Watoto wengi wameuwawa Afghanistan 2016, yasema UN
Idadi ya watoto waliouwawa katika machafuko ya Afghanistan katika nusu ya kwanza mwaka huu, imeongezeka ikilinganishwa na mwaka jana, limesema shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Afghanistan UNAMA.
Idadi hiyo imekuja katika ripoti ya katikati ya mwaka, iliyotolewa siku chache tu baada ya shambulio baya zaidi la bomu kuwahi kuikumba Kabul tangu uvamizi wa mwaka 2001, ulioongozwa na Marekani na kuufurusha utawala wa Taliban.
Jumamosi watu wasiopungua 80 waliuwawa na wengine 231 kujeruhiwa katika shambulio la kujitoa muhanga, wakati wa maandamano ya amani ya waafghanistan wa jamii ya wachache wa Hazara, ambao ni waumini wa Kishia. Wengi wa waliouwawa ni raia wa kawaida.
Kundi la dola ya kiislamu IS lilikiri kuhusika, jambo lililozua wasiwasi kwamba kundi hilo ambalo limekuwa katika maeneo ya mpakani ya mashariki mwa nchi hiyo karibu na Pakistan kwa mwaka mmoja uliopita, linapanga kustawisha uwepo wake Afghanistan, baada ya kupoteza maeneo mengi nchini Syria na Iraq.
Idadi hiyo ya watu waliouwawa Jumamosi haikuwepo kwenye ripoti hiyo ya UNAMA, kwani ripoti hiyo inaangazia wahanga wa kuanzia Januari 1 hadi Juni 30 mwaka huu. Inasema kwamba theluthi moja ya wahanga katika hiyo miezi 6 walikuwa watoto, huku 388 wakiuwawa na 1,121 wakijeruhiwa, hiyo ikiwa ni asilimia 18 zaidi ya nusu ya kwanza ya mwaka 2015.
Ripoti hiyo imetaja makabiliano baina ya wanamgambo na vikosi vya Afghanistan vinayoungwa mkono na NATO kama chanzo kikuu cha mauaji hayo. Idadi ya waliojeruhiwa imefikia kiwango cha juu zaidi tangu Umoja wa Mataifa uanze kutoa ripoti zake mwaka wa 2009, na umoja huo umeitaja idadi hiyo kama jambo la kushtusha na la aibu.
Takwimu hizi ni ishara ya ongezeko la ukosefu wa usalama unaoendelea kuikumba Afghanistan wakati ambapo kundi la Taliban linaeneza mashambulizi yake nchi nzima.
"Kila muhanga aliyenukuliwa kwenye ripoti hii, kutoka wale waliouwawa wakiwa wanasali, waliouwawa kazini, wakisoma, wakiteka maji, wakitibiwa hospitalini, kila mmoja anawakilisha kushindwa kwa dhamira, na huu unapaswa kuwa wito kwa pande zote zinazohusika katika mzozo huu kuchukua hatua zinazohitajika ili kupunguza mateso kwa raia," alisema mkuu wa UNAMA Tadamichi Yamamoto.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kwamba makundi yanayoipinga serikali kama Taliban yamechangia kwa asilimia 60 ya wahanga. Vikosi vya Afghanistan vimehusika kwa asilimia 22 ya majeruhi wote, na vikosi vya kimataifa vilivyosalia nchini humo vimesababisha asilimia 2 ya wahanga, huku asilimia 17 ikiwa haiwezi kutambulika iwapo ilisababishwa na pande moja ua mwengine.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema pande zote mbili zilisema zinajitolea kwa kiasi kikubwa, ingawa ni hatua chache mno zilizochukuliwa kuwalinda raia.
Majeruhi kutokana na mabomu yaliyotegwa barabarani yalipungua pakubwa kwa asilimia 21, jambo ambalo Umoja wa Mataifa unasema limetokana na kubadilika kwa mfumo wa machafuko hayo na pia mfumo mzuri wa serikali wa kufahamu palipo na mabomu.
Post a Comment