri wa miaka miwili akifa maji wakati akijaribu kuvuka mto kumfuata baba yake mzazi aliyekuwa akifua nguo zake mtoni.
Katika tukio la kupigwa radi ambalo lilihusisha watu wa familia moja, mtoto wa miaka mitano alijeruhiwa vibaya baada ya kupigwa na radi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, George Kyando alimtaja mtoto huyo kuwa ni Barick Gervas (2) mkazi wa Kijiji cha Mombo katika Kata ya Legezamwendo wilayani Kalambo ambaye alikufa maji wakati akijaribu kuvuka mtoto akimfuata baba yake mzazi, Gervas Bitwelo (25) aliyekuwa akifua nguo zake mtoni hapo.
Kamanda Kyando alisema kifo hicho kilitokea Machi 15, mwaka huu saa tano asubuhi katika Kijiji cha Mombo kilichopo katika Kata ya Legezamwendo wilayani Kalambo.
Katika tukio lingine, watu wawili wa familia moja wakazi wa Kijiji cha Mpanga, Samwel Siame (30) na Makuto Siame (13) ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mpanga walikufa baada ya kupigwa na radi wakiwa ndani ya nyumba yao kijijini humo.
Kwa mujibu wa Kamanda Kyando, katika ajali hiyo iliyotokea Machi 15, mwaka huu, mtoto mwenye umri wa miaka mitano wa familia hiyo, Assa Siame alijeruhiwa vibaya baada ya kupigwa na radi na amelazwa katika Zahanati ya Mpanga akitibiwa.

No comments