Header Ads

Kocha Simba SC Pierre Lechantre amebakiza takriban wiki sita kumaliza mkataba




WAKATI Simba ikiendelea kujiandaa vikali kwa ajili ya mchezo wake muhimu wa Jumapili hii dhidi ya Ndanda, Kocha mkuu wa timu hiyo, Pierre Lechantre amebakiza takriban wiki sita kumaliza mkataba wake klabuni hapo.
Hata hivyo kocha huyo alisema yupo tayari kuendelea kuinoa timu hiyo kama watafikia muafaka na mabosi wake.
Kocha huyo aliliambia gazeti hili kuwa anachoshukuru wakati anakaribia kumalizia mkataba wake huo wa muda mfupi aliokuwa nao, tayari amekaribia kumaliza kazi kubwa aliyopewa ya kuipa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
“Mkataba wangu ni wa miezi sita ndiyo maana siwezi kuzungumzia zaidi mambo ya msimu ujao kwa kuwa kazi yangu kubwa kwa sasa ndani ya mkataba wangu mfupi ni kuhakikisha naipa ubingwa Simba na baada ya hapo ndiyo tunaweza kukaa na uongozi kuzungumza kuhusu kinachofuata,” amesema kocha huyo ambaye hivi karibuni alikuwa miongoni mwa waliotuma maombi ya kuifundisha Cameroon.
“Ndiyo, nimepeleka maombi ya kuinoa tena Cameroon lakini hata kusalia Simba kwa misimu mingine ijayo ni kitu kizuri pia kwangu, ni sehemu nzuri pia ya kufanyia kazi na nimependa hata mwamko wake ulivyo kwa hiyo hayo yote kujua itakuwaje baada ya hapa, bado hatujakaa kuyajadili mpaka nitakapomaliza kazi ya kwanza niliyopewa,” amesema Lechantre.
Lechantre ambaye pia aliipa Cameroon ubingwa wa Afrika mwaka 2000 alijiunga na Simba mapema Januari, mwaka huu akichukua nafasi ya Mcameroon, Joseph Omog na kuendeleza gurudumu la ushindi na Simba kutokufungwa mpaka sasa ikiwa inaongoza msimamo wa ligi kwa pointi 62 baada ya mechi 26.
“Nashukuru nimekuwa na wakati mzuri hapa na nafikiri naweza kuendelea kuwepo kama kutakuwa na makubaliano mazuri kutoka kwa uongozi ingawa kikubwa kilichopo kichwani kwangu kwa sasa ni kuendelea kupigania kuipa ubingwa Simba,” alieleza Lechantre.
Mpaka sasa Simba imebakisha michezo minne, inahitaji pointi tano kutangaza ubingwa mapema kabla ya kumalizika kwa Ligi Kuu.
Ukiondoa mechi hiyo ya Ndanda, Wekundu hao wanatarajia kumaliza ngwe kwa kucheza dhidi ya Singida United Singida, kabla ya kurejea Dar es Salaam kuumana na Kagera Sugar kisha kufunga dimba ikiwa Ruvuma dhidi ya Majimaji.


No comments