KODI YA ARDHI AMBAYO IJAPIMWA ITAANZA KULIPIWA
SERIKALI imetangaza kuwa kodi ya ardhi kwa wamiliki wa majengo na maeneo makubwa mijini ambayo hayajapimwa, itaanza kulipwa rasmi Januari mwakani.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati wa ufunguzi wa kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasisi ya Wathamini, Maofisa Ardhi, Mawakala wa Miliki, Wasimamizi na Wachambuzi wa Miliki Kuu (TIVEA).
Lukuvi alisema wamiliki wa majengo na maeneo makubwa mijini ambayo hayajapimwa wataanza kulipa kodi ya ardhi kuanzia Januari mwakani kwa kuwa serikali inapoteza kiasi kikubwa cha fedha katika eneo hilo.
Alisema eneo hilo ni miongoni mwa maeneo yenye fedha nyingi, lakini wataalamu wameshindwa kuziona na kuipatia serikali mbinu ya kuzichukua. “Wenye majengo na wale wenye maeneo makubwa mjini wanaoyafanya kama mashamba lazima walipe kodi ya ardhi, wengine wamekuwa wakiuza ardhi kidogo kidogo kwa kuwakatia watu vipande bila ya kulipa kodi jambo hilo halitakubalika tena,” alisema Lukuvi.
Alisema hao wote lazima watafutiwe viwango vya kulipia kodi na jambo hilo limeanza kufanyiwa kazi. Lukuvi alisema macho ya Watanzania kwa sasa yanaangalia maeneo ya bandari na migodi ya madini kwamba ndivyo vyanzo vya mapato, lakini zaidi ya asilimia 80 ya majengo katika maeneo ya mijini hayalipi kodi ya ardhi kutokana na kujengwa katika maeneo ambayo hayajapimwa.
“Hata ninyi mnahusika, maana ninazo taarifa zenu kuwa mnachukua bahasha na kufanya vitu vya ovyo kabisa, naomba muache maana tumeshawabaini na lazima tutachukuliana hatua kwa haraka sana,” alisema Lukuvi katika mkutano huo unawashirikisha maofisa ardhi wa wilaya, wathamini wa serikali na binafsi na wakadiriaji.
Aidha, aliwanyooshea kidole wathamini kwamba wamekuwa wakiiumiza serikali kutokana na tamaa ya fedha kwani katika tathimini nyingi wanazofanya zimekuwa hazilingani na thamani halisi ya kile wanachokitathimini ukilinganisha na wathamini binafsi.
Katika hatua nyingine, waziri huyo alitangaza kuunda Bodi ya Wathamini kama sheria inavyomuelekeza na kuwateua wathamini wa kanda ili ifikapo Januari 2018, kusiwepo na masuala yote ya uthamini yaishie kwenye ngazi za kanda kama walivyopanga kuondoa ukilitimba.
Rais wa TIVEA, Linus Kinyondo alisema wathamini wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya kukosa usajili utakaowezesha kufanya kazi yao kulingana na sheria na akahoji ni lini bodi hiyo itaanza kufanya kazi.
Kinyondo alitaja changamoto nyingine kuwa ni gharama ya ada ya uthamini kwa ajili ya mizania ya shirika la umma lenye mali na kufanya watu wengi kuelewa na kushindwa kufanyia uthamini akaomba serikali kulitazama jambo hilo.
Mthamini Mkuu wa Serikali, Evalyne Mgasha alikiri kuwepo kwa rushwa katika baadhi ya maeneo kwa wathamini, lakini alitaja sababu za mgongano wa sheria unaosababisha baadhi ya watu kuhisi kuwa watumishi wa serikali wanawaonea.
Pia alisema muda wa ulipaji wa fidia kwa waliofanyiwa tathmini kwani sheria inataka walipwe mapema baada ya kufanyika kwa tathimini, lakini wamekuwa wakichelewa hadi kufikia zaidi ya miaka miwili bila ya kulipwa fidia yao
Post a Comment