Header Ads

Hofu yatanda Arusha nchini Tanzania kufuatia visa vingi vya mauaji ya wanawake



Arusha

Sintofahamu ya kiusalama bado imetanda katika mji wa Mto wa Mbu, wilaya ya Monduli mkoani Arusha kufuatia mfululizo wa vitendo vya unyanyasaji wa kimwili na kingono dhidi ya wanawake na baadae kuuawa kwa wanawake hao.
Hadi hivi sasa wanawake wanane wameripotiwa kuuawa huku wengine kadhaa wakiwa wamefanyiwa vitendo vya kiudhalilishaji.
Tukio la mwisho limetokea katikati ya mwezi wa saba ambapo muathirika aitwaye Ruth Elias alikutwa ametupwa darajani, pembezoni mwa barabara kuu.
Uchunguzi wa kitabibu ulionyesha kwamba, kama ilivyokuwa kwa wanawake wengine, yeye pia alijeruhiwa na kufanyiwa vitendo vya kidhalilishaji.
"Majeraha yanafanana, na yanafanana kwa sehemu moja ya kuingiliwa. Lakini haya mengine ndio yanatofautiana kwasababu mwingine inawezakana alipata majeraha kichwani, mwingine shingoni ambayo ndiyo yanayopelekea vifo vyao. Lakini jambo linalotuonyesha kuwa hivi visa vinafanana ni kwasababu walikuwa wameingiliwa kimwili." alisema Dr Emma Msofe, Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Makao Mapya
Ruth aliuwawa siku chache kabla binti yake Sarah kujifungua. Sarah aliiambia BBC namna gani ambavyo kuuwawa kwa mama yake kumemuathiri

Kwakweli huu msiba wa mama umeniumiza sana hadi hivi sasa sielewi yaani, nachanganyikiwa kwakweli. Yaani ni mtu ambaye nilikuwa namtegemea sana, ni mtu muhimu sana katika maisha yangu. Hadi sasa hivi siamini bado kwamba amekufa" alisema Sarah
Viongozi wa Mto wa Mbu na vyombo vya usalama wanasema wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na mauaji haya. Hata hivyo polisi wanasema wanaamini mauaji haya ni uhalifu tu na si visa vinavyowalenga wanawake. Hata hivyo walidai wameongeza juhudi za ulinzi kukabiliana na vitendo hivi.
"Tulichofanya ni kwamba tumekusanya vikundi vya ulinzi shirikishi lakini pia tulizungumza na wananchi ili kuwapa hamasa pia washirikiane na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu wenyewe. Na bahati nzuri walitupa taarifa na hadi sasa hivi tunawashikiria watu tisa kuhusiana na tukio hilo la mauwaji" Ramadhani Ng'anzi, Kamanda wa Polisi Arusha.

No comments