Header Ads

Mikakati elimu yaongezewa




Mikakati ya elimu yaongezewa bajeti Na Magnus Mahenge, Dodoma KATIKA kuhakikisha sekta ya elimu kuanzia ya awali hadi elimu ya juu inapata mafanikio ya haraka, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeongeza bajeti yake kwa asilimia tano kutoka Sh trilioni 1.34 za mwaka 2017/18 hadi Sh trilioni 1.41 za mwaka huu wa fedha 2018/19.
Hayo yalibainika jana jijini Dodoma wakati Waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Profesa Joyce Ndalichako aliposoma makadirio ya bajeti ya wizara yake.
Aliliomba Bunge liridhie na kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya Sh trilioni 1.41 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Wizara hiyo inaomba Bunge liidhinishe fedha hizo kwa malengo mbalimbali yakiwemo ya kuboresha elimu tangu awali hadi elimu ya juu, miundombinu ya shule zote, rasilimali watu pamoja na kutoa mafunzo ndani na nje ya nchi.
Alisema katika kuboresha elimu wizara yake, inakusudia kudahili wanachuo 8,152 ya vyuo mbalimbali vya elimu ya ualimu, wakiwemo 2,470 wa ngazi ya Astashahada na 5,682 wa ngazi ya stashahada.
Alisema, kati ya walimu wa stahashada wapo walimu 2,863 wa masomo ya sayansi, elimu maalumu (395), wa elimu ya awali (163), masomo ya fani (124), michezo (315), elimu ya msingi (762) na stahashada ya sayansi jamii (2,014).
Katika kuimarisha mafunzo ya vitendo, wizara itatoa mafunzo kwa wanachuo 20,535 wa vyuo vya ualimu wa mwaka wa kwanza hadi wa tatu ili kuainisha na kuwianisha nadharia na vitendo.
"Pia itatoa mafunzo kabilishi kwa wanafunzi wasichana 200 wa kidato cha sita wa masomo ya sayansi na hisabati wenye sifa pungufu kwenye masomo hayo ya kufundishia ili wapate sifa stahili za kusomea stashahada ya ualimu za masomo hayo.Wizara pia imeweka malengo ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Elimu (EP4R) ambapo imetenga Sh bilioni 140.0 kwa ajili ya kutoa motisha kwa halmashauri zote zinazotekeleza mpango huo. Programu hiyo inalenga kujenga madarasa 2,000 na matundu ya vyoo 2,000 kwa shule za msingi na sekondari, kujenga mabwalo katika shule 85 zilizopanuliwa kwa ajili ya kuhadili wanafunzi wa kidato cha tano.
"Kununua vifaa vya maabara awamu ya pili kwa shule 1,800 za sekondari za wananchi," alisema Prof Ndalichako.
Pia inakusudia kukarabati shule kongwe 25 za sekondari, kukarabati na kupanua vyuo 8 vya ualimu vya Bustani, Vikindu, Mtwara Kawaida, Mtwara Ufundi, Singachini, Monduli, Bunda na Katoke na kununua magari 20 kwa ajili ya vyuo vya ualimu.
Katika mradi wa Programu ya Maendeleo ya ELimu ya Msingi (MMEM) wa kuimarisha mafunzo ya stadi za kusoma, kuandioka na kuhesabu (KKK), serikali imetenga Sh bilioni 4.0 kufanya tathmini ya ufuatiliaji wa mikakati ya sekta ya elimu nchini.







Katika kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na elimu ya ualimu, wizara imetenga Sh bilioni 24 ili kukamilisha ujenzi wa chuo cha ufundi stadi mkoa wa Njombe na kuanza ujenzi katika mikoa ya Simiyu, Geita na Rukwa.
Waziri Ndalichako alisema, wizara pia imetenga Sh bilioni 5.45 kwa ajili ya kuanza ujenzi katika vyuo vya ualimu sita vya Dakawa, Mpwapwa, Kleruu, Marangu, Tabora na Butimba.
Pia imepanga kuanza ujenzi wa chuo cha ufundi stadi katika mkoa wa Kagera chini ya ufadhili wa Serikali ya China, ambapo Sh bilioni 14.99 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo. Alisema pia serikali imetenga Sh bilioni 12.4 kwa ajili ya mradi wa ukarabati wa vyuo vya ualimu vya shinyanga, Mpuguso, Ndala na Kitangili.
Alisema katika kuendeleza elimu ya ualimu imetenga sh bilioni 20.24 kwa ajili ya kununua vifaa vya kufundishia na kijifunzia katika vyuo 35 vya ualimu na vifaa vya elimu maalumu kwa vyuo vya Patandi, Mtwara Ufundi na Mpwapwa.
"Serikali imeamua kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari kutenga Sh bilioni 21 kwa lengo la kwa kujenga shule mpya katika makao makuu ya saba," alisema.
"Pia imetenga Sh bilioni 2.8 kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu nane kwa kila shule katika shule mpya saba za mikoa ya Geita, Njombe, Lindi, Singida, Katavi, Ruvuma na Manyara," alisema Prof Ndalichako.
Pia ilisema imepanga kununua samani na vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika shule mpya saba ambazo jumla ya Sh bilioni 7.0 zimetengwa.
Profesa Ndalichako alisema katika mwaka 2018/19, wizara inaendelea kuviimarisha vyuo vya maendeleo ya wananchi kwa kujenga na kukabarati miundombinu katika vyuo 20 vya maendeleo ya wananchi nchini.
Kupitia mradi wa kukuza stadi za kazi kwa ajili ya shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi, Profesa Ndalichako alisema, wizara itatoa ruzuku kwa ushindani kwa vyuo vya ufundi nchini ili vijana 7,00 wasio na uwezo wa kujiendeleza ili wapate mafunzo.
Pia itasimamia ithibati na uthibiti wa ubora wa shule na vyuo vya ualimu kwa kukagua asasi 11,327 zikiwemo shule za msingi 8,785 na za sekondari 2,480 na vyuo vya ualimu 62.
Katika kusimamia elimu ya msingi na sekondari, wizara itagharamia chakula kwa wanachuo 20,236 na mafunzo kwa vitendo kwa wanachuo 12,782 katika vyuo vya serikali 35 vya ualimu.
Katika mwaka huu, Baraza la Mitihani Taifa limepanga kuendesha upimaji wa kitaifa wa darasa la nne kwa watahiniwa 1,609,247, kuendesha mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi wanafunzi 965,255 na upimaji wa kitaifa kidato cha pili watahiniwa 547,846.
Pia itashughulikia upimaji wa mtihani wa kidato cha nne watahiniwa 440,382, kuendesha mitihani ya kidato cha sita kwa watahiniwa 80,628 na mitihani ya cheti na stashahada ya ualimu 12,500.
Mamlaka ya Elimu Tanzania imetenga Sh bilioni 9.75 ili kuwezesha ujenzi wa nyumba 15 za walimu katika shule za sekondari na ujenzi wa madarasa 300 kwenye shule za msingi 60 zenye uhitaji mkubwa.

No comments