tetesi za michezo barani ulaya
Hamilton ashinda Azerbaijan Grand Prix
Katika mashindano ya magari ya Formula One, bingwa wa dunia wa timu ya Mercedes Lewis Hamilton alishinda mashindano ya ya Grand Prix ya Azerbaijan na kutwaa uongozi wa msiamamo wa ubingwa wa dunia
Muingereza huyo alitwaa ushindi baada ya tairi la dereva mwenzake wa Mercedes Valtteri Bottas kulipuka wakati akiwa uongozini wakati naye Sebastian Vettel akafunga breki wakati alipotaka kumpiku.
Dereva huyo wa Ferrari ambaye alianza mashindano ya jana akiwa katika nafasi ya kwanza alimaliza wa nne. ""ni mbio ambazo zilikuwa na hisia nyingi kusema kweli. Valtteri alifanya kazi nzuri sana leo na ndiye aliyestahili kushinda. Pia Sebastian Vettel alifanya kazi nzuri. Nadhani nilikuwa na bahari nzuri sana sana leo, na nahisi sio kawaida kuwa hapa jukwaani, lakini nauchukua ushindi huo. SIkukata tamaa, niliendelea kupambana lakini hazikuwa mbio nzuri kwangu"
Dereva wa Ferrari Kimi Raikkonen alipanda jukwaani katika nafasi ya pili mbele ya Sergio Perez wa timu ya Force India. Ushindi huo wa kwanza wa Hamilton msimu huu, baada ya Vettel kuibuka mshindi katika mikondo miwili ya kwanza na Daniel Ricciardo wa Red Bull kutamba nchini China wiki mbili zilizopita, unamuweka mbele ya Vettel na pengo la pointi nne.
Barcelona mabingwa wa Uhispania
Barcelona ilinyakua taji lao la 25 la ligi kuu ya kandanda Uhispania – La Liga baada ya kuifunga Deportivo La Coruna mabao manne kwa mawili wakati zikiwa zimesalia mechi nne msimu kukamilika
Lionel Messi alifunga hat trick na kufikisha mabao 32 ya ligi msimu huu na kuipa Barca taji lao la 7 la Laliga katika miaka 10. Ni kombe la pili la nyumbani kwa Barca ambao waliwazaba Sevilla 5-0 na kutwaa Kombe la Mfalme wiki iliyopita. Erneste Velverde ni kocha wa Barca "bila kujali mengine, tuna furaha sana kwa sababu tulikuwa na msimu mzuri sana. kwa sababu La Liga ndio kitu kinachokuambia wewe ni nani na ni wapi uliko kwa sababu sio kazi ya siku moja tu, bali kazi ya siku nyingi kutokana na mechi nyingi. Na unapaswa kucheza msimu wa baridi, mapukutiko na kisha mapuchiko ndio ufike mwisho na kusherehekea na watu wako.
Lakini wakati Barcelonsa walipiga muhuri wa muongo mmoja wa udhibiti wa kandanda la nyumbani, nao Real Madrid wanaendelea kutamba katika jukwaa la Ulaya.
Real Madrid kupambana na Bayern
Kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane amewataka mashabiki wa klabu hiyo kushangilia vilivyo dhidi ya Bayern Munich uwanjani Santiago Bernabeu hapo kesho, wakati timu hiyo ya Uhispania ikilenga kutinga fainali ya Champions League kwa mwaka wa tatu mfululizo. "sidhani kuwa wanatuogopa. watakuja hapa bila hofu yoyote. nikirudia nilichosema, nadhani tunapaswa kucheza vizuri saan. Nnawaomba mashabiki kutushangilia, tutawahitaji sana kuliko ilivyokuwa awali. Wanafahamu tunachokitaka na wamekuwa nyuma yetu muda wote. Nnawaomba mashabiki. tunawahitaji sana kuliko wakati mwingine wowote.
Real walishinda mabao mawili kwa moja uwanjani Allianz Arena wiki iliyopita. Msimu uliopita, mambo yalikuwa hivyo hivyo, kabla ya MADRID kuwabwaga Bayern katika muda wa ziada. Nyota wa Bayern Frank Ribery amesema vita bado havijamalizika.
Katika mtanange wa Jumatano, Roma watahitaji muujiza kama waliofanya dhidi ya Barcelona walipotoka nyuma mabao manne kwa moja na kuwaondoa katika robo fainali. Mara hii watajitaji kuwakabili vilivyo Liverpool ambao waliwapa kichapo cha mabao matano kwa mawili uwanjani Anfield katika mkondo wa kwanza. Kocha wa Roma Eusebio Di Francesco amesema lazima wajiamini kuwa na matumaini ya kuyageuza matokeo hayo. Mashabiki karibu 5,000 watakuwa mjini Rome na polisi ya Italia imeimarisha ulinzi baada ya shabiki wa Liverpool kujeruhiwa vibaya kabla ya mechi ya mkondo wa kwanza. Hakuna vinyaji vya pombe vitakavyouzwa karibu na uwanja wa Stadio Olimpico na katikati mwa mji.
Cologne yaiaga Bundesliga
Walikuwa wameshazikwa tayari, lakini msururu wa ghafla wa matokeo mazuri umewapa Hamburg matumaini ya kweli ya kuponyoka tena kaburi la kushushwa ngazi
Baada ya kushinda mechi mbili tu kuanzia mwishoni mwa Agosti hadi mapema Aprili, Hamburg wameshinda tatu kati ya mechi zao nne za mwisho na kuwaweka katika nafasi nzuri ya kuepuka kushushwa ngazi. Ushindi wao wa 3-1 Jumamosi unaweka pointi mbili nyuma ya wapinzani wao Wolfsburg ambao wanashikilia nafasi ya mechi ya mchujo ambayo walimaliza msimu uliopita.
Freiburg hatimaye waligonga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Cologne na kuwatimua katika Bundesliga baada ya ushindi wa 3-2. Lakini ushindi wa kushangaza wa wikiendi ulikuwa wa Mainz kuwapa RB Leipzig kipigo cha tatu bila hapo jana. Sandro Scwarz ni kocha wa Mainz "ulikuwa ushindi mkubwa na muhimu sana kwetu. Lakini licha ya kila kitu, bado hatujaponea mpaka sasa. jinsi tulivyocheza tulizidiwa nguvu katika kipindi cha pili. kulikuwa na mapambano katika kipindi cha kwanza na matukio ambayo bahati ilikuwa upande wetu. Ni mwanzoni tu ambapo tulipoteza mpira mara kadhaa. lakini uwanja ulikuwa wa kushangaza, mashabiki, kelele, mazingira na hisia. Na kisha tukapata matokeo yanayostahili".
Kileleni mwa msimamo wa ligi, Bayern Munich, iliyofanyiwa mabadiliko makubwa iliibumburusha Eintracht Frankfurt mabao manne kwa moja. Ni mchuano ulioonekana kuwa kionjo tu cha fainali ya kombe la Shirikisho la Ujerumani mnamo Mei 19 mjini Berlin kati ya timu hizo mbili.
Schalke walitoka sare ya 1-1 na Borussia Moenchegladbach na kuendelea kuyashikilia matumaini yao ya kucheza Champions League msimu ujao.
Lakini watamshukuru kipa wa Werder Bremen aliyefanya kazi kweli kweli langoni na kuhakikisha kuwa timu yake inatoka sare ya bao moja kwa moja na Dortmund. Hivyo BVB walioshindwa kuwapokonya Schalke nafasi ya pili.
Post a Comment