Nduguye Obama kumpigia kura Donald Trump
Nduguye wa kambo wa Rais wa Marekani Barack Obama, Malik, ametangaza kwamba atampigia kura mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump.
Malik ameamua kutounga mkono chama cha Democratic chake Rais Obama ambacho mgombea wake ni Hillary Clinton.
Amesema anampenda sana Bw Trump kutokana na “uwazi wake” na kuongeza kwamba amesikitishwa sana na uongozi wa Rais Obama.
Ameambia BBC kwamba anaamini BwTrump, ni mtu mwenye huruma, mkweli na mwenye ushawishi.
"Akizungumza kwenye runinga anaonekana mtu anasemaye ukweli, kuhusiana na dunia kwamba imeharibika na hakuna usalama,” amesema Bw Malik.
Malik, 58, kwa muda mrefu alikuwa mfuasi wa chama cha Democratic lakini anasema utawala wa nduguye umemfanya kubadilika na kuanza kuunga mkono Bw Trump.
Akizungumza awali na gazeti la New York Post la Marekani, Malik alisema jambo lililomtamausha zaidi ni hatua ya mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani FBI James Comey kupendekeza Bi Clinton asishtakiwe kutokana na hatua yake ya kutumia sava ya kibinafsi ya barua pepe akiwa waziri wa mambo ya nje.
Hajafurahia pia kwamba Bi Clinton na Rais Obama waliongoza vita vilivyopelekea kuuawa kwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi ambaye anasema ni mmoja wa marafiki zake wakuu.
- Sikiliza: Sababu ya nduguye Obama kumuunga mkono Trump
- Barua za babake Obama zafichuliwa
- Mkewe Obama amtambua mbunifu kutoka Kenya
Pia, hafurahishwi na hatua ya chama cha Democratic cha Marekani kuunga mkono ndoa za wapenzi wa jinsia moja.
“Nampenda Donald Trump kwa sababu anazungumza kutoka moyoni. Ningependa kukutana naye,” anasema.
Baba yao Barack Obama Sr., aliondoka Kenya mwaka 1959 Malik alipokuwa na umri wa mwaka mmoja na akajiunga na chuo kikuu cha Hawaii, ambapo alikutana nan a baadaye akamuoa mamake Rais Obama, Stanley Ann Dunham.
Malik Obama alikutana na Obama mara ya kwanza 1985.
Wawili hao hata hivyo wamekuwa wakigombana. Malik amekuwa akimshutumu nduguye akisema hajakuwa akimsaidia.
Malik aliwania ugavana Siaya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013 lakini akashindwa.
Amesema amejiandikisha kama mpira kura katika jimbo la Maryland na anapanga kupiga kura mwezi Novemba.
Bw Malik amesema hakuna uhasama mkubwa kati yake na Rais Obama lakini hamuamini sana. Amesema wakati Rais Obama alipokuwa akiomba kura alizungumza sana zake Kenya lakini alipoingia uongozini hajakuwa akiwasiliana nao sana.
Post a Comment