RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ameongoza wananchi kumuagaClement George mwanasiasa mkongwe
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ameongoza wananchi na viongozi mbalimbali wa dini na siasa katika tukio la kumuaga mwanasiasa mkongwe na Waziri katika Serikali ya Tanganyika, Clement George Kahama (Sir George Kahama) aliyezikwa Machi 16 katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Mbali ya Mzee Mwinyi, wengine walioshiriki ni Marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.
Viongozi mbalimbali walisema Kahama (89) aliyefariki Machi 12, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matatizo ya figo, alionesha ubora wa uongozi unaostahili kuigwa.
Rais mstaafu Mwinyi alisema Kahama ameacha historia nzuri duniani kutokana na utendaji kazi wake. “Huu ni msiba mzito kwa Watanzania…,” alisema Mwinyi.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema Sir George Kahama alijenga msingi wa uongozi kwa taifa na alikuwa mstari wa mbele kupigania uhuru wa taifa.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akisema Kahama alitoa mchango mkubwa kwa Chama tangu enzi ya TANU kupigania uhuru hadi kuundwa CCM.
Alisema Kahama aliitumikia Serikali kwa uzalendo na alikuwa hazina kubwa na mchapakazi.
“Hatunaye leo ni kweli tunahuzunika, lakini kwa mchango wake mkubwa tunafarijika sana kwa utumishi wake uliokuwa wa hali ya juu,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Edward Lowassa ni miongoni mwa watu waliomuaga Sir Kahama.
Mbowe alisema katika Baraza la Kwanza la Mawaziri, Kahama alikuwa na sifa iliyomtofautisha na wengine ambayo ni uchapakazi na msimamo wa hali ya juu.
Post a Comment