Israel yafanya mashambulizi makali Gaza
Israel imefanya mashambulizi makali kulipiza kisasi katika Ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia leo baada ya makombora 150 kurushwa katika eneo lake. Maafisa wamesema watu watatu wameuawa akiwemo mtoto mdogo katika mashambulizi hayo makali.
Makombora kadhaa yaliyofyatuliwa na wanamgambo wa Kipalestina, yalianguka katika maeneo yaliyo wazi, lakini mbili yalishambulia mji wa Israel uitwao Sderot ulioko karibu na ukanda wa Gaza.
Wahudumu wa afya waliripoti kuwa watu wasiopungua wanne walijeruhiwa na kupelekwa katika hospitali za Israel, akiwemo mwanamke wa Thailand mwenye umri wa miaka 30, ambaye hali yake ya majeraha imeelezwa kuwa kati ya wastani mbaya sana. Meya wa mji wa Sderot Alon Davidi amesema wamekuwa na usiku mgumu sana. "Haujawa usiku mzuri kwa watu wa Sderot. Mamia ya watoto na vijana mahali hapa. Sio Hali ya kupendeza. Kando na kuwa meya, mimi ni mzazi na ninaweza kuhisi kile wanahisi, ninaweza kuwasikia wanangu, ulikuwa usiku mgumu."
Kulingana na maafisa wa afya katika uzio wa Gaza unaodhibitiwa na kundi la Hamas, waliouawa katika Ukanda huo ni pamoja na mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka 23 na bintiye mwenye umri wa miezi 18.
Wizara ya afya imesema waliuawa kutokana na mashambulizi makali yaliyofanywa kwa ndege katika eneo la kati la Gaza-Jafarawi. Na kwamba mume wa marehemu alijeruhiwa.
Kwa mujibu wa wizara ya afya, mpiganaji mmoja wa kundi la Hamas pia aliuawa na wengine 12 walijeruhiwa.
Hii ilikuwa mara ya tatu kwa machafuko kuzuka ghafla tangu Julai, na yalijiri licha ya juhudi za Umoja wa Mataifa na Misri kutafuta suluhisho la kudumu la usitishaji machafuko kati ya Israel na Hamas.
Nickolay Mladenov ambaye ni mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Mashariki ya Kati na ambaye amekuwa akijaribu kutafuta suluhisho la kudumu kati ya israel na Hamas amesema amesikitishwa sana na ametaka pande zote kuacha vita.
Kuzuka mara tatu kwa ghasia hizo, ambazo zimejiri baada ya miezi kadhaa ya vurugu na machafuko katika mpaka wa Gaza, kumeibua hofu ya kuzuka kwa vita vya nne kati ya pande hizo mbili tangu mwaka 2008.
Jeshi la Israel limesema lililenga zaidi ya maeneo 140 ya kijeshi ya Hamas, ikiwemo kambi ya kijeshi na maeneo ambako vuguvugu hilo la Kiislamu hutengenezea silaha.
Israel imesema ililengwa kwa roketi 150 ambazo zilifyatuliwa kwanzia Jumatano hadi kuingia Alhamisi, na kwamba 20 kati yazo zilizuiliwa na mfumo wa ulinzi wa angani. Hayo ni kulingana na jeshi la Israel.
CHANZO DW SWAHILI
kIAPO CHA MKUU WA WILAYA YA UYUI MKOA WA TABORA
Post a Comment