Kiungo wa Kevin Prince Boateng alifunga
Kiungo wa Kevin Prince Boateng alifunga baso safi la ushindi zikiwa zimesalia dakika kumi mechi kukamilika, na kuipa ushindi Eintracht Frankfurt wa 2-1 dhidi ya klabu yake ya zamani Hertha Berlin
Matokeo hayo yamewapandisha Frankfurt hadi nafasi ya nane, wakati Hertha wako katika nafasi ya 12, ikiwa ni pengo la pointi tano tu kutoka eneo la kushushwa ngazi. Niko Kovac ni kocha wa Frankfurt. "Hertha walicheza vuzuri sana katika kipindi cha kwanza. Na wakati wao walikuwa wazuri, sisi hatukucheza kabisa, tulishindwa katika kila pambano, na hatukuwa wakakamavu kabisa. Baada ya kusawazisha moja kwa moja tulibaki mchezoni na tukapata ushindi ambao tulistahili".
Borussia Monchengladbach walikosa nafasi ya kupanda hadi nafasi ya pili baada ya kuchabangwa tatu bila na Wolfsburg. Matokeo hayo yamewaweka Gladbach katika nafasi ya nne wakati Wolfsburg wakisonga hadi nafasi ya 11. Daniel Didavi ni mshambuliaji wa Wolfsburg "Kila mara mimi husema sisi sio timu inayopaswa kuwa katika vita vya kushushwa ngazi. Tuna uwezo mkubwa sana, ni vile tu hatujawahi kuutumia. Sasa tunaweza kutumia. Kinachokosa tu ni mwendelezo, na kama tutafanya hivyo kwa wiki kadhaa, basi karibuni tutakuwa mahali pengine".
Siku ya Jumamosi, Bayern waliutanua uongozi wao kileleni na pengo la pointi sita baada ya kuifunga Hanover mabao matatu kwa moja. Nambari mbili RB Leipzig walizabwa nne bila na Hoffenheim, katika mechi ambayo DW Kiswahili ilikutangazia moja kwa moja,
Borussia Dortmund waliteremka hadi nafasi ya sita baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja na Bayer Leverkusen. Dortmund sasa hawajashinda mechi yoyote kati ya saba za mwisho. kocha wa BVB Peter Bosz anakabiliwa na shinikizo lakini uongozi wa klabu yake unamuunga mkono…angalau kwa sasa. Msikilize Bosz "Tulicheza ovyo sana, hasa katika udhibiti wa mpira. Wachezaji wazuri kila mara huwa watulivu wakiwa na mpira na sio kuupoteza. Hilo halikufaa kabisa kwa sababu tuna nafasi ya kujijenga na kucheza kandanda, lakini unaweza kuhisi wakati wa shinikizo, hata wachezaji wazuri hupoteza mpira".
Schalke ilikosa nafasi ya kupanda hadi nafasi ya pili kutoka ya tatu baada ya kutekwa kwa sare ya mabao mawili kwa mawili na washika mkia Cologne. Matokeo hayo yalitosha kuwashawishi viongozi wa Cologne kuwa sasa ni wakati wa kumwambia kwaheri kocha wa Peter Stoeger, ambaye alionekana kuwaaga mashabiki baada ya mtanange huo. Stoeger aliyasema haya kabla ya kutimuliwa jana Jumapili "Angalau hiyo ni dalili kuwa walijiamini leo, kama tulivyojadili katika kipindi cha mapumziko: kuwa tuko nyuma na Schalke huenda ndio timu bora, kitu ambacho hakishangazi baada ya wiki chache zilizopita lakini kuwa nimeona uwezekano wa sisi kufunga, kuwa hawapo imara na chochote kinaweza kutokea, na kwa bahati nzuri waliitumia fursa hiyo pia. Kama haujashinda kwa muda mrefu basi inakuwa hatua nzuri ya kupata pointi tatu, lakini hatukufanya hivyo. Pointi moja ni nzuri na ni wazi kuwa tuna hamu ya kupata kitu kutoka kwa mchuano wa wiki ijayo dhidi ya Freiburg".
Kwingineko, Augsburg wako katika nafasi ya saba baada ya ushindi wao wa tatu moja dhidi ya Mainz. Werder Bremen wanabakia katika nafasi ya 17 hata ingawa walipata ushindi wa moja bila dhidi ya Stuttgart.
Post a Comment