Header Ads

kuhakikisha wanafuatilia bei ya sukari


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

WAKUU wa mikoa, wilaya na maofisa biashara katika ngazi zote wametakiwa kuhakikisha wanafuatilia bei ya sukari na kuona kwamba bei iliyopo haiwaumizi wananchi.
Aidha sukari iliyoagizwa nchi za nje kwa ajili ya kukabiliana na upungufu unaojitokeza kila mwaka imeshaanza kuingia. Pia serikali imesema inalitafutia ufumbuzi tatizo la kukwama kwa meli za mafuta ya kula katika Bandari ya Dar es Salaam linaloambatana na mgongano wa taarifa na maamuzi. Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo Bungeni jana. Maelekezo hayo ya Waziri Mkuu yalitokana na maswali ya wabunge mbalimbali waliopata nafasi ya kuuliza maswali ya papo kwa hapo.
Kupanda kwa bei ya sukari Mbunge wa kuteuliwa Abdallah Bulembo (CCM) alitaka kujua hatua zinachukuliwa na serikali kukabiliana na kupaa kwa bei ya sukari huku mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ukiwa karibu. Alisema kwamba bei ya sasa imepanda kufikia Sh 2,800 na kwingine Sh 3,300 na kutishia waumini wa dini ya Kiislamu wanaotarajia kufunga siku saba zijazo;kwa kuwa sukari ni kiungo muhimu wakati wa mfungo wa Ramadhani. Waziri Mkuu alisema kwamba serikali inatambua kuwa kila mwaka kuna pengo linalohitaji kufidiwa na kwamba vibali vimeshatolewa na sukari imeanza kuingia na hivyo kuwaagiza watendaji kusimamia bei ya sukari ili wananchi wasiumizwe.
Pamoja na kutoa maagizo hayo, Waziri Mkuu aliwatoa hofu Watanzania juu ya shaka ya kupandishwa kwa bei ya vyakula kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Akisisitiza aliwataka maofisa biashara, wakuu wa wilaya na mikoa yote nchini kusimamia na kuhakikisha wafanyabiashara hawapandishi bei ya bidhaa zozote, kwani kufanya hivyo ni kuwapa adha waumini wa madhehebu ya Kiislamu na wananchi wengine. Alisema kama taifa serikali imelipatia ufumbuzi suala la sukari, ambapo imelenga upatikanaji wa bidhaa yenyewe iwe ya kutosha na kila mwenye mahitaji ya matumizi aweze kuipata kwa urahisi katika maeneo yote nchini. Alisema nia ya kutoa vibali vya kuingiza sukari ya kutoka nje ya nchi ni kulifanya soko la sukari kuendelea kuwepo katika unafuu wake.
Aliiagiza Bodi ya Sukari kupitia Wizara ya Kilimo kuendelea kufuatilia mwenendo wa uingizwaji wa sukari nchini ili iweze kusambazwa hadi kwenye vijiji na huduma hiyo ipatikane maeneo yote. Aidha alisema kwamba Serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa bei ya sukari katika maduka yote ili kuwabaini wanaopandisha bei kwa makusudi na kuwachukulia hatua. Mahitaji ya sukari nchini ni tani 450, 000 lakini uwezo wa kuzalisha wa viwanda vyote kwa jumla ni tani 320,000 na hivyo kusababisha upungufu wa tani 130,000.
Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa mkoani Morogoro kina uwezo wa kuzalisha tani 30,000, Kiwanda cha Sukari cha TPC mkoani Kilimanjaro tani 100,000, Kiwanda cha Sukari cha Kilombero mkoani Morogoro tani 109,000, Kiwanda cha Sukari mkoani Manyara tani 6,000, Kiwanda cha sukari cha Kagera tani 65,000 hadi tani 67,000. Aidha mwaka jana serikali ilitoa bei elekezi ya sukari ambapo ilisema haipaswi kuvuka Sh 2,000 mbili katika maeneo mbalimbali nchini. Sakata la mafuta ya kula bandarini Akijibu swali la Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) kuhusu mafuta ghafi ya kula na kupanda kwa bei ya mafuta hayo sokoni kwa asilimia 15 na 30, Waziri Mkuu Majaliwa alikiri kuwapo kwa tatizo la uingizwaji wa mafuta ya kula nchini.
Alisema kwamba wapo baadhi ya wafanyabiashara wachache wasio waaminifu wamekuwa wakifanya udanganyifu na kusababisha mgongano wa kimamlaka. Alisema ili kulinda viwanda vya ndani serikali iliweka kodi kwa mafuta ghafi na mafuta safi na kwamba wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiingiza mafuta safi na kudanganya ni ghafi hali ambayo imesababisha sintofahamu ambayo serikali sasa inaifuatilia.
Alisema mkanganyiko unaofanywa na TRA kutotambua Mkemia Mkuu wa Serikali na maelezo yake yamesababisha meli mbili za mafuta kubaki bandarini huku bei ya mafuta ikiwa inaendelea kupanda sokoni. Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema ni utaratibu uliopangwa wa mfumo wa kodi kwa ajili ya kulinda viwanda vya ndani ambapo pia Bunge liliridhia tozo ya asilimia 10 kwa mafuta ghafi na yale yaliyosafishwa kidogo asilimia 25.
“Ni utaratibu wa kufuatilia mwenendo wa uingizaji wa mafuta hapa nchini, baadhi ya wafanyabiashara wasio waamini wamekuwa wakiingiza mafuta safi na kusema ni ghafi, kila aina ya mafuta hayo yana kodi yake,” alisema Waziri Mkuu. Hata hivyo, alisema ameunda timu ya kufuatilia suala hilo, ili kutatua tatizo lililopo sasa kuona litatuliwaje, ikiwa ni kujua ukweli kuhusu madai ya TRA kuhusu mafuta hayo. Katika majibu yake pia alisema Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watakutana Jumamosi ijayo mjini Arusha kuweka msimamo wa pamoja kuhusiana na tozo za kodi katika sekta hiyo.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Suleiman Murad, ambaye pia ni Mbunge wa Mvomero (CCM) aliitaka serikali kuingilia kati utata wa kodi inayopaswa kulipa kwenye meli mbili za mafuta zilizotia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuepusha upandaji bei wa mafuta ya kula na bidhaa zingine zitokanazo na mafuta ghafi.
Mwenyekiti huyo alisema hayo wakati wa semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo wabunge kuhusu utendaji kazi na majukumu ya taasisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Tume ya Ushindani (FCC) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela). Murad alisema kumetokea tofauti kati ya utambuzi wa mzigo uliobebwa na meli mbili za mafuta ambazo zimekaa bandarini kwa zaidi ya wiki mbili sasa.
Meli moja ikiwa na tani 30 za mafuta na meli nyingine tani 31 za mafuta. “Kuna meli mbili bandarini kwa wiki mbili sasa zimeleta mafuta. TBS wametoa cheti cha kuwa mafuta yale ni crude oil (mafuta ghafi), Mkemia Mkuu wa Serikali amesema crude oil, lakini TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wamekataa na kusema ni semi-refined (yaliyosafishwa kidogo).
Murad aliongeza: “Hivi sasa mafuta ya kula yameanza kupanda bei, kwa sababu watu wa viwanda wameanza kutumia mafuta yaliyopo nchini hivyo kuishiwa na malighafi. Naibu Waziri (Stella Manyanya) upo naomba ulichukue na kulishughulikia.” Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ambayo kutokana na tatizo hilo walipaswa kuketi jana kulijadili, sasa kwa mujibu wa Spika wa Bunge Job Ndugai halitaketi tena na badala yake wanasubiri serikali kutoa majibu ya ufuatiliaji.

No comments