Kepa Arrizabalaga: Chelsea wamnunua kipa wa Athletic Bilbao
helsea wamevunja rekodi ya dunia katika ununuzi wa mlinda lango kwa kumnunua kipa Kepa Arrizabalaga kutoka klabu ya Athletic Bilbao ya Uhispania kwa £71m.
Mlinda lango huyo mwenye miaka 23 amenunuliwa kujaza nafasi ya Thibaut Courtois ambaye anakaribia kukamilisha uhamisho wake kutoka Stamford Bridge kwenda Real Madrid ya Uhispania.
Ada hiyo imezidi £66.8m ambazo Liverpool walilipa mwezi Julai kumchukua kipa wa Brazil Alisson.
Courtois, ambaye huchezea timu ya taifa ya Ubelgiji, alikosa kurejea mazoezini Jumattau huku tetesi zikimhusisha na kuhamia Real Madrid. Mchezaji huyo mwenye miaka 26 alikuwa ametarajiwa kujiunga na wenzake kwa mazoezi ya kuanza msimu Jumatatu lakini hakufika.
Jumatano, Chelsea walitoa taarifa kueleza kuwa wameafikiana na Real Madrid kuhusu uhamisho wa Mbelgiji huyo.
Kepa ni kipa nambari mbili katika timu ya taifa ya Uhispania, akiwa nyuma ya kipa wa Manchester United David de Gea, na amechezea timu ya taifa mechi moja pekee.
Alikuwa amekaa misimu miwili katika kikosi cha kwanza cha Bilbao na kuwalindia lango katika mechi 53 La Liga.
Chelsea wamevunja rekodi yao ya ununuzi wa mchezaji, kwani uhamisho wake umegharimu zaidi ya £60m walizolipa kumnunua mshambuliaji Mhispania Alvaro Morata kutoka Real Madrid Julai mwaka 2017.
"Kuna mambo mengi sana ambayo yamenivutia katika klabu hii - mataji ambayo wameshinda, wachezaji walio katika klabu hii, jiji lenyewe, na Ligi Kuu ya England," amesema Kepa.
"Ni mambo mengi tu, na nina furaha kwamba Chelsea wameamua kuwa na imani nami na kunipokea.
Post a Comment