TANZANIA hupoteza kiasi cha Sh bilioni 400
TANZANIA hupoteza kiasi cha Sh bilioni 400 kutokana na hali duni ya usafi hasa ukosefu wa huduma ya vyoo bora. Fedha hizo ni zile kwa kutibu maradhi yanayotokana na kukosekana kwa matumizi ya vyoo.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya taifa ya usafi wa mazingira. Makamu wa Rais alisema katika uzinduzi huo kuwa takwimu nchini zinaonesha watu wapatao 30,000 huugua magonjwa ya kuhara kila mwaka na baadhi yao hupoteza maisha. Idadi ya wanaougua ni sawa na wastani wa wagonjwa 83 kwa siku moja.
Alisema katika hotuba yake kwamba hapa nchini asilimia 40.5 pekee ya kaya ndizo zenye vyoo bora ambapo kaya zipatazo 600,000 hazina vyoo kabisa. “Hali hii inabainisha kiini cha kuendelea. Kushamiri kwa magonjwa ya kuambukiza hususan kuhara na kipindupindu ambapo hadi sasa kinajitokeza katika baadhi ya mikoa na halmashauri nchini,” alisema.
Akizungumzia hali ilivyo duniani Makamu wa Rais, alisema utafiti unaonesha kwamba watu wapatao bilioni 2.3 hawatumii vyoo bora duniani kote, hii ikiwa ni takribani theluthi moja ya watu wote duniani. Akizungumzia hali halisi nchini serikali imejiwekea mikakati mbalimbali ya kupambana na maradhi ya kuambukiza ambapo usafi wa mazingira ni njia mojawapo.
Kupitia awamu ya kwanza ya kampeni ya usafi wa mazingira alisema jumla ya kaya 1,662,550 zilijenga vyoo bora katika vijiji na mitaa ipatayo 6,628 aidha shule za msingi 2,133 zimejenga vyoo bora kwa kuzingatia mahitaji ya jinsia. “Hatuwezi kuzungumzia kujenga uchumi wa viwanda na kuelekea uchumi wa kati kama watu wetu wanakosa huduma ya vyoo bora, kimsingi hakuna utetezi unaokubalika wa mtu au kaya yoyote kukosa choo hata kile cha gharama nafuu,” alisema.
Makamu wa Rais alisema usafi wa mazingira ni mojawapo ya viashiria 169 vilivyopo kwenye malengo 17 ya maendeleo endelevu, kati ya malengo hayo 17, lengo la tatu linahusu uboreshaji wa afya na ustawi wa jamii na lengo la sita linahusu upatikanaji wa huduma za maji safi na salama na usafi wa mazingira.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema benki ya dunia iko tayari kuchangia fedha kuhakikisha kampeni hiyo ya usafi wa mazingira inatekelezwa. Akizungumza kwa niaba ya washirika wa Maendeleo, Elizabert Arthur alisema takwimu zinaonesha watoto 18,500 wanapoteza maisha kila mwaka, ikiwa na maana ya watoto 50 kwa wiki na watoto wawili kwa saa.
Post a Comment