Header Ads

Mlinzi wa Kampuni ya Ulinzi Ajinyonga Baada ya Kugundulika ana Maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI

 
Mlinzi wa Kampuni ya Ulinzi ya Imara, Samwel Arcado (39) amejinyonga ndani ya chumba chake kwa madai ya kugundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU). 


Mlinzi huyo ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Mji wa Zamani, Manispaa ya Mpanda alikutwa amejinyonga kwa kutumia shati. 


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda alisema jana kuwa uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea. 


Mwenyekiti wa mtaa huo, Margaret John alisema tukio hilo lilitokea jana saa kumi na moja alfajiri ndani ya chumba alichokuwa akiishi Arcado. 


Alisema Samwel alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya mara kwa mara, hali iliyosababisha kwenda hospitali kufanyiwa uchunguzi wa afya yake, ambako aligundulika kuwa na VVU. 


John alisema baada ya kupatiwa majibu hayo alichanganyikiwa, hali iliyosababisha utendaji wake wa kazi kuzorota. 


Alisema kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi, mwajiri wake alitaka kumrejesha nyumbani kwao mjini Sumbawanga mkoani Rukwa. 


Hata hivyo, taarifa zinadai kuwa siku ya safari ilipofika, mmoja wa wafanyakazi wenzake alifika kwenye nyumba aliyokuwa amepanga kwa lengo la kumwamsha ili ajiandae, lakini alipomgongea mlango hakujibiwa hali iliyompa shaka na kuwaamsha wapangaji wengine. 


Mwenyekiti huyo alisema mfanyakazi huyo na wapangaji wenzake, walitoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya mtaa na ulipofika uliamuru mlango uvujwe na kukuta amejinyonga. Alisema walitoa taarifa polisi ambao walifika na kuchukua mwili.

No comments