Header Ads

BEI ya jumla na rejareja ya mahindi imeshuka


BEI ya jumla na rejareja ya mahindi katika Mji wa Sumbawanga uliopo katika mkoa wa Rukwa imeshuka kufuatia wafanyabiashara wa nafaka waliohodhi bidhaa hiyo kuanzia Julai mwaka jana kuamua kuyauza mapema mwaka huu.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika soko la nafaka la Mandela lililopo katika Kata ya Mazwi iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga umebaini kuwa gunia la mahindi lenye ujazo wa debe sita za mahindi sasa linauzwa kati ya Sh 75,000 na Sh 76,000 tofauti na bei ya awali ambapo yalikuwa yakiuzwa kati ya Sh 80,000 na 95,000.
Aidha bei ya rejareja ya dagaa daraja la kwanza maarufu kama kauzu imeendelea kushuka katika masoko ya mjini Sumbawanga mkoani humo ambao kwa muda mrefu walikuwa wakiuzwa kwa bei ya Sh 20,000 kwa kilo sasa wakiuza kati ya Sh 15,000 hadi Sh 17,000 kwa kilo.
Kuhusu mahindi, gazeti hili pia limebaini kuwa wafanyabiashara wa nafaka ‘walanguzi’ walianza kununua mahindi kutoka kwa wakulima kuanzia mwezi Julai hadi Septemba mwaka jana kwa bei ya ‘kutupa’ kati ya Sh 30,000 na 40,000 kwa gunia lenye ujazo wa debe sita za mahindi na kuyahifadhi wakisubiri kuyauza kwa bei nzuri.
“Si hapa nafaka hii (mahindi ) niliyanunua kwa bei ya Sh 40,000 kwa gunia lenye uzito wa debe sita kutoka kwa wakulima na sasa nauza gunia hilo kwa Sh 76,000 kwa bei ya jumla faida ipo kwani napata Sh 36,000 kwa kila gunia,” alisema mmoja wa wafanyabiashara kwa masharti ya kutotajwa jina lake.
Wakulima pia wanakiri kuwa wanalazimika kuwauzia walanguzi mahindi kwa bei ndogo ili kujikimu kimaisha, kwani kwao mahindi ni kila kituo kwa kuwa ni zao la chakula na biashara.
Mmiliki wa Mwilima, stoo iliyopo katika soko la nafaka la Mandela mjini Sumbawanga na mfanyabiashara wa nafaka, Okoka Mwinuka alisema kuwa bei ya jumla ya ulezi kwa gunia lenye uzito wa kilo 100 limeendelea kuuzwa kwa Sh 100,000 kwa muda mrefu .
“Bei ya rejareja ya gunia la mahindi lenye ujazo wa debe sita imeshuka kutoka kati ya Sh 90,000 hadi Sh 100,000 wakati bei ya ulezi haijapanda kwa muda mrefu sasa, bado tunauza gunia moja lenye uzito wa kilo 100 kwa bei ya jumla ya Sh 100,000,” alieleza Mwinuka.
Kuhusu bei ya kitoweo cha dagaa imeelezwa kuwa kilo ya dagaa daraja la kwanza imeshuka na kuuzwa Sh 17,000 kwa bei ya rejareja wakati dagaa daraja la pili sasa wanauzwa Sh 9,000 kwa kilo .
Awali dagaa daraja la kwanza walikuwa wakiuzwa kati ya Sh 20,000 na Sh 22,000 kwa kilo huku daraja la pili wakiuzwa Sh 13,0000 kwa kilo kwa bei ya rejareja baada ya kuadimika sokoni katika Mji wa Sumbawanga mkoani Rukwa .
Mfanyabiashara wa dagaa, Chrisant Makungu alisema kuwa kushuka kwa bei ya kitoweo hicho kunatokana na kufurika kwa bidhaa hiyo sokoni huku akisema kuwa wakazi wa mjini humo wamekuwa wakiichangamkia biashara hiyo kwa kununua bidhaa hiyo kwa wingi.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa mjini hapa walisema kuwa kitoweo hicho licha ya kuwa ni rahisi kukipika, lakini pia kina ladha ya kipekee.
“Bei ya dagaa kwa rejareja tunashukuru imeshuka na sasa tunamudu kula kama kitoweo lakini pia kuwatumia ndugu zetu waishio nje ya mkoa huu kama zawadi,” alisema mkazi wa mjini hapa, Agness Mathew.

chanzo habari leo

No comments