ZAIDI ya Sh milioni 800 zinatarajiwa kukusanywa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) kwa ajili ya kusaidia waathirika wa Virus
ZAIDI ya Sh milioni 800 zinatarajiwa kukusanywa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) kwa ajili ya kusaidia waathirika wa Virusi Vya Ukimwi mwaka huu.
Fedha hizo zitakusanywa kupitia kampeni maalumu ya kupanda mlima Kilimanjaro ijulikanayo kama Kill Challenge inayofanyika kwa mwaka wa 15, ambayo kwa mwaka huu wapanda mlima 100 wamejitokeza kushiriki.
“Mgodi wa Geita kwa kushirikiana na Tacaids unatarajia kupandisha watu 50 katika kilele cha mlima Kilimanjaro na kundi lingine la waendesha baiskeli 50 linataraji kuzunguka mlima huo kwa ajili ya kukusanya fedha hizo,” alisema Meneja Mawasiliano wa Mgodi wa GGM, Tenga Tenga.
Tenga alisema kampeni hiyo ya Kili Challenge inaongozwa na Balozi wake, Mrisho Mpoto ambaye ni msanii wa kughani mashairi na upandaji huo wa mlima utafanyika Julai 16 na kumalizika Julai 22, mwaka huu.
Alisema mgeni rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, ambaye ataanzisha safari hiyo huku mapokezi ya kuwapokea wapandaji hao akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecky Sadiki.
Naye Mwakilishi wa Tacaids, Jackson Peter, alisema Kili Challenge ya mwaka huu imepata uzito wa kipekee kutokana na Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika lake la Maendeleo la (UNDP) kutoa wawakilishi wanane kushiriki upandaji mlima huo kwa ajili ya kusaidia watu walioathirika na Virusi Vya Ukimwi nchini.
Balozi wa Kili Challenge, Mpoto aliwataka wananchi na jamii kwa ujumla kutambua mapambano dhidi ya Ukimwi ni ya jamii yote hivyo inapaswa kuunga mkono jitihada za serikali kwa ajili ya kupambana ili kufikia sifuri tatu.
“Naamini kwamba jitihada zinazofanywa na mfuko huu zinahitaji kuungwa mkono na Watanzania wote na wadau wenye machungu na nchi hii, hivyo tuungane kila mmoja wetu ama kwa kuxchangia au kumuelisha mwenzake ili mapambano haya yalete mabadiliko,” alisema Mpoto.
Tangu kuanza kwa kampeni hiyo miaka 15 iliyopita zaidi ya Dola za Marekani 8,000 zimekusanywa na kugawiwa katika asasi mbalimbali nchini zinazoshiriki katika mapambano na kusaidia waathirika wa Ukimwi.
Fedha hizo zimepelekwa katika kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi, ikiwamo kujenga vituo vya ushauri na upimaji wa Ukimwi, ambavyo baadhi yao ni vile vilivyopo mkoani Tanga, Manyoni mkoani Singida na Geita.
Post a Comment