Kocha wa yanga aomba kazi Singida United
Baada ya hivi karibuni kuongea na East Africa Television na kuthibitisha kuwa wanaachana na kocha wao Hans Van Pluijm, Mkurugenzi wa Singida United Festo Sanga, leo ameweka wazi kuwa wamepokea maombi ya kocha wa zamani wa Yanga Dusen Kondic.
Sanga amesema bado wanapitia wasifu wa makocha mbalimbali kutoka maeneo tofauti ambao wameomba kuchukua mikoba ya Hans ambaye anaondoka klabuni hapo baada ya mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mtibwa Sugar Juni 2.
''Mpaka sasa hatuna uhakika wa nani atachukua nafasi ya Hans, lakini tutatangaza hivi karibuni baada ya watalaam wetu wa masuala ya ufundi kumaliza kazi ya kupitia majina yaliyoomba kazi, akiwemo kocha wa zamani wa Yanga Mserbia Dusen Kondic pamoja na wengine wa nje na hapa kwetu'', amesema.
Dusen Kondic alijiunga na Yanga November 2007, akichukua mikoba ya Mserbia mwenzake Sredejovic 'Micho' Milutin. Hata hivyo hakudumu ndani ya klabu hiyo kwani alifutwa kazi mwishoni mwa msimu wa 2007/08.
Singida United ambayo imerejea ligi kuu msimu huu, imeonesha ushindani mkubwa ambapo hadi sasa ipo katika nafasi ya 5, ikiwa imesalia mechi moja kumalizika kwa msimu. Timu hiyo pia inaweza kupata nafasi ya kuwakilisha nchi endapo itaifunga Mtibwa Sugar kwenye fainali ya FA Juni 2.
Post a Comment