Iraq na Syria zimetangaza ushindi dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu
Iraq na Syria zimetangaza ushindi dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu
Iraq na Syria zimetangaza ushindi dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu katika wiki za karibuni, baada ya mwaka mmoja ulioshuhudia mataifa ya nchi hizo, washirika kadhaa wa kimataifa na vikosi mbalimbali vya ndani vikiwafurusha wapiganaji kutoka miji na vijiji vilivyounda himaya ya ukhalifa lililokuwa limejitangazia kundi hilo.
Marekani imeongoza muungano wa kijeshi wa kimataifa ulioendesha kampeshi ya mashambulizi ya ndege dhidi ya Dola la Kiislamu tangu 2014, wakati kundi hilo lilipoteka theluthi moja ya ardhi ya Iraq. Wanajeshi wa Marekani wametumika kama washauri kwa vikosi vya ardhini vya Iraq na makundi ya Kikurdi na Kiarabu nchini Syria.
Muungano huo umeliambia shirika la habari la reuters katika taarifa kwa njia ya barua pepe, kwamba kuna magaidi chini ya 1,000 wa IS katika eneo lao la pamoja la operesheni, ambapo wengi wao wanaendelea kusakwa katika maeneo ya jangwa mashariki mwa Syria na magharibi mwa Iraq. Idadi hiyo haihusishi maeneo ya magharibi mwa Syria yalio chini ya udhibiti wa serikali ya rais Bashar al-Assad na washirika wake.
Mshirika mkuu wa Assad, Urusi nayo imetangaza leo kuwa vita kuu na Dola la Kiislamu vimekwisha. Waziri wa mambo ya kigeni Sergei Lavrov, alisema jukumu muhimu kwa sasa ni kuliangamiza kundi jengine la Kiislamu, la Nusra Front.
"Jeshi la Syria, pamoja na washirika wake na kwa msaada wetu, linapambana na wapiganaji wa Al-Nusra Front, lakini wanaweka upinzani, kutokana kwa sehemu, kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, na msaada wa kutoka nje," alisema Lavrov alipokutana na kiongozi wa upinzani kutoka Syria Ahmed Jarba mjini Moscow.
Muungano wa Marekani ulisema Desemba 5 kwamba kulikuwa na chini ya wapiganaji 3000 waliosalia. Iraq ilitangaza ushindi wa mwisho dhidi ya kundi hilo Desemba 9. Muungano huo umesema wengi wa wapiganaji hao ama waliuawa ua kutekwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Urusi yaituhumu Marekani kwa kuwapa mafunzo IS
Wakati huohuo, mkuu wa wa majeshi ya Urusi ameituhumu Marekani kwa kuwapa mafunzo wapiganaji wa zamani wa IS nchini Syria, ili kuivuruga nchi hiyo, madai yake yakijikita kwenye kituo cha kijeshi cha Marekani kilichopo kwenye eneo la kimkakati la Taf kwenye kivuko kati ya Syria na Iraq. Urusi inasema kituo hicho kipo kinyume na sheria na kwamba chenye pamoja na eneo linalokizunguka vimekuwa tundu jeusi ambamo wapiganaji wanaendesha shughuli zao bila kizuwizi.
Na kwingineko shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema wapiganaji kutoka jamii ya Yazidi ya nchini Iraq, ambayo ilikandamizwa vibaya na Dola la Kiislamu, wamliwauwa raia 52 katika tukio linalodhihirika wazi kuwa la ulipizaji kisasi, baada ya kuteka maeneo kutpkakwa wapiganaji hao.
Human Rights Watch imesema katika ripoti yake kuwa ndugu wa wahanga hao waliiambia kuwa Juni 4, 2017, vikosi vya Yazidi viliwazuwia na kuwachinja wanaume, wanawake na watoto, kutoka familia nane za kabila la Wasunni la Al-Bu Metewut, ambao walikuwa wakikimbia mapingano kati ya IS na wapiganaji wanaoiunga mkono serikali kaskazini mwa mji wa Mosul.
Post a Comment