Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha tuhuma
Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha tuhuma Yakwamba anapanga kumfuta kazi mwendesha mashtaka maalum Robert Mueller, ambaye amekuwa akiongoza uchunguzi kuhusu madai kwamba Urusi waliingilia kati uchaguzi wa mwaka 2016 nchini Marekani.
Uhasama umekuwa ukiongezeka kati ya White House na Bw Mueller na maafisa wake.
Jumamosi, wakili wa kundi la watu waliomfanyia kampeni Bw Trump alisema maelfu ya barua pepe zilikuwa zimechukuliwa kinyume cha sheria na kundi la bw Mueller.
Akijibu maswali kuhusu mzozo huo wa kisheria, Bw Trump alisema hali "si nzuri sana" na kwamba watu wake "wamejawa na ghadhabu".
"Siwezi nikafikiria kwamba kuna chochote (ndani ya barua pepe hizo), kwa kweli, kwa sababu, kama tulivyosema, hatukushirikiana nao (na Urusi)," alisema baada ya kurejea kutoka safari ya wikendi Camp David.
Utawala wake umekanuisha tuhuma kwamba ulishirikiana na Urusi wakati wa uchaguzi wa mwaka 2016 na Bw Trump amedai tuhuma hizo ni za kumwandama tu bure.
Akijibu swali kutoka kwa wanahabari akiwa White House kuhusu iwapo anapanga kumfuta kazi Mueller, Bw Trump alijibu: "La hasha".
Wabunge akdha wa chama cha Democratic wameeleza wasiwasi wao, na siku ya Ijumaa afisa mkuu wa chama hicho katika kamati ya ujasusi Bungeni Adam Schiff, alisema ana wasiwasi kwamba wabunge wa Republican wanataka kulemaza uchunguzi huo.
Maafisa kadha wa zamani wa kampeni wa Bw Trump wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali kama sehemu ya uchunguzi huo.
Wakili anayefanya kazi na kundi la Trump for America (TFA) ambalo lilisaidia Donald Trump kipindi cha mpito kuingia White House baada ya kuchaguliwa kwake, alilalamika Jumamosi kwamba kundi hilo limefahamu maafisa wa Mueller wamepata maelfu ya barua pepe za kundi hilo.
Kory Langhofer alituma barua kwa kamati za Bunge la Congres akidai kwamba barua hizo zilichukuliwa kwa njia iliyo kinyume cha sheria.
- Kundi la TFA lilitumia mitambo ya shirika la serikali kuhifadhia data katika kipindi kati ya kuchaguliwa kwa Trump Novemba 2016 hadi alipoapishwa Januari 2017.
Barua pepe hizo zinadaiwa kujumuisha barua za maafisa 13 wa mpito wa Bw Trump, akiwemo mshauri wa zamani wa masuala ya usalama wa taifa Michael Flynn ambaye alikiri kutoa taarifa za uongo kwa FBI mapema mwezi huu.
Msemaji wa Bw Mueller amesema hawakufanya makosa yoyote.
"Tumezipata barua pepe katika shughuli zetu za kuendelea na uchunguzi wa jinai, tumepata idhini ya mmiliki wa akaunti hizo za barua pepe au tukafuata shughuli inayofaa kisheria," Peter Carr alisema.
Post a Comment