Header Ads

WANANCHI WASHINIKIZA WAELEZWE HATMA YAO

Picha

WAKAZI wa Kijiji cha Buigiri, Wilaya ya Chamwino, Dodoma, wametishia kujisaidia vichakani na mifuko ya Rambo kama serikali haitawapimia maeneo ya makazi wanayoishi.
Wametoa tishio hilo kwa Diwani wa Kata ya Buigiri, Kenneth Yindi (CCM) alipokuwa akizungumza nao kuhusu matatizo yao huko.
Walisema halmashauri hao imekuwa ikiwataka wajenge vyoo bora vya kisasa wakati hawana makazi ya uhakika ya kuishi kutokana na kuzuiwa na serikali kuendeleza ujenzi wao.
Athanasi Yohana mmoja wa waathirika na amri hiyo alisema, ameshangazwa na utaratibu huo wa kujenga choo cha kisasa lakini si makazi.
Amesema pamoja na kukubali kwamba vyoo ni muhimu, hawawezi kujenga choo kizuri cha kisasa wakati hafahamu kama ataendelea kuwepo kwenye eneo analoishi kwa sasa.
"Heri kujisaidia katika mifuko ya rambo au vichakani. Hii ya kuingia gharama eneo ambalo hujui kama utaishi au la si sawasawa," alisema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chikuyu 'A' Emmanuel Masima alisema, ujenzi wa vyoo bado ni kitendawili katika kijiji hicho huku akihoji inakuwaje wazuiwe kujenga nyumba lakini suala la vyoo likisisitizwa zaidi kwao.
"Tunafahamu Dodoma ndiko walikohamishiwa wafanyakazi hivyo ardhi imekuwa dili, hatuna raha watu wanazunguka kuangalia maeneo yetu na Serikali haitaki tuendelee na ujenzi. Kwa nini tunateseka, watueleze hatma yetu," alisema.
Matheo Mazengo alisema, kutokana na Serikali kuagiza vijengwe vyoo vizuri na vya uhakika, hawaoni sababu kufanya hivyo kwani wakijenga hawatalala kwenye vyoo hivyo vya kisasa.
Diwani Yindi aliwataka wananchi kutulia kwa kuwa Jumatano ijayo atafika na wataalamu watakaosema lini wataanza kuwapimia maeneo.
"Tutakuwa na mkutano mkubwa wa hadhara na wataalamu watasema lini wataanza kupima maeneo yenu. Msiwe na wasiwasi ndio maana nimezuru vitongoji kujua shida zenu,"alisema.
Yindi alikagua machinjio ya kijiji na kusema hajaridhishwa na hali ya usafi aliyoikuta hivyo kuagiza Ofisa Mtendaji wa Kijiji kuhakikisha machinjio yanakuwa safi katika wiki mbili.
Pia alikagua mradi wa maji kwa watu wasioona wa kijiji cha Buigiri waliopewa Sh milioni 150 zilitolewa na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, lakini hadi leo mradi huo hautoi maji.

No comments