Header Ads

Kutembeza chakula wazi hatari kwa afya




MFANYABIASHARA wa vyakula, matunda yaliyomenywa na juisi zinazoandaliwa nyumbani, kwa ajili ya mlo wa asubuhi, mchana au usiku, anapaswa kuzingatia masharti ya msingi ya afya, kuepuka kumsababishia mteja wake (mlaji) madhara ya kiafya.
Wafanyabiashara wanapaswa kuzingatia usafi na kuhakikisha vyakula vinafunikwa wakati wote vinaposafirishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Kwa ufupi, kuvifunika ni ishara kuwa mfanyabiashara anajali usafi wa mazingira anayouza vyakula na kuthamini ulinzi wa afya ya mteja.
Kitabu kiitwacho Kitchen Companion: Your Safe Food Handbook, kinachoelezea miongozo mbalimbali ya namna mlo wa nyumbani na wa biashara unavyoweza kuandaliwa, kwa kuzingatia usalama wa afya ya mlaji na muandaaji mwenyewe, jinsi ya kuuhifadhi na kuusambaza kwa watu (kuhudumia wateja chakula) kinasema, kwa sababu ya uzembe tu mteja anaweza kusababishiwa maradhi.
Kwa mujibu wa kitabu hicho, usalama wa chakula ni muhimu wakati wa kukiandaa, kukigawa kwa walaji na wakati wa kukila pia. Kinasema, “Makosa yanayofanywa na muandaaji wa chakula au kimiminika, mfano juisi inayotakiwa kutengwa mezani pamoja na chakula, yanaweza kumfanya mlaji apate matatizo ya kiafya yenye madhaa ya muda mrefu, kilema au kupoteza maisha”.
Kitabu hicho kinaeleza kuwa, muandaaji wa chakula au juisi anapaswa kuwa na mikono misafi wakati wote. Hiyo ina maana kuwa, mpishi, kabla ya kuandaa vifaa muhimu vya kupika, ni lazima anawe mikono kwa sabuni na kuisuuza vizuri kwa maji safi isibaki na harufu, hata kama ni nzuri.
Mbali na hayo, kitabu hicho kinasisitiza umuhimu wa kuwa na vifaa vya kusafirishia vyakula, vinavyo takiwa kupelekwa kwa mlaji kutoka upande A wa eneo vinako andaliwa au kupatikana, kwenda upande B vinakotakiwa kuliwa.
Ingawa maelezo hayo hayajalenga moja kwa moja kuwa anayepelekewa chakula hicho, akiwa upande B ni mteja na anayeandaa akiwa upande A ni mfanyabiashara, yanatoa majibu ya nini kinapaswa kuzingatiwa na mtu yeyote wakati wa kusafirisha chakula.
Kwa kuzingatia maelezo ya kitabu hicho, ifahamike kuwa, kusafirisha chakula kwa kuzingatia masharti ya afya, hakutegemei umbali kinako takiwa kufikishwa, ilimradi kunakuwa na hatua kadhaa, uwezekano wa kukifikisha kikiwa kichafu upo kwa asilimia 100.
Wataalamu wa masuala ya usalama wa chakula kutoka katika mtandao huu; www.fsis.usda.gov, wanasema, kwa kuzingatia usalama wa chakula na wa mlaji, kinapoandaliwa, kinapaswa kiliwe wakati huo.
Aidha, mtandao huo unaeleza kuwa, endapo walaji wanakuwa mbali na chakula kinapoandaliwa, muandaaji wa meza (mhudumu) au mpishi, anapaswa kuwa makini kutekeleza yafuatayo;
(i). Kuhakikisha hakiandai mapema zaidi ya muda unaostahili mlaji kusubiriwa.
Inaelezwa kuwa, si vizuri kwa usalama wa chakula, kukiandaa mapema na kukiacha kwa zaidi ya saa tano kabla ya kuliwa. Mtandao huo unasema, kufanya hivyo ni kulazimisha watu wale kiporo, kwa sababu kitahitaji kurudishwa kwenye moto.
“Lakini, kwa waandaaji wenye vifaa vya upishi vya kisasa, wanaweza kuandaa vyakula saa tatu kabla ya watu kukaribishwa mezani, kwa sababu wanakuwa wameviacha kwenye moto mdogo wakati wote... haviwi viporo.”
(ii). Kuhakikisha kimefunikwa wakati wote, hata kama baada ya dakika chache tangu kiandaliwe, mteja au mlaji atakuwa amekwishafika mezani tayari kuanza kula.
Inaelezwa kuwa, hilo linapaswa lifanyike endapo mteja au mlaji hayuko mbali.
Kuhusu kuhudumia chakula mbali na mahali kinapoandaliwa, mfano upande wa pili wa barabara au katika shule iliyoko nje ya kinapoandaliwa, muandaaji au mhudumu wa chakula anapaswa;
(a). Kuwa na kifaa maalum cha usafirishaji ikibidi kiwe na matairi kuepusha kubeba chakula au vyakula mkononi. Ubebaji wa vyakula kwa mikono huku vikiwa wazi, kutokana na maelezo ya the Kitchen Companion, unaweza kuleta hatari mbalimbali ikiwemo kumwagika.
Hata hivyo, kumwagika huko kunaweza kusiwe suala kubwa sana kwa sababu, katika eneo la wazi, mbebaji hawezi kujaribu kukiokota, badala yake ataishia kupoteza muda wa msubiri chakula, kwa kurejea jikoni kuchukua kingine.
Hatari nyingine ambayo kitabu hicho kimeieleza na kusisitiza kuwa ndio yenye kuweza kusababisha mlaji aathirike, ni ya kuguswaguswa kwa vyakula vilivyo wazi ikiwa ni jitihada za mbebaji kuhakikisha havitoki kwenye sahani na kumwagika.
Kinasema kuwa, wakati anapokuwa amebeba vyakula au matunda yaliyomenywa bila kufunika, huku akitembea kumfuata mlaji na wakati mwingine kulazimika kuvuka barabara, anakuwa akigusa nguo zake, kujigusa katika maeneo mengine ya mwili wake, au kugusana na watu, kushikana mikono pindi wakisalimiana.
“Kitendo hicho kinatoa mwanya kwa bakteria walio katika vumbi na uchafu mwingine wa mikononi, kuhamia katika vyakula alivyovibeba, hasa wakati akivishika kwa lengo la kuviweka sawa kwenye sahani”,ilisema sehemu ya kitabu hicho.
Kwa ufupi, kitabu hicho kinaonya kuwa, kutembeza chakula kikiwa wazi ni hatari kwa afya ya mlaji.
Pia kina ongoza kuwa, hata kama hakisafirishi, chakula kikiandaliwa na kumsubiri mlaji mezani ni lazima kifunikwe kwa namna inayozingatia usafi.
Kitabu hicho kinataja bakteria wa aina mbili; ajulikanaye kwa jina pathogenic, anaye sababisha mlaji wa chakula chenye uchafu kuumwa na mwingine, spoilage bacteria, anayefanya chakula kichache.

No comments