Header Ads

MKUU wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu amefunguka kuhusu mambo juu ya utendaji wa jeshi hilo na kueleza kuwa wakati wowote litamburuza mahakamani Katibu Mkuu wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad kwa kuhamasisha uchochezi visiwani Zanzibar.


Amebainisha kuwa jeshi hilo, kamwe halikandamizi wala kuonea chama chochote cha siasa, kwani limekuwa likitekeleza wajibu wake kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo. 


Akizungumza katika mahojiano yaliyofanyika kwenye kipindi cha Funguka, kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Azam jana, IGP Mangu alisema hali ya siasa Zanzibar ilikuwa shwari katika chaguzi zote mbili na kwamba machafuko na vurugu vilianza kutokea baada ya uchaguzi wa pili. 


Alisema vurugu hizo zilianza baada ya kubainika kuwa Maalim Seif, alikuwa akifanya mikutano ya ndani na mingine ya chini kwa chini na wafuasi wake katika maeneo ya Kaskazini na Kusini. 


“Kwa sababu ilikuwa ni mikutano ya ndani, Polisi hatukuona tatizo na wala hatukumzuia, tuliona ni mwananchi anataka kuzungumza na wafuasi wake, tukasema mwache aongee nao tu,” alisema IGP Mangu. 


Alisema baadaye jeshi hilo liligundua kuwa kiongozi huyo wa CUF, alikuwa anawachochea wananchi waichukie serikali iliyopo madarakani na wapinzani wao ambao ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwafanyia uhalifu. 


Alisema baada ya vikao hivyo vya Maalim Seif, visiwani humo kukaanza kuibuka matukio ya vurugu kama vile mashamba kuchomwa moto na mazao kung’olewa. 


“Haya mambo hayakutokea kabla ya vikao vya Seif, yalitokea baada ya vikao vyake,” alifafanua mkuu wa polisi. 


Alisema wafuasi hao walichochewa, kiasi cha kususa hadi shughuli za kijamii, kama vile misiba na wakati mwingine ilifikia hatua ya kususa kuwauzia bidhaa wafuasi wa CCM. 


“Tukasema kama wameona kugeuza biashara zao siasa, basi waendelee tu. Biashara inadumu kwa sababu unatengeneza faida, sasa kama umeamua kuchagua wa kumuuzia ni shauri yako. Hawa tuliwaacha kwa sababu tuliona hawana makosa,” alisema. 


Hata hivyo, alisema jeshi hilo kamwe halikuwanyamazia wahalifu waliochoma na kung’oa mazao kwenye mashamba ya wenzao, eti tu kwa kigezo cha ufuasi wa chama au siasa. 


“Hawa tuliwakamata na wapo wengine tunaendelea kuwatafuta, watakapoacha ndio hatutawatafuta. Wale wahalifu ndio tunaowatafuta. Pengine kwa sababu ya siasa wanadhani Polisi tunawaonea wananchi tunawakamata bila sababu. Sasa hawa watu tunawaoneaje wakati tunawapeleka mahakamani?” Alihoji. 


Maalim Seif kuhojiwa 
Alisema kutokana na matukio hayo, tayari Maalim Seif amehojiwa na jalada lake halijaamuliwa, lipo kwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) Zanzibar. “Lakini pia tunataka tumpeleke mahakamani kumshitaki kwa makosa aliyofanya ya kuchochea fujo,” alieleza. 


Alisema kazi kubwa ya Polisi kwa sasa si kujiingiza kwenye siasa au kupatanisha pande mbili zinapokwaruzana, bali kazi yake ni kuhakikisha inadhibiti na kuwakamata wahalifu. 


Alisema endapo vyama viwili vinavyolumbana visiwani Zanzibar, vitaamua kuchukua hatua za kisheria kumaliza tofauti zao, polisi haina tatizo, lakini endapo vyama hivyo vitachukua hatua za kijinai au kukomoana, jeshi hilo halitokaa kimya. 


“Kazi ya polisi iko wazi, tunakamata tunapeleleza na kupeleka mahakamani umma unatuona tunachofanya hatuna cha kuficha,” alisisitiza. 


Maandamano na mikutano 
Akizungumzia madai ya jeshi hilo kukandamiza demokrasia na wapinzani kwa kudhibiti shughuli za siasa nchini, IGP Mangu alisema hakuna mwanasiasa au chama chochote, kilichozuiwa kufanya shughuli zake, ikiwemo mikutano. 


Alisema kinachotakiwa ni kwa mwanasiasa au chama hicho, kupeleka maombi yake Polisi kwa mujibu wa sheria na baada ya jeshi hilo kufanyia tathmini maombi hayo, endapo yataonekana hayana tatizo yataruhusiwa kuendelea. 


Alisema endapo jeshi hilo linazuia shughuli za kisiasa, hutokana na uchunguzi au tathmini lililofanya na kujiridhisha kuwa shughuli husika si salama na inatishia usalama wa raia. 


“Unajua unapozungumzia masuala hayo tuwe makini kidogo, kwa sababu hapa kuna watu wa aina mbili kuna wanaofanya siasa na sisi watendaji tunaotekeleza sheria. Ila sisi pia hatuko juu ya sheria, kama kuna mahali tunakiuka upo utaratibu wa kutushughulikia,” alisisitiza. 


Alisema hata katika suala la kuzuia shughuli za kisiasa, kama vile mikutano na maandamano endapo, kuna chama au mwanasiasa anahisi kuwa jeshi hilo, halikutenda haki au limeenda nje ya mstari, taratibu zinamruhusu kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais na Mahakama. 


Hata hivyo, alisema jeshi hilo halifanyi jambo lolote nje utaratibu wa kisheria, akifafanua, “lakini sisi hatuwezi kujiingiza kwenye siasa kwa sababu sisi sio wanasiasa, pia hatuwezi kuzuia wanasiasa kulumbana kwa sababu ni uwanja wao wa kulumbana. Sasa kama tulitoa maelekezo fulani basi ujue tulikuwa tunatekeleza sheria na utaratibu uliopo.” 


“Sidhani kama sisi tunakandamiza upinzani, tunachofanya sisi ni kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na watu wako huru kama wanafikiri tumeenda nje ya mipaka yetu wakatuchukulie hatua,” alisisitiza. 


Alitoa mfano wa matukio yaliyozuiwa na Polisi kwa sababu za kiusalama kuwa ni pamoja na mkutano wa mahafali wa Dodoma, ambao ulifanyika siku moja na mkutano wa mahafali uliofanyika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam ambao wenyewe haukuzuiwa. Yote ilikuwa mikutano ya wanafunzi wafuasi wa Chadema. 


“Kama sisi tuna sera ya kuzuia, mbona wa Karimjee hatukuuzuia? Dodoma kulikuwa na sababu na imeelezwa na viongozi wa Dodoma. Hii si sera yetu, usichukulie mkutano mmoja kuzuiwa basi ndio yote nchi nzima imezuiliwa. Haiwezekani,” alifafanua. 


Alisema sheria inazungumzia wanaohitaji kufanya mkutano au kufanya maandamano, wanatoa taarifa kwa mkuu wa polisi wa hilo eneo, na mkuu huyo ataangalia kama mazingira yanaonesha hakuna tatizo, mkutano utaendelea, kama kuna tatizo atauzuia. 


“Sasa ni wapi sisi tumefanya kitu ambacho ni kinyume na tunaonekana tunakandamiza upinzani? Na ikumbukwe kuwa kuna mikutano baadhi iliombwa tukaizuia kwa sababu kipindi hicho kulikuwa na kelele za mauaji Mwanza, Sengerema, Tanga mpaka tunahojiwa Polisi mko wapi,” alisema. 


Alisema wakati Polisi ikihojiwa kuhusu dawa ya mauaji, baadhi ya vyama viliwasilisha maombi ya maandamano. 


“Hivi kweli? Kwanza mauaji yenyewe mtindo wake ni mpya unajuaje kama wanaoomba wangeenda nao kuvamiwa? Lazima tuchukue tahadhari,” alisema na kuongeza kuwa Polisi imepewa jukumu la kisheria kuhakikisha panakuwepo na amani. 

“Sasa tunapochukua hatua kuhakikisha kuna amani, naomba tuvumiliane. Msione kuna amani, basi mkajua ipo tu na ni ya kudumu, mjue kuna wengine wameumia kuhakikisha hiyo amani inakuwepo. Lazima iwe hivyo ndio utaratibu wa kuongoza nchi, sisi hatubagui wala kukandamiza chama chochote,” alieleza IGP Mangu. 


Matumizi ya nguvu 
IGP Mangu alisema si kweli jeshi hilo limekuwa likitumia zaidi nguvu katika kudhibiti vurugu na kubainisha kuwa nguvu hutumika, pale tu inapobainika kuwa upande wa pili unaodhibitiwa nao unatumia nguvu. 


Hata hivyo, alisisitiza kuwa Polisi nchini imekuwa ikitekeleza wajibu wake vyema bila kukandamiza wala kutumia nguvu, kwani hata taasisi ya kimataifa iliyofanya tathmini juu ya utendaji wa jeshi hilo katika uchaguzi mkuu nchini ilibainisha kuwa jeshi hilo lilifanya vyema. 


Polisi na rushwa 
Akizungumzia tuhuma zinazorushiwa Jeshi la Polisi kwamba kuna baadhi ya askari wake, wanatuhumiwa kwa rushwa, alisema askari hawana mamlaka ya kula rushwa na kujilimbikizia mali halafu wasiguswe na mtu.


“Hili haliwezekani. Kwa hiyo nasema bado wananchi wanaweza wakasaidia kama kweli wanazo taarifa za Polisi na zitafanyiwa kazi. Kama hawaamini kama sisi wenyewe hatuwezi kudhibitiana, vipo vyombo vingine vinaweza kufanya hivyo,” alisema. 


Hata hivyo, alisema wapo askari Polisi wenye maisha mzuri kwa maana ya nyumba na magari, ambao wamepata mali hizo kupitia taasisi mbalimbali za mikopo ikiwemo Saccos ya Polisi, ambayo ndio kubwa nchini. 


“Askari polisi kumiliki gari nzuri si kosa, la msingi amepataje hilo gari, kama kuna polisi ana mali au gari isiyo na maelezo tuleeteni, polisi hazuiliwi kuwa na gari nzuri. Siku hizi kuna taasisi nyingi zinakopesha anaweza kukopa,” alisisitiza. 


Kashfa ya Lugumi 
Akizungumzia suala la kashfa ya mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara Said Lugumi, IGP Mangu alisema suala hilo lilichukuliwa na Bunge na kufanyiwa uchunguzi hivyo, matokeo ya uchunguzi hawezi kuyazungumzia. 


Alisema anachoweza kukizungumzia ni maelekezo ambayo jeshi hilo limepatiwa na Bunge, ambayo ni kukamilisha yale ambayo hayajakamilishwa. 


“Tunaendelea kuchukua hatua za kukamilisha.Kuhusu uchunguzi kazi ilifanywa na Bunge kwa anayetaka anaweza kuwasiliana na Bunge na kupatiwa matokeo kwa kuwa naamini Bunge linawakilisha wananchi, taarifa zao ziko wazi,” alisema.

No comments