Header Ads

Spika atamani Bunge EAC litumie Kiswahili



SPIKA wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dk Martin Ngoga amesema kama kuna kitu anachotamani kifanikiwe kabla ya kumalizika kwa muda wake wa kukaa madarakani, basi ni kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa rasmi kwa matumizi ya bunge analoliongoza.
Amesema lugha ya Kiswahili inayotumika katika mataifa yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), itawaunganisha zaidi wananchi zaidi ya milioni 150 wa Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini kuliko Kiingereza, ambayo ni lugha rasmi ndani ya bunge hilo.
Alisema hayo hivi karibuni wakati wa mahojiano maalumu mjini Dodoma, ambapo alisisitiza kuwa, kwa nafasi aliyonayo, ataendelea kujenga ushawishi kwa wakuu wa nchi ndani ya jumuiya waweze kurekebisha kifungu kinachohusu lugha rasmi za jumuiya.
“Namuomba Mungu kabla sijamaliza muda wangu wa uongozi katika nafasi hii ya Uspika, niwe nimeshatimiza kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi pia ya Bunge la Afrika Mashariki,” alisema Dk Ngoga, mwanasheria nguli raia wa Rwanda.
Alisema katika bunge la tatu lililopita, EALA walipitisha azimio la kuwaomba viongozi wa nchi za EAC, warekebishe mkataba wa kifungu kinachohusu lugha rasmi za jumuiya.
“Ombi letu kama bunge lilihusu lugha ya Kiswahili iwe mojawapo ya lugha rasmi za jumuiya ya Afrika Mashariki. Hili halijatimizwa, lakini tutaendelea kuomba. Hatufurahishwi kuona kwamba lugha ambayo inazungumzwa na watu wengi katika jumuiya yetu haijawa rasmi katika matumizi yetu ya kila siku.
“Nchi zetu karibu zote wanazungumza Kiswahili, hivyo hatuoni fahari kwamba tunapokutana kama Jumuiya ya Afrika Mashariki tunaongea Kiingereza. Hilo sio jambo la fahari hata kidogo. Tunatakiwa tuongee lugha mojawapo ya lugha zetu na hii lugha ya Kiswahili ni kubwa na tayari katika Umoja wa Afrika inatumika sasa. Kama tumefanikiwa lugha hiyo kutumika na Umoja wa Afrika kwa nini isitumike hapa ilipoanzia na ndiyo nyumbani kwake,” alisema.
Kauli ya EAC
Mapema mwaka huu, Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko alielezea mikakati ya jumuiya hiyo kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi. Naibu Waziri Mkuu wa Pili wa Uganda anayeshughulikia masuala ya EAC, Kirunda Ali Kivejinja pia amekuwa akisisitiza umuhimu wa wananchi kwenye nchi wanachama kukitumia Kiswahili kuwaunganisha.
Kiongozi huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri EAC, alisema, nchi wanachama wa EAC hazitafanikiwa kutekeleza kifungu cha 137 (2) cha makubaliano ya kuanzishwa jumuiya hiyo kama hazitakitumia Kiswahili kuwaunganisha.
Aliyasema hayo akiwa Zanzibar mwishoni mwa mwaka jana wakati wa hafla ya kufungwa kwa Mkutano wa kwanza wa Kimataifa, ulioandaliwa na Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (EAKC).
Alisema ni muhimu kwa Kiswahili kifanywe rahisi na sehemu kubwa ya watu kwenye eneo la EAC, waitumie lugha hiyo sanjari na lugha zao za asili zikiwemo za zaidi ya makabila 120 nchini Tanzania.
Aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa licha ya kuwepo kwa idadi hiyo ya makabila, Kiswahili kilitumika kuwaunganisha.
Alitoa pendekezo kwa EAKC kutoa mapendekezo kwamba Kiswahili kitumike vipi ili kufanikiwa katika utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs).
Katibu Mtendaji wa EAKC, Profesa Kenneth Simala alisema kwenye mkutano huo kuwa, tume hiyo inafanya kazi kwa karibu na vyama vya Kiswahili kwenye nchi wanachama ili viwe na umoja.
Kwa mujibu wa Profesa Simala, mambo kadhaa yanatekelezwa ili kukiwezesha Kiswahili iwe lugha rasmi ya EAC.
Wajumbe wa mkutano huo walijadili, pamoja na mambo mengine namna Kiswahili kinavyoweza kutumika kuzidisha mtangamano EAC na kuchangia utekelezaji wa SDGs.
Walieleza umuhimu wa kuanzishwa haraka mabaraza ya Kiswahili na vyama vya lugha hiyo kwenye kila nchi, kutumia lugha hiyo kwenye ngazi mbalimbali za elimu, kuhamasisha tafiti za Kiswahili na nchi wanachama kuitumia lugha hiyo kwenye programu za elimu ya watu wazima.
Mkurugenzi wa Taasisi yaTaaluma za Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TATAKI), Dk Ernesta Mosha ilisema Kiswahili ni lugha muhimu ya mawasiliano kwa nchi za Afrika Mashariki, kwa kuwa inafundishwa katika viwango vya elimu, shughuli za kijamii, kisiasa na kiuchumi. Wahadhiri wa vyuo vikuu vya ndani na nje ya Afrika Mashariki wapo TATAKI kujifunza lugha hiyo ngazi ya shahada za juu.
Dk Mosha alisema kutumika kwa lugha hiyo kwa kiasi kikubwa kunaimarisha umoja na ushirikiano kwenye nchi wanachama EAC na pia inaendelea kuwa lugha ya ukanda huo.
Alisema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia taasisi hiyo, kina wanafunzi wanaosoma Shahada za Uzamili katika Kiswahili na pia Shahada za Uzamivu katika Kiswahili kutoka nchi wanachama EAC. “Kwa mfano katika mwaka wa masomo 2016/2017 tuna wanafunzi wa Uzamivu kutoka Kenya na Uganda.
Hawa ni walimu kutoka katika vyuo vikuu. Aidha, Taasisi ina wanafunzi ambao ni wafanyakazi wa vyuo vikuu vya Ghana na Zimbabwe ambao wanasoma Programu za Uzamili na Uzamivu.
“Lakini pia Taasisi ya Taaluma za Kiswahili kwa sasa ina walimu wanaofundisha Kiswahili Chuo Kikuu cha Zimbabwe na Chuo Kikuu cha Namibia,” alisema.

No comments