Header Ads

Benki ya Exim ya China kujenga reli ya kati Tanzania



Image copyrightSTATEHOUSE TANZANIA
Image captionDr John Pombe Magufuli
Benki ya Exim ya China imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani Bilioni 7.6 sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 16 za kitanzania kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mradi mkubwa wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa unaotarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha.
Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang amemueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma kuwa pamoja na kutoa fedha hizo zitakazofanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za reli ya kati benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalamu katika ujenzi na uendeshaji wa reli hiyo.
Pamoja na kukubali kutoa fedha hizo, Rais huyo wa Benki ya Exim ya China amempongeza Rais Magufuli na serikali yake kwa dhamira ya dhati ya kuiletea Tanzania maendeleo ikiwemo kuharakisha ujenzi wa reli ya kati na ameahidi kuwa benki yake itatoa ushirikiano wa karibu katika kufanikisha mradi huo na miradi mingine ya maendeleo.
Image copyrightSTATEHOUSE TANZANIA
Kwa upande wake Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang kwa kukubali kutoa fedha hizo na amemuhakikishia kuwa Tanzania imedhamiria kutekeleza mradi huo ambao tayari ujenzi wake umepangwa kuanza
katika mwaka huu wa fedha kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha shilingi Trilioni 1 zilizotengwa katika bajeti.
Rais Magufuli amebainisha kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kutasaidia kuinua uchumi wa Tanzania na nchi jirani zisizopakana na bahari zikiwemo Uganda,Rwanda, Burundi, na Congo.
Mradi wa ujenzi wa reli ya kati utahusisha ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa kutoka Dar es salaam-Tabora- Isaka-Mwanza, Tabora-Mpanda-Kalemela, Tabora-Uvinza- Kigoma na Isaka-Keza- Msongati.
Mazungumzo kati ya Rais Magufuli na Rais wa benki ya Exim ya China yamehudhuriwa na Balozi wa China nchini Tanzania Dkt. Lu Youqing, Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba.
VIEW BBC

No comments